Home Maoni Walimu wamegeuzwa mabuzi ya kuchunwa!

Walimu wamegeuzwa mabuzi ya kuchunwa!

2436
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA

Mitaani tumezoeshwa kuambiwa dhana ya kulichuna buzi. Mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka 2000 neno ‘kulichuna buzi lilikuwa mashuhuri sana.

Neno hilo lilitumika kuwataja wanawake wanaojiingiza kwenye mapenzi na wanaume wasiowapenda kwa madhumuni ya kujipatia kipato. Vilevile kulikuwa na wanaume waliojiingiza kwenye mapenzi na wanawake wenye uwezo kiuchumi ili kujipatia kipato.

Neno ‘kulichuna buzi’ lilishika kasi kipindi hicho. Likawa linatumika kuwanga watu wote wanaojihusisha na mapenzi bila kuwapenda wapenzi wao.

Aidha, lilitumika kwa wale waliokuwa wakishinda baa kuvizia wanaume wenye fedha ili wajipatie angalau bia moja na fedha za matumizi. Ndiyo kulichuna buzi huko.

Na kwa kawaida tungeweza kusema tabia ya namna hii inaweza kutumia kwa taasisi yoyote ambayo inawatumia vibaya wafanyakazi wao. Kwamba inawafanyisha kazi nyingi na ngumu lakini malipo yao ni madogo wala hayakidhi mahitaji ya wafanyakazi husika.

Kwa mfano, taasisi moja inavuna taifa kubwa na kuhakikisha inapandisha mapato yake kwa kuwafanyisha kazi nyingi na ngumu wafanyakazi ao. Lakini hakuna kinachowanufaisha wafanyakazi hao zaidi ya kuambulia malipo yasiyo na cha mno.

Dhana hiyo inalingana na ile ya mtu kupata fedha bila kuvuja jasho, kwamba anachuma fedha za mtu mwingine pasipo kujishughulisha. Mtu wa namna hii anamchuna mwenzake kama buzi. Kwahiyo anayechukuliwa fedha ndiyo huitwa buzi. Ni buzi linalochunwa.

Katika mantiki hiyo ndipo utakutana na serikali zetu namna zinavyowatumia walimu kama mabuzi ya kuyachuna fedha pasipo kujali maslahi yao.

Imezoeleka kwa baadhi ya watu duniani kote kuwa serikali hujijiengea ‘fikra’ kwamba ni za kitakatifu. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopo kwenye dunia hiyo na serikali inajidhania yenyewe kuwa ya ‘kitakatifu’. Serikali inaamini ili kushughulikia matatizo ya wanajamii basi ni kuwashughulikia pale wanapokosea.

Ilhali wenye madaraka ya kuwashughulikia wadogo wanapokosea, wenyewe hawajishughulikii kutokana na uozo wao. Ndiyo! Kwa kawaida wadogo ndiyo hukosea na badala yake dhana ya kuwa serikali haikosei imekuwa kubwa mno. Serikali ikihojiwa ama kukosolewa juu ya uamuzi au makosa kadha wa kadhaa utasikia unaambiwa wewe mchochezi.

Mathalani kwa miaka nenda rudi, sekta ya elimu imekuwa kama shamba la bibi. Walimu wamekuwa kama mabuzi yanayochunwa tu. Walimu wengi katika utumishi wa umma wamekuwa na madai mazito na sugu kwa serikali kwa miaka mingi tu.

Kuna malimbikizo, uhamisho, makato, na madeni mengi kuliko kawaida. Lakini miaka yote hiyo kwa serikali inajidhania kuwa walimu ndiyo wenye matatizo huku yenyewe iwachuna kama mabuzi.

Walimu ndani ya utumishi wa umma wamegeuzwa shamba la bibi. Wanageuzwa watwana. Wamegeuzwa kuwa watu ambao sauti zao hazifiki kokote, na kila mwaka wanatumbuizwa kwenye sherehe za Mei Mosi.

Ikifika Mei Mosi walimu wanakuwa na matumaini kweli kweli! Lakini utekelezaji wa matumaini yao ni bure tu. Wataekelezwa na nani ikiwa serikali inaamini walimu hawako sahihi kudai haki zao na kwamba inawachukulia kama wakosaji?

Kuna wakati malalamiko yanapotolewa na Chama cha Walimu nchini huwa nayaona kama kero tu. Ni usumbufu ambao unatuelemea sisi wana jamii na kudhani TUCTA ni walalamishi. Kumbe wanakwepa kuwa mabuzi.

Ukweli ni kwamba TUCTA wanakuwa na hoja nzuri tu. Wanadai malimbikizo ya wateja wao. Wanadai haki za wateja wao. Lakini hakuna kipindi ambacho walimu wamewahi kutekelezewa madai yao tangu utawala wa awamu ya kwanza ya Julius Nyerere, awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa, awamu ya nne ya Jakaya Kikwete hakuna cha mno.

Na sasa wapo kwenye awamu ya tano, ambayo wamejibiwa swali lao walilouliza katika awamu ya nne; Shemeji (Rais Kikwete) unatuachaje? Jawabu alililokuja nalo Kikwete ni kumkabidhi nchi Mwalimu mwenzao, John Magufuli.

Naye Magufuli amkamchagua Mwalimu mwenzake kuwa waziri mkuu, Kassim Majaliwa. Rais na waziri mkuu wote wameoa wanawake walimu. Makamu wa Rais, Mama Samia ni mwalimu pia kitaaluma. Utaona serikali ya awamu ya tano ni ya walimu. Hata hivyo utekelezaji wa madai ya walimu hautazingatia watawala hao kuwa walimu.

Ipo mifano ya dhahiri ambayo inaudhi kwenye sekta ya umma hususani Walimu. Kuna masimulizi ya kuudhi na kukera mno ambayo yanawahusu walimu. Wapo walimu watiifu, wapo wakaidi ambao wanaachana na ajira za serikali.

Fuatilia mfano huu kutoka kwa rafiki yangu; Kuna walimu huko mkoani Shinyanga wanalalamikiwa kuacha kufundisha na kwenda kufanya kazi ya kuendesha Bodaboda na upigaji wa picha kwenye sherehe kwa ajili ya kujiongezea kipato cha kukidhi kwenye familia zao.

Serikali ya mkoa wa Shinyanga tayari imetoa tamko juu ya sakata hilo. Kwa kuanzia imeomba majina ya walimu wanaojihusisha na shughuli hizo mbadala na kuwataka waamue kuendelea na ualimu au kufanya kazi ya bodaboda na upigaji wa picha kwenye sherehe.

Hapa kosa ninaloliona ni walimu kuacha vipindi na kuingia mtaani kusaka noti. Lakini kujiongezea kipato kwa njia za halali sioni kama ni kosa. Hautakuwa uungwana kuwazuia kutafuta malisho zaidi ambayo yanachangia kodi kwa njia nyingine badala ya utumishi wa umma peke yake ambako wamegeuzwa mabuzi ya kuchunwa fedha zao tu na kujaziwa ahadi zisizotekelezeka.

Lakini tujiulize, kwanini walimu hao wamefikia hatua hiyo? Bila shaka ni kutokana na maslahi duni wanayopata katika kazi zao, pamoja na kugeuzwa shamba la bibi ambapo wanachunwa kama mabuzi kuliko wanachoingiza.

Naamini watu hawa muhimu wakiboreshewa kipato watatumia muda mwingi zaidi kwenye ajira zao. Kuwazuia kutafuta kipato mbadala bila kutatua changamoto zao ni kuwaonea na kuwafanya watafute mbinu nyingine wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi ambazo zinaweza kuwa hatari zaidi.

Walimu kama binadamu wanazo familia. Wana ndugu, wake, waume, wapenzi, wategemezi na kadhalika. Wakati wanaamini kupandishwa madaraja na kuongezewa mishahara itakuwa njia nzuri wamejikuta wakibanwa kila hatua ya nyongeza ya mishahara yao.

Kila hatua ya kupanda daraja ndipo kodi inapokuwa zaidi. Kibaya zaidi walimu hawajawahi kuheshimika kwa kutekelezewa madai yao. Wangeheshimiwa wangelipwa madeni yao sugu wanayodai.

Lakini hadi sasa wamegeuzwa kuwa mabuzi ya kuchunwa. Haifurahishi, lakini ni jukumu lao kudai haki zao na kuacha kuchunwa kama mabuzi. Sijui serikali haioni fedheha, kila mwaka haitekelezi madai ya walimu, huku ikijenga dhana kuwa walimu ni wakosaji tu.