Home Makala WANAODAI AZIMIO LA ARUSHA NYAKATI HIZI NI VIGEUGEU

WANAODAI AZIMIO LA ARUSHA NYAKATI HIZI NI VIGEUGEU

868
0
SHARE
Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza katika moja ya mikutano ya chama hicho.

NA JOEL NTILE


AZIMIO la Arusha ni moja ya nyaraka muhimu na ya kihistoria kuwahi kutangazwa barani Afrika. Februari 5, mwaka huu, Azimio la Arusha lilitimiza miaka 50 toka kutangazwa kwake mwaka 1967 na Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa Rais wa Chama cha TANU (Tanganyika Africans National Union) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Azimio la Arusha lilikuwa ni tamko la chama cha TANU lililopitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho mjini Arusha, mwishoni mwa Januari mwaka 1967. Mkazo ulikuwa katika ujenzi wa Taifa la kijamaa na kujitegemea.

Hii ilikuwa ni hatua muhimu sana kwa Taifa changa ambalo limetoka kwenye minyororo ya ukoloni mkongwe kuchukua hatua ya kutamka lengo la Taifa, ambalo lilitambulisha Taifa la Tanzania duniani kote juu ya msimamo huo thabiti uliobebwa ndani ya Azimio.

Azimio la Arusha ni Azimio la kimapinduzi lililopinga kila aina ya unyonyaji, matabaka, dhuluma na kuweka miiko ya uongozi kwa viongozi wote wa Serikali na chama kilichoshika hatamu ya uongozi nchini wakati huo.

Huu ndio ulikuwa msimamo wa kitaifa japo ilikuwa ngumu sana kueleweka na wasomi hasa wa mrengo wa kulia, warasimu pamoja na wanasiasa wa wakati huo.

Wakulima, wafanyakazi na walalahoi wa mijini na vijijini waliliunga mkono Azimio hili, kwa imani ya kwamba limekuja kutimiliza uhuru na ukombozi halisi ndani ya Taifa lao ambalo walikuwa wakilitumainia.

Katika kipindi hiko, mara baada ya kutangazwa kwa Azimio, Serikali kwa niaba ya wananchi, iliingilia kati suala la uchumi wa nchi kwa kutaifisha na kumiliki njia zote kuu za uchumi na kupiga marufuku ubinafsishaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya.

Uhai wa Azimio la Arusha kwa minajili ya utekelezaji wake, ulidumu kwa miaka 23 tu. Kimsingi nakubaliana na wachambuzi na wanazuoni mbalimbali, juu ya kifo cha Azimio la Arusha, kwamba azimio halikufa kwa tukio moja tu la mwaka 1990, yaani baada ya kutangazwa kwa Azimio la Zanzibar.

Bali kifo cha Azimio la Arusha kilitokana na mfululizo wa matukio  yaliyotokana na jitihada za warasimu, wasomi waliokuwa wanapinga ujamaa na baadhi ya wanasiasa na mwishowe Azimio la Zanzibar likawa ndio msumari wa mwisho uliopelekea kifo cha Azimio la Arusha mwaka 1990.

Sasa tunazungumzia miaka 50 tangu kutangazwa kwa Azimio la Arusha na miaka 27 tangu Azimio hilo kuzikwa kisiwani Zanzibar na waliokuwa viongozi wetu, huku wakijinasibu kuwa ni waboreshaji wa Azimio la Arusha kutokana na alama za nyakati kubadilika.

Ni dhahiri kwamba katika kipindi hiko chote tokea mwanzoni mwa miaka ya 90 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, ilikuwa ni nadra sana kusikia mazungumzo juu ya Azimio. Hata wale waliokuwa bado wanaliamini Azimio la Arusha walihitaji kuwa uwendawazimu kulizungumzia Azimio kwenye kadamnasi kama alivyosema mwandishi mwenyewe wa Azimio la Arusha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Taratibu walau ikaanza kuingia vichwani mwa watu baada ya kushuhudia madhara ya hatua zinazoitwa za kimageuzi zilizochukuliwa na Serikali yetu mwanzoni mwa miaka ya 90, baada ya kuua Azimio la Arusha ambapo tumeshuhudia kuongezeka kwa kundi kubwa la watu waishio katika umasikini, kuongezeka kwa tofauti ya kipato baina ya wachache walio nacho na wengi wasio nacho, ufisadi na rushwa, uporaji wa ardhi za wakulima vijijini na ubidhaishaji wa huduma za kijamii ambao  umepelekea kundi kubwa la wananchi wasio na kipato cha kukidhi mahitaji kukosa huduma za kijamii.

Uwendawazimu wa kudai Azimio la Arusha, ghafla ukachipukia na kumea mizizi kwa kasi hasa katika taasisi za elimu ya juu kwa kuanzisha makongamano na majukwaa ambayo ilifanyika mihadhara ya wazi juu ya Azimio la Arusha na falsafa za mwasisi wa Taifa letu, Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Hii ilikuwa ni hatua nzuri na muhimu sana ya kukikumbusha kizazi cha sasa historia yake, japo miongoni mwa vijana waliojishughulisha kujielimisha kuhusu Azimio la Arusha walionekana ni wendawazimu walioshikilia ukale usiokuwa na tija katika zama zetu.

Lakini bado haikuwarudisha nyuma wendawazimu hao kuacha kujielimisha na kuhubiri Azimio hilo la haki. Upotofu wa kudhani Azimio la Arusha ni ukale, linatokana na nguvu kubwa ya propaganda iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na wanyonyaji, wakishirikiana na wanasiasa masilahi na viongozi tulionao.

Sasa cheche zinazidi kuwaka kila kukicha, vijana wake kwa waume, wanawehuka na kuwa wendawazimu walioshindikana. Wamejitoa ufahamu na kuanzisha mijadala na madarasa ya kujielimisha  juu ya mustakabali wa Taifa lao na bara la Afrika kwa ujumla na wanalitumia Azimio la Arusha kama mwongozo wa kutimiza ukombozi halisi na uhuru wa bara la Afrika.

Wananchi hususan vijana, wanatamani kuona misingi ya Azimio la Arusha tunairejea kama Taifa, ili tuweze kuyakabili matatizo yanayoikumba jamii yetu hivi sasa.

Lakini ndani yao, wametokea ‘vigeugeu’ wanaojinasibu kuwa nao ni waombolezaji wa kifo cha Azimio la Arusha na wanadai wanalifufua kupitia mbadala wake. Mbadala wenyewe wa Azimio la Arusha unaohubiriwa na ‘vigeugeu’ hao umeondoa misingi ya Azimio la Arusha ambayo ililenga kubomoa unyonyaji, matabaka, dhuluma na kuweka miiko ya uongozi, lakini wao wanapaka rangi unyonyaji, matabaka na dhuluma ili wavuja jasho na wananchi kwa ujumla wasifanye mapinduzi ya kutimiza uhuru na ukombozi halisi.

Vigeugeu kwa kujiita Wajamaa, wanajaribu kuudanganya umma wa wakulima na wafanyakazi, kwa manufaa yao binafsi ya kusaka madaraka ya kisiasa, ni kitu cha hatari sana kwani wasipokemewa wataendelea kulinajisi Azimio la Arusha.

Wendawazimu hawa wanapaswa kupingwa kwa nguvu zote kama vile wanavyopingwa watetezi wa dhuluma dhidi ya wanyonge, ni wajibu wa wendawazimu na wajamaa halisi kuwapinga watu hawa ambao wanaendelea kujiimarisha kupitia propaganda nyepesi zinazouhadaa umma.

Muhimu sasa kwa wakulima, wafanyakazi, pamoja na wavuja jasho wengine kulibeba Azimio la Arusha kama beramu ya mapambano ya kuwania masilahi yao.

Wakulima katika vikundi au vyama vyao, waone haja ya kuainisha misingi ya Azimio katika mapambano yao. Wamachinga na mama ntilie nao waungane huku wakijua mabadiliko ya sheria za miji au kauli za wenye mamlaka kuwa hazitoshi kuwa suluhu ya matatizo yao, kama misingi ya Azimio la Arusha haitarudishwa katika Taifa. Vivyo hivyo, kwa wafanyakazi, wajasiriamali na wasomi.

Mwisho wa siku, kama alivyoamini Baba wa Taifa, nami bado naamini kuwa ipo siku kama Taifa, tutarejea kwenye misingi ya Azimio la Arusha ambayo ni kupinga unyonyaji, matabaka, ubinafsishaji wa huduma za kijamii kama vile elimu na afya na kurudisha miiko ya uongozi katika Taifa letu.

0754255744/0652068952 au mwankina1993@gmail.com