Home Latest News Wamorocco, Zamalek hapatoshi fainali CAF

Wamorocco, Zamalek hapatoshi fainali CAF

2632
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

MCHEZO wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirisho Afrika utachezwa mwishoni mwa wiki hii nchini Morocco, ambapo Zamalek watakuwa ugenini dhidi ya RS Berkane.

Huo ni mwendelezo wa ubabe wa mataifa ya Kiarabu katika soka la Afrika kwani tangu mwaka 2004, ni mara mara tatu pekee kwa walau moja kukosa hatua ya fainali.

Mshindi wa mtanange huo atasubiri hadi wiki moja baadaye, siku ambayo timu hizo zitarudiana kule Misri na matokeo ya jumla ndiyo yatakayoamua bingwa wa michuano ya mwaka huu.

Zamalek walifika fainali kwa kuwaondosha wababe wa soka la Tunisia, Etoile du Sahel, baada ya suluhu iliyotanguliwa na ushindi wa bao 1-0.

Baada ya kuwasukuma nje Watunisia hao, kocha wa Zamalek raia wa Uswis aliyewahi pia kuinoa Tottenham, Basel na VfB Stuttgart, Christian Gross, alisema:

“Tulionesha kiwango kizuri katika ulinzi dhidi ya Etoile du Sahel. Mabeki wetu walikua kama simba na waliweza kutibua mipango yote ya mashambulizi ya timu ya Tunisia. “Tunastahili kuwa fainali. Tulicheza vizuri…”

Matokeo hayo yalikuwa ni kisasi kwa Zamalek dhidi ya Etoile du Sahel kwani haijasahaulika kuwa zilipokutana fainali ya michuano hiyo mwaka 2015, Mafarao hao waliambulia patupu, wakilishuhudia taji likienda Morocco.

Hata hivyo, mabingwa hao mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek, watawavaa RS Berkane wakiwa na morali ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho.

Wakati huo huo, wanatambua haitakuwa kazi rahisi kwani RS Berkane, ambao walitinga Ligi Kuu ya Morocco mwaka 2012 hawajawahi kuchukua ubingwa nchini humo lakini waliwatoa nishai wakali wa soka la Tunisia, CS Sfaxien, katika hatua iliyopita ya nusu fainali.

CS Sfaxien ‘Juventus ya Uarabuni’, moja kati ya timu tishio Afrika ikiwa imeutwaa mara tatu ubingwa wa Kombe la Shrikisho, ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwao, Tunisia.

Wakijua wameshatanguliza mguu mmoja fainali, walikumbana na kichapo cha mabao 3-0 kule Morocco, hivyo safari yao mwaka huu ikaishia hatua ya nusu fainali.

Katika hatua ya makundi, RS Berkane ilimaliza kileleni mwa Kundi A, huku ikiwapiku mabingwa watetezi msimu huu, Raja Casablanca, walioshindwa kutinga 16 bora.

Wakati hatua ya robo fainali ikiwashuhudia wakiitoa Gor Mahia ya Kenya kwa kichapo cha jumla ya mabao 7-1, wenzao Zamalek waliwang’oa Hassania Agadir.

Ni kwa mazingira hayo basi, Zamalek si wageni huko Morocco kwani katika mchezo wa kwanza wa robo, ilikwenda nchini humo na kutoa suluhu, kabla ya kutinga nusu kwa bao 1-0 pale Misri.

Aidha, kwa mechi tano zilizopita katika mikikimikiki ya Kombe la Shirikisho, RS Berkane wameshinda tatu na kufungwa mbili, wakati Zamalek wameibuka na ushindi mara moja tu, iliyobaki wakiambulia suluhu.

Kwa mwaka huu, Zamalek watakuwa wakijaribu kuchukua taji lao la kwanza kwa michuano ya kimataifa tangu walipolibeba lile la Ligi ya Mabingwa mwaka 2002.

RS Berkane nao watakuwa na kiu ya kuwa timu ya tano kukipeleka katika ardhi ya Morocco kikombe cha Kombe la Shirikisho.

Lakini, watacheza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Zamalek bila huduma ya kiungo wao hatari, Najji Larbi, atakayekuwa akitumikia adhabu ya katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Sfaxien.

Wakali wengine nchini humo waliowahi kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa nyakati tofauti ni FAR Rabat (2005), FUS Rabat (2010), MAS Fes (2011) na Raja Casablanca (2018).