Home Makala WAKUU WETU WAKO TAYARI KULIPA GHARAMA YA UZALENDO?

WAKUU WETU WAKO TAYARI KULIPA GHARAMA YA UZALENDO?

463
0
SHARE
Samuel Langhorne Clemens

NA OVERCOMER DANIEL


NINATAKA kuandika kama raia wa Tanzania, mimi ni raia wa Tanzania, na kwa mujibu wa Katiba yetu, niko huru kusema. Ninataka kutoa maoni yangu, ninataka kupendekeza, kushauri na kukosoa ikibidi. Nasukumwa na uzalendo kwa nchi yangu!

Ninaandika huku nikisukumwa na mapenzi ya dhati ya kabisa kwa nchi yangu, na shauku kubwa ya kufikia ndoto ya kuwa taifa ambalo kila raia wake anafurahia na kujivunia kuishi ndani yake.

Miongoni mwa mambo ambayo huwa yananifurahisha sana ninapowasikiliza viongozi katika nchi hii, ni pale mmoja anaposimama na kuhutubia na kisha kutoa wito wa Watanzania kuwa wazalendo kwa taifa lao.

Huwa nafurahishwa na kufarijika na viongozi wa siasa, serikali na mamlaka mbalimbali za nchi yetu wanapohimiza wananchi kuwa wazalendo kwa Taifa hili, nasema kweli kutoka moyoni, huwa inanipendeza kwelikweli.

Lakini furaha yangu huwa haidumu sana pindi ninapojikuta nimezama kwenye dimbwi zito la tafakuri juu ya mambo yafuatayo;

  1. Je, uzalendo ni nini hasa?
    2. Je, viongozi au watawala wetu wanaelewa hasa maana ya neno uzalendo?
  2. Je, wanaohubiri uzalendo wana udhu kuwataka raia wawe wazalendo? Wanastahili kuhimiza hayo?

Uzalendo katika tafsiri rahisi na ya kawaida kabisa ni ile hali ndani ya mtu kuithamini na kuipenda nchi yake. Mambo haya mawili (kuipenda na kuithamini nchi) kutampelekea mtu huyu daima kuweka maslahi ya nchi/taifa lake mbele kwa gharama yoyote iwayo.

Na niseme pia kwamba, uzalendo si maneno mdomoni, uzalendo si majigambo, mbwembwe, madoido, tambo na mikogo kujaribu kushawishi watu waamini kuwa unaipenda nchi yako, bali ni hali inayokaa ndani ya mtu hata kama wanaomzunguka hawajamsikia akitamka kwamba anaipenda nchi yake.

Hali ya ndani ya vilindi vya moyo wa mtu ya kuwa tayari kujitoa muhanga kwa ajili ya kulinda hadhi, heshima, mali na usalama wa nchi yake, ndiyo hufanya mtu awe mzalendo, hata kama hajawahi kusikika akitamka kuwa yeye ni mzalendo kwa kinywa chake.

Niseme wazi kwamba, kwa viongozi wetu, wenye mamlaka na madaraka wetu, serikalini, vyama vya siasa, idara mbalimbali, mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi wanapohubiri uzalendo lazima wawe wameazimia wao ndani kuwa wazalendo kwelikweli.

Ni ndoto, narudia tena, ni ndoto za hovyo sana kutazamia kwamba nchi hii itakuwa na watu wazalendo kwa matamko na wito unaotolewa majukwaani. Ni lazima tuamue, na wa kwanza wawe wale waliopewa dhamana ya kusimamia usalama na ustawi wa mali na raia wa nchi hii.

Nitatoa mfano hapa; nchi yetu ina rais, makamu wa rais, waziri mkuu, mawaziri, spika wa bunge na wasaidizi wake, wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa, wakurugenzi wa taasisi na mashirika mbalimbali ya umma nk nk!

Kama rais na wasaidizi wake (serikali), spika na wenzake, kama Mkuu wa Majeshi na jeshi lake, kama IGP na wenzake, kama Jaji mkuu na wenzake na mamlaka nyingine kama TRA, TPA, mashirika mwengine kama hifadhi za taifa na kwingine kote hawatajua maana ya uzalendo, hawatakuwa wazalendo, na kama watakuwa wanahimiza uzalendo mbele ya kamera na vipaza sauti ili warushwe kwenye vyombo vya habari, kamwe wasitazamie nchi hii kufikia ndoto za maendeleo.

Tutakusanya kodi nyingi, tutaweka sheria nyingi, tutaweka juhudi nyingi sana ili tuendelee kama taifa, lakini bila uzalendo tutakuwa tunafanya mzaha tu. Tutakuwa taifa la kulaumiana, kushutumiana, kuhukumiana, kutukanana, kutafutana uchawi, lakini uzalendo ni kitu muhimu sana!

Kuna wakati nawaza kwamba nchi si kwamba haina viongozi watendaji wenye weledi, bali tuna viongozi au wenye mamlaka waliokosa uzalendo.

Fikiria wanaogawana pesa za EPA, Escrow, Kagoda, huku hospitali zetu zikiwa hazina dawa, vifaa tiba, shule hazina madawati, hazina majengo ya kusomea, walimu wanadai mishahara, madaktari wanadai mishahara, barabara hazipitiki, nk, ni wasomi, ni viongozi waandamizi, lakini wanatoa wapi unyama huu? Uzalendo!

Nawaza, mtu anaulizwa kwamba ana tuhuma za kuficha mamilioni ya pesa nje ya nchi, halafu anajibu kwa dharau na kejeli kuwa “hivyo ni vijisenti tu”, ni msomi na kiongozi mwandamizi, jeuri hii anaitoa wapi kama si kutokuwa na mapenzi kwa nchi na raia wake?

Nadhani tatizo la nchi yetu kwa sasa si kukosa viongozi wenye elimu, maana tunao, ndio hao ambao wanagawana pesa za umma na kuita ni za mboga tu.

Kama kuna kitu namuunga mkono Rais wangu Magufuli ni suala hili la ufisadi, Mungu ampe roho ya uzalendo, asukumwe na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yake, amuepushe na ile roho nyingine inayowatesa baadhi ya viongozi wengi wa Afrika, kufanya mambo kisiasa, bali Mungu ampe roho ya kweli ya uzalendo, na nina hakika atapewa hiyo. Amen!

Hoja yangu kubwa katika makala hii, katika sehemu hii ya kwanza ni kwamba tunapotoa wito wa raia kuwa wazelendo tuhakikishe sisi tuliopewa dhamana tuwe mfano katika maneno na matendo yetu kwa habari ya uzalendo.

Askari wetu wawe wazalendo, wakiwa wazalendo hawataonea watu, watafanya yote kwa kufuata sheria za nchi hii, ili tuwe na taifa lenye furaha badala ya maombolezo. Uzalendo ni zaidi ya kushika mitutu ya bunduki, uzalendo pia ni kutenda haki kwa raia wenzako wa Tanzania ukitumia nafasi uliyo nayo. Vivyo hivyo kwa majaji, mahakimu na wenye mamlaka wengine! Askari wa usalama barabarani wafundishwe uzalendo, wana mengi mapungufu kwa sababu ya kukosa uzalendo.

Viongozi na wenye mamlaka wanapohimiza uzalendo wawe tayari kukabiliana na gharama za uzalendo wananchi wakiamua kuishi kizalendo. Katika toleo lijalo nitakuja nieleze sababu za kwa nini wanapaswa kuwa tayari kulipa gharama ya uzalendo.

Kwa sababu ni hatari sana wale wanaohubiri uzalendo wanaposhindwa kuelewa au kujua dhana na maana nzima ya uzalendo. Wakishindwa kujua maana ya uzalendo hawawezi kuishi uzalendo, na wakishindwa kuishi uzalendo wale watakaoishi uzalendo watawachukulia kama wahalifu, uzalendo utageuka kuwa uhalifu, uovu, dhambi nk.

Na ndio maana Mwanafalsafa mmoja wa zamani huko Marekani aliyeitwa Max Eastman aliwahi kusema: “Uzalendo ni moja kati ya uhalisia wa mwanadamu usioweza kubadilika, ni mzuri kama utaupenda, lakini ni uovu kama utauchukia”

Ni lazima watawala wetu, viongozi wetu na wengine wote wanaosimamia nchi hii kwa niaba ya Watanzania wengine wajue maana ya uzalendo, wakishajua wajifunze kuupenda uzalendo, wakishaupenda watajikuta tu wanauishi.

Wakifanikiwa kuuishi uzalendo waelewe viashiria vya uzalendo ndani ya mtu au wale wanaowaongoza, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba si wakati wote wale unaowaongoza au kuwasimamia watakuunga mkono. Kuna wakati tunapokosa kuungwa mkono si kwa sababu wanatuchukia, bali ni kwa sababu yale tunayosema au kuyafanya hayana maslahi au wema wowote kwa mustakabali wa taifa letu.

Kwa mfano, ni muhimu viongozi wa serikali kujifunza na kukubaliana na ukweli kwamba kama tunahimiza na kuhamasisha wananchi kuwa wazalendo, basi tuwe na uhakika kwamba watakapoamua kuwa wazalendo halisi kuna mambo tutapishana mitazamo, muono na misimamo kwa maslahi ya taifa.

Kwamba si kila wakati wataunga mkono maamuzi, maazimio, mipango au utendaji wa serikali. Wapo wanaopinga serikali si kwa sababu ni wazalendo, bali wahalifu na wasiolitakia mema taifa hili, lakini wapo wanaoipinga serikali kwa msingi kwamba watendaji wa serikali kwa ngazi yoyote si miungu au malaika kwamba hawawezi kukosea au kughafilika, wanapokosea kuna wale ambao wataipinga serikali.

Mwandishi wa Kimarekani, Samuel Langhorne Clemens, maarufu kama Mark Twain, aliandika akisema uzalendo ni kuiunga mkono nchi yako wakati wote na kuiunga mkono serikali yako pale inapostahili.

Kwa maslahi ya nchi, wapo watakaoipinga serikali, lakini hawataipinga tu kama wehu na mazuzu, wataipinga kwa hoja wakieleza na kuonyesha madhara au hasara ya kile wanachokipinga kwa nchi. Uzalendo ni gharama, lakini ni nyenzo muhimu ya kujenga taifa imara, zuri na lenye watu wenye furaha na kujivunia nchi yao!

+255 672663482