Home Maoni WALIMU, WAZAZI JILINDENI DHIDI YA WAKUU WA WILAYA WANAOWASHAMBULIA

WALIMU, WAZAZI JILINDENI DHIDI YA WAKUU WA WILAYA WANAOWASHAMBULIA

856
0
SHARE

“Mtu yeyote ambaye anafanya shambulio linalosababisha madhara mwilini, atakuwa anatenda kosa na atawajibika kwa kifungo cha miaka mitano jela”  [Kifungu cha 241- Kanuni ya adhabu]

” Kwa mujibu wa masharti ya kanuni hii, kila mtu ana haki ya:(a) kujilinda yeye binafsi au mtu mwingine dhidi ya kitendo chochote ambacho kiko kinyume na sheria au shambulio au utumiaji nguvu dhidi ya mwili.” [Kifungu cha 18A(1)(a)-Kanuni ya adhabu].

“Kila mtu ambaye anajua kwamba mtu fulani anaazimia kutenda au anatenda kosa, na akashindwa kutumia kila njia inayofaa ya kuzuia utendaji au ukamilishaji wa kosa, atakuwa anatenda kosa” [Kifungu cha 383-Kanuni ya adhabu].

“Kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 18A, mtu hawezi kuwajibika kijinai kwa kitendo alichokifanya wakati anajitetea au kumtetea mtu mwingine au kutetea mali kwa mujibu wa masharti ya kanuni hizi” [18-kanuni ya adhabu]

Hivi karibuni kumekuwa na matukio yasiyokuwa ya kawaida ya wakuu wa wilaya kuwapiga wazazi au walimu. Mfano wa matukio hayo ni pamoja na lile la mkuu wa wilaya ya Nchemba, Simon Odunga kumpiga Chindika Pingwa ambaye ni mzazi mpaka kumsababishia jeraha lilopelekea kushonwa nyuzi tisa.

Matukio mengine yameripotiwa kutokea kwa nyakati tofauti Wilayani Hai na Arumeru kwa wakuu wa wilaya wa maeneo hayo kuwacharaza viboko walimu.

Mambo haya sio sawa bila kujali kama waalimu walikuwa na makosa au lah. Zipo taratibu za kisheria za kuwachukulia hatua wote wanaokosea na sio kuwapiga.

Kwa mkuu wa wilaya kufanya kitendo hicho cha kushangaza ni kuvunja sheria za nchi na zile za kimataifa.

Katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania chini ya ibara ya 12 na 13 zimeanisha kuwa binadamu wote ni sawa mbele ya sheria na wanapaswa kuheshimiwa kwa utu wao.

Kwa wakuu wa wilaya kuwachapa waalimu na wazazi tena hadharani hasa mbele ya watoto wao na wanafunzi wao, ni kuvunja utu wao. Ni kujichukulia sheria mkononi kwa kudhani kwamba, kuwa mkuu wa wilaya unakuwa tofauti na wengine kwa kiwango cha kujichukulia sheria mkononi.

Ibara ya 26 ya Katiba ya nchi yetu, inatoa wajibu wa kila mtu kuheshimu katiba ya nchi na sheria zote za Tanzania. Wakuu hawa wa wilaya, wao bila ajizi wanavunja sheria za Tanzania.

Kama hiyo haitoshi, ibara ya 107A imetoa mamlaka kwa mahakama kuwa ndio chombo cha utoaji haki nchini. Maana yake ni kwamba, yeyote anayemkosea mwingine au anayevunja sheria za nchi anapaswa kufikishwa mahakamani kwajili ya kujibu mashitaka.

Kwa niaba ya TSNP, napenda kuwashauri waalimu na wazazi kujilinda kwa nguvu stahaki dhidi ya uvunjifu wa sheria za nchi. Nawashauri na wanafuzi pamoja na raia yeyote ambaye atashuhudia kitendo kingine cha aina hiyo, kutovumilia uvunjifu wa sheria kwani ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 383 cha Kanuni ya adhabu.

Hawa wakuu wa wilaya wanaojifanya vichaa, wanatakiwa kuzuiwa kutovunja sheria za nchi hii. Tusipowazuia wataendelea kuumiza watu kwa kutafuta sifa za kijinga. Hii ya kuwazuia ni njia ya kwanza kabla ya kufika mahakama either kwa sisi kuwashitaki au kwa wao kutangulia. Tusimame kidete kulinda sheria zetu.

Bob Chacha Wangwe
Mkurugenzi wa sheria TSNP