Home Makala Wananchi waonesha imani na Hospitali za Serikali

Wananchi waonesha imani na Hospitali za Serikali

700
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE

TAFITI zinaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa Watanzania hasa waishio  maeneo ya vijijini wamekuwa na uhakika wa kupata huduma bora zaidi za afya sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Uhakika huo unachangiwa kwa kiwango kikubwa na maboresho ambayo yamefanyika kwenye sekta ya afya, ambapo maeneo mbalimbali kwa sasa yamekuwa yakiangaliwa kwa jicho la tatu na serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa zaidi kwenye uongozi huu wa awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambaye siku chache zilizopita alitimiza mwaka mmoja madarakani.

Hali ya kuboreshwa kwa huduma za afya inaelezwa kuchangiwa zaidi na ongezeko la watanzania ambao awali walikuwa wakipata matibabu kwenye hospitali za binafsi, ambazo zinatajwa kuwa na kiwango bora cha utoaji huduma.

Kurejea huko kwenye kupata huduma katika hospitali zilizo chini ya serikali kunaelezwa kuchangizwa zaidi na mabadiliko makubwa ya mfumo wa kifedha uliopo sasa, ambapo wananchi wengi wamejikuta wakilazimika kuishi kulingana na hali halisi ilivyo.

Ni wazi kuwa kumekuwa tofauti kubwa kwenye afya za wakazi wengi, mfano ni wale wa jijini Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa tafiti iliyofanyika miaka miwili iliyopita na taasisi inayojishughulisha na masuala ya utafiti ya Twaweza ilionyesha kuwa, ni nusu tu ya wakazi wa mji huo ndio wanaochemsha au kutia dawa kwenye maji yao ya kunywa.

Kutokana na hali hiyo, wale wasiotumia dawa hizo hujikuta wakiishia kunasa magonjwa yanayotokana na uchafu kwenye maji ni kama vile kipindupindu na homa ya matumbo. Mgonjwa haya yamekuwa yakiwasumbua Watanzania walio wengi, huku sababu kubwa ikiwa ni ukosefu wa elimu na mazingiza machafu ambayo siyo salama kwa afya ya binadamu.

 

Utafiti huo ulienda mbali zaidi kwa kubainisha kuwa, kaya maskini ndizo zenye uwezekano mkubwa wa kuhudumiwa katika vituo vya afya vya serikali huku zile zenye kipata cha juu zikiishia kwenye hospitali za binafsi.

 

Chanzo cha vituo vya afya vya watu binafsi kujinyakulia umaarufu ilitajwa kuwa ni kutokana na kutoa huduma bora zaidi na pia kutoa huduma inayowaridhisha zaidi wagonjwa. Ambapo katika hatua nyingine ilikuwa ni, wagonjwa 8 katika 10 ambao wanaonesha kuridhishwa na huduma katika vituo vya afya vya watu binafsi, ikilinganishwa na wagonjwa 6 katika 10 wanaosema wameridhika na huduma katika vituo vya afya vya serikali.

 

Sababu nyingine ambayo iliyotajwa na wananchi kama chanzo cha wakazi wengi mijini kupendelea kupata huduma za afya kwenye vituo vya binafsi, ni pamoja na kuwapo kwa mazingira ya kutoa rushwa katika kituo vya serikali na hivyo kujikuta wengi wakilazimika kutafuta huduma kwingine.

 

Hata hivyo, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka huu wa sauti za wananchi uliofanywa na  Twaweza unaonyesha maoni chanya kutoka kwa wananchi juu ya sekta ya afya nchini Tanzania.

 

Utafiti huo ambao umeonyesha kuwapo kuwa na matokeo chanya, uonayesha kuwa kwa sasa ni asilimia 18 ya wananchi wanaoripoti juu ya kuwapo kwa upungufu wa madaktari katika vituo vya afya miezi mitatu iliyopita, ikilinganisha na asilimia 43 walioliona tatizo hili mwaka 2015.

 

Pia katika upande mwingine ni asilimia 73 ya watanzania ambao wanasema kuwa waliheshimiwa ipasavyo mwaka 2016, idadi hii ikiongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2015, pia Usafi kwenye vituo vya afya umeonekana kuimarika zaidi katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016.

 

Hali inayoonyesha kuwa waliolalamikia jambo hili walipungua kutoka watu 3 kati ya 10 mwaka 2015, hadi mtu mmoja tu kati ya watu 10 mwaka huu. Vilevile, malalamiko yahusuyo kushindwa kumudu gharama za matibabu pia yanaonyesha kupungua kwa kiwango kikubwa.

 

Kwani mwaka 2015, asilimia 34 ya wananchi walisema gharama zilikuwa kubwa mno au hawakuweza kulipa gharama hizo huku mwaka 2016, asilimia 19 ndio waliolalamikia gharama hizo, Hata hivyo, upungufu mkubwa wa dawa na vifaa vingine muhimu vya afya bado ni tatizo sugu kwani mwaka 2015, asilimia 53 walisema hivyo ukilinganisha na asilimia 59 mwaka huu.

Matokeo  hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,836 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya Mei 2 na 17  mwaka huu.

Katika kipindi cha mwaka, 2016, asilimia 61 ya Wananchi wameripoti kutibiwa katika vituo vya afya vya serikali, ambapo ni ongezeko la mahudhurio ukilinganisha na asilimia 47 mwaka jana.

Huku upande wa maduka ya dawa, wananchi wanaotembelea maduka hayo wamepungua kutoka asilimia 19 mwaka 2015 hadi asilimia 13 mwaka huu.

Hali hii inaonyesha fika kuwa kumekuwapo na ukomo wa ukiritimba ambao awali ulikuwa ukifanywa na baadhi ya madaktari kwenye hospitali mbalimbali, ambao walikuwa wakiwalaghai wagonjwa kwa kuwambia kuwa dawa hakuna na hivyo wakazitafute kwenye maduka ya jirani kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanajikusanyia pesa hiyo ambayo kwa kawaida ilikuwa ichukuliwe na serikali.

Pia inaelezwa kuwa asilimia 73 ya waliripoti kusubiri kwa muda usiozidi saa moja kabla ya kumuona daktari.  Wengi wao walikiri kupewa maelezo mazuri kuhusu maradhi yanayowasibu (asilimia 92) na kuandikiwa dawa stahiki (asilimia 81),  Asilimia 70 walifanikiwa kupata angalau baadhi ya dawa walizozihitaji kutoka kwenye kituo hicho hicho cha afya.

Utafiti huo pia umeonekana kuungwa mkono na serikali kupitia kwa, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla ambaye anasema kuwa kuwa tafiti hizo zinasaidia Serikali katika kupanga mipango yake thabiti na kufahamu wapi panamapungufu ilikuchukua hatua zaidi.

Huku akisisitiza kujipanga nyema kwa Serikali ya awamu ya tano, katika kuhakikisha kuwa inasaidia wananchi kupitia sera za Afya ambapo kila mwananchi atapata huduma bora za Afya hapa nchini licha ya changamoto zilizopo Wizara ya Afya ipo katika kuboresha mifumo yake mbalimbali ikiwemo suala la bima ya Afya kwa kila mtanzania na huduma bora za Afya kuanzia ngazi ya chini.

“Matokeo haya ya Twaweza yameonyesha matokeo mazuri hii ni pamoja na huduma nzuri ikiwemo lugha ya kiutendaji kwa sasa imekua ni ya kiungwana zaidi tofauti na kipindi cha nyuma. Serikali ya awamu hii ya tano imekuwa ikifanya kazi kwa kasi sana kwa sasa hatukai maofisini zaidi muda wote ni kazi tu,” anasema Dk. Kigwangalla.

Upande wake Afisa mipango wa Twaweza, Nelline Njovu anabainisha kuwa, Twaweza wamezindua matokeo ya utafiti huo ambao uliendeshwa kwa njia ya simu katika mfumo wa Afya ambapo waliangalia mambo mbalimbali ikiwemo juu ya Maboresho ya Huduma za Afya kwa mwaka 2015-16 ambayo yanajumuisha Serikali ya awamu ya tano tokea kuingia madarakani.

“Utafiti wa Sauti za Wananchi wa Twaweza unaonyesha maoni chanya kutoka kwa wananchi juu ya sekta ya afya nchini Tanzania. Kwa mfano, ni asilimia 18 wananchi wanaoripoti kuona upungufu wa madaktari katika vituo vya afya miezi mitatu iliyopita, ukilinganisha na asilimia 43 walioliona tatizo hili mwaka 2015.,” anasema  Nelline.

Mazingira haya huenda yakasawiri vuilivyo kauli ya Dk. Magufuli ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari alitamka kuwa lengo lake ni kutoka kuinyoosha nchi hii.