Home Makala Walemavu wa akili wanapaswa kuhudumiwa

Walemavu wa akili wanapaswa kuhudumiwa

3179
0
SHARE

Josephine Bakhita, (katikati), akiwa na raia wa Uholanzi waliotembelea taasisi hiyo mjini Morogoro hivi karibuni.

NA VICTOR MAKINDA

Upo ulemavu wa aina nyingi. Ulemamavu wa akili ni moja ya aina mbaya kabisa za ulemavu.  Wapo wanaopata ulemavu wa akili kwa ama kuzaliwa au hupata ulemavu huo wakati wa hatua za ukuaji. Yapo magonjwa mengi yanayoweza kusababisha kupata ulemavu wa akili. Magonjwa kama polio, malaria kali na kifafa husababaisha ulemavu wa akili kwa watoto.

Kundi hili la walemavu wa akili hususani watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi wao na wazazi wao kwa ujumla  kama zinavyobainishwa na Mama Josephine Bakhita, Mkurugenzi wa kituo cha kulelea, kutoa elimu na marekebishao kwa watoto wenye ulemavu wa akili na viungo cha Erick Memerial Foundation for Education Rehabilation of Disabled (EMFERD).

Mama Josephine Bakhita ambaye ni mwasisi wa taasisi  Amani Center ya mjini Morogoro taasisi inayojihusiahsa na kulea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo, ambaye  kwa sasa ameasisi  na kuindesha  taasisi ya EMFERD, anasema kuwa watoto wenye ulemavu wa akili ni kundi lililotengwa na jamii hali inayosabaisha madhira makubwa kwa kundi hili.

Anasema watoto walemavu wa akili si tu hutengwa na jamii bali pia hutengwa  hata na wazazi wao hasa akina baba.  Anaeleza kuwa baadhi ya wanaume huona kuwa ni mzigo mzito kulea  wataoto wenye ulemavu na kuna wakati huwakimbia wake zao kwa kudhani kuwa tatitizo la ulemavu wa akili la mtoto linasababishwa na mama.

Mama Josaephine Bakhita anakwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa utafiti alioufanya kwa muda mrefu akiwa katika kazi hiyo ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa akili na viungo, amebaini kuwa familia nyingi zenye watoto wenye ulemavu wa akili na viungo, zinakabiliwa na umaskini wa kipato kwa kuwa muda mwingi wazazi hao hutumia kuwaangalia watoto na kutopata wasaa wa kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Hivi karibuni Taasisi ya  EMFERD, ilipata ugeni kutoka Uholanzi. Wageni hao licha ya kutembelea kituo cha EMFERD pia walitembelea baadhi ya kaya zilizo na watoto wenye ulemavu wa akili na viungo katika kijiji cha Makuyu, Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro. Huko walipata nafasi ya kujionea hali halisi ya maisha wanayoishi watoto wenye ulemavu wa akili na viungo pamoja na familia zilizo na watoto wenye matatizo hayo. Wageni hao walizungumza na wazazi na kubadilishana uzoefu wa namna nzuri ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa akili na viungo huku wakisistiza kuwa mazoezi ya viungo yanawezaa kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za ulemavu wa viungo kwa watoto.

Jacques Vissers, aliyejitambulisha kuwa anafanya kazi katika moja ya taasisi za kuwahudumia walemavu nchini Uholanzi kwa upande wake yeye aliifananisha hali ya kaya zilizo na watoto wenye ulemavu nchini na hali kama hiyo nchini Uholanzi. Jacques anasema kuwa nchini Uholanzi walemavu wanaishi katika vituo maalumu vya kuwalelea na wakiwa huko wanapatiwa mafunzo na stadi za maisha huku wakiwa na ustawi mzuri.

Anasem kuwa walio wengi wanajimudu kiuchumi kwa kuwa wanafundishwa shughuli mbali mbali za uzalishaji mali hususani kazi za mikono, kulima bustani za mboga hata ufugani wakiwa chini ya uangalizi wa watoa huduma ambao hulipwa na serikali. Anaishauri serikali ya Tanzania kuanzisha vituo maalumu vya kuwalelea watoto wenye ulemavu wa akili ili kuondoa mzigo huo kwa familia masikini ambazo kwa kuwa na changamoto ya kuwalea walemavu umaskini wa kaya hizo huongezeka.

Kwa upande wake Lisa Holtman, ambaye aliwahi kuishi nchini na kufanya kazi za kujitolea katika kituo cha Amani cha mjini Morogoro, yeye anashauri kuwa kazi ya kuwalea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo isiachwe kufanywa na familia na taasisi binafsi.

Lisa anashauri serikali kutenga kiwango fulani cha fedha kutoka kwenye kodi inayokusanywa au kuanzisha kodi na tozo mpya ambayo moja kwa moja itakuwa inakwenda kuwahudumia watoto wenye ulemavu wa akili na viungo pamoja na kuimarisha ustawi wa familia zao.

Anatolea mfano katika sekta ya utalii ambayo inaonesha kuingiza fedha nyingi za kigeni, Lisa anasema kuwa serikali inaweza kutenga asilimia moja ya fedha zinazoingia katika sekta ya utalii ikatumika kuwahudumia walemavu hususani watoto wenye ulemavu wa akili na viungo.

Ria Vissers,mgeni mwingine kutoka kutoka Uholanzi, yeye alieleza kuwa nchini Uholanzi wazazi wanaruhusiwa kutoa mimba ikiwa itabainika kuwa mimba hiyo mtoto ni mlemavu.  Anasema kuwa kuliko mtoto mlemavu kuzaliwa na kuachwa  anateseka kwa kukosa mahitaji muhimu na ustawi wake, anashauri serikali ya Tanzania kama inashindwa na kubaini kuwa mzigo wa kuwalea walemavu hasa wa akili ni mkubwa basi ikapitisha sheria ya kuruhusu kutoa mimba ambazo zinabainika kuwa na watoto walemavu kama inavyofanyika nchini mwao.

HALI HALISI YA WALEMAVU WA AKILI

Kundi la walemavu wa akili ni kundi linalohitaji uangalizi maalumu. Ulemavu wa akili ni tofauti na ulemavu wa aina nyingine. Kiziwi na bubu wanaweza kuongea na kutoa hisia zake kwa njia ya ishara. Ulemavu wa miguu, mikono na viungo vingine vina unafuu kulinganisha na ulemavu wa akili. Walemavu wa ngozi wana vyama vyao  kama ilivyo walemavu wa aina nyingine. Tatizo linakuja kwa ulemavu wa akili.

Meler Vissers anataja ulemavu wa akili kama aina mbaya kabisa ya ulemavu.Anasema kuwa katika ulemavu wa akili kuna ambao wanaweza kujifunza taratibu, lakini pia kuna ambao wanatumia muda mrefu sana kujifunza na kuelewa jambo hivyo inapaswa kuwa mstahimilivu mno kutoa mafunzo kwa kundi hili. Licha ya ustahimilivu bali pia hugharimu muda na rasimali fedha kutoa mafunzo kwa kundi la walemavu wa akili ili nao waweze kuwa na stadi za maisha na kuchangia pato.

Mwisho analitaja kundi hili la walemavu wa akili kama kundi ambalo haliwezi kujisemea na sharti lipate huruma kutoka kwa asiye na ulemavu wa akili kulisemea kwa kuwa kwao kufikiri  ni tatizo na kuwasilisha tatizo pia ni tatizo. Hili ni kundi la wasio na sauti.

Ukweli Ulivyo  walemavu wa akili wanapaswa kutazamwa kwa jicho la hisani na huruma huku serikali ikielekeza nguvu katika kulihudumia kundi hili sambamba na watu binafsi  na taasisi mbali mbali kwa lengo la kuleta ustawi wa walemavu wa akili hususani watoto.