Home Uchambuzi Afrika Waliostaafu wawania upya madaraka Madagascar

Waliostaafu wawania upya madaraka Madagascar

3649
0
SHARE

Rais wa Madagascar na mgombea wa urais katika uchaguzi Hery Rajaonarimampianina.

NA HILAL K SUED NA MITANDAO

Madagascar, nchi ya kisiwa kusini mwa Bahari ya Hindi inatarajia kufanya uchaguzi wake wa urais Novemba 7, na uwezekano wa marudio Desemba 19.

Katika uchaguzi wa 2013 jumla ya wagombea urais 33 walishiriki – ilikuwa ni rekodi kwa nchi hiyo. Kulikuwapo changamoto nyingi – kama vile majina ya watu 33 na picha zao wataeneanea vipi katika karatasi moja ya kura? (karatasi ya saizi ya A3 ilitumika).

Baada ya uchaguzi wa marudio kwa wagombea wawili wa juu Hery Rajaonarimampianina ndiye aliyeibuka mshindi. Hata hivyo haikushangaza wengi safari hii ilipotangazwa watu 36 wamepitishwa kugombea nafasi hiyo.

Hali kadhalika haikushangaza wengi pia pale baadhi ya wagombea hao ni wale wale wa kila mara. Rais aliye madarakani Rajaonarimampianina ameomba kuchaguliwa tena, wakiwemo pia marais watatu wa zamani: Didier Ratsiraka, mtawala wa kibabe kuanzia 1975 hadi 1993, na tena 1997 hadi 2002;

Marc Ravolamanana, aliyechaguliwa kuanzia 2002 hadi alipopinduliwa mwaka 2009, na Andry Rajoelina, aliyeyaongoza mapinduzi hayo ya 2009 na ambaye alikaa madarakani kama rais wa mpito hadi 2013.

Kwenye karatasi ya kura hao wanaungana na wanasiasa wengine mbali mbali, maafisa wa jeshi, wafanyabiashara na watu wengine mashuhuri katika jamii.

Katika kundi hilo pia wamo mawaziri wakuu watatu wa zamani: Jean Ravelonarivo (2015-16), Jean Omer Beriziky (2011-14) na Olivier Mahafaly (2016-18), pamoja na mwanamuziki mashuhuri wa ‘pop’ – Dama na mchungaji André Mailhol. Kuna wanawake watano tu katika orodha hiyo.

Kwa kiawango fulani, idadi kubwa hii ya wagombea ambayo haijawahi kutokea pia inaendana na utamadauni wa chaguzi za nchi hiyo. Watu wengi huteuliwa kugombea, na wale wanaoshindwa katika duru la kwanza huamua kuwaunga mkono mkono wale wawili waliomaliza juu katika tarajio la kupata masilahi ya kisiasa endapo mgombea wao atashinda na kuwa rais wa nchi.

Aidha inasemekana hayo ni “mahesabu ya kisiasa.” Kwanza wapigakura wengi hupiga kura kwa misingi ya kikabila na hawa ”washindwa” hulipwa fedha au ahadi hata ya uwaziri iwapo watawahamsisha wanachama wao kuwapigia kura.

Na kwa wafanyibiashara wakubwa ni suala la kimasilahi ya biashara zao. Mfanyibiashara akigombea urais, ina maana kwamba hawezi kulazimishwa kufadhili kampeni za wagombea wengine ambazo hugharimu fedha nyingi.

Msimu wa kampeni nchini Madagascar ulianza rasmi mapema mwezi huu (Oktoba), lakini wagombea wengi tayari walikuwa barabarani kwa miezi kadha wakinadi sera zao. Hakuna sheria nchini humo zinazoratibu gharama za kampeni, suala ambalo limeelezwa na of Mkurugenzi wa Shirika la Kupambana na Rushwa Duniani (Transparency International (TI) nchini humo Ketakandriana Rafitoson kuwa ni tatizo kubwa kwani vianzo vya gharama za kampeni ya vyama vingi huwa havijulikani.

Kwa mfano utafiti uliofanywa 2016 uligundua kwamba kampeni za rais wa sasa Hery Rajaonarimampianina katika uchaguzi wa 2013 zilikuwa za gharama kubwa sana haijapata kutokea duniani kote. Mwaka huo Rajaonarimampianina alitumia Dola za Kimarekani 21.5 kwa kila kura moja aliyoshinda, ikizidi hata za Hilary Clinton na Donald Trump katika uchaguzi wa 2016.

Hivyo wengi wanaona mpambano wa safari hii utakuwa ni mpambano wa nguvu ya fedha – kwani wagombea wote watatu wakubwa – Rajaonarimampianina, Rajoelina na Ravalomanana wana nguvu kubwa ya kifedha.

Katika kusaidia kuleta uwazi na usawa katika gharama za kampoeni, kutokana na rushwa kutumika sana katika kampeni, kundi moja la asasi za kiraia limeanzisha Uratibu wa Tabia Njema katika uchaguzi (Charter of Good Behaviour) ambapo wagombea urais wanatakiwa watangaze fedha na mali zao kwa taasisi ya kuzuyia rushwa nchini humo, kwa kutangaza tarakimu halisi na wapi walikozipata mali hizo.