Home Latest News WANAOHAMIA CCM NI NUKSI, AU WATU MBADALA KATIKA UJENZI MPYA WA CHAMA

WANAOHAMIA CCM NI NUKSI, AU WATU MBADALA KATIKA UJENZI MPYA WA CHAMA

5987
0
SHARE

DEOGRATIAS MUTUNGI


Ifahamike kuwa kuhama chama  ni jambo la kawaida katika medali za ushindani wa kisiasa unaokolezwa na demokrasia iliyotukuka. Si dhambi wala kosa la jinai mwanasiasa kuhama chama chake, bali ni sehemu ya haki ya kikatiba na kisheria.  Aidha ni  kipimo cha ukomavu wa demokrasia ya kitaifa na watu wake.

Profesa Fulbert Namwanga anadai kuwa demokrasia ya Afrika haijakomaa, lakini hoja hii inaweza ikajibiwa katika sehemu kuu mbili—mosi, ni kweli kuwa demokrasia ya Kiafrika ina makandokando mengi, pili si kweli kuhama chama kunaweza kukajengwa katika misingi ya ukosefu wa ukomavu wa demokrasia , na demokrasia ya Afrika imekomaa kimazingira eneo na ukanda husika.

Tunapozungumzia ukomavu wa demokrasia Afrika hatuwezi kufananisha demokrasi ya Tanzania na DRC Congo, Zimbabwe au Burundi tusijumuishe madhaifu ya demokrasia za kikanda kutoka   eneo moja kwenda linguine, kufanya hivo ni udhaifu wa hoja.

Aidha kinachoendelea hivi sasa ndani ya siasa zetu za ndani ni demokrasia ya maamuzi na utashi kwa Watanzania kuamua kufanya walitakalo pasipo kuvunja sheria na taratibu za nchi, hoja za wanazuoni kuwa Tanzania hatuna demokrasia ni hoja mfu kabisa ambazo zinajengwa kwa makusudi ya upotoshaji wa umma.

Uwepo wa wimbi la uhamiaji wa wanasiasa kutoka chama kimoja kwenda kingine unaweza ukatafsiriwa kama kipimo cha kulinganisha itikadi imara  za chama na chama cha siasa,  katika kusimamia masuala muhimu ya kimaendeleo kwa  taifa  kulingana na ilani  zilizotambulishwa na vyama husika kwa wanachi.

Ieleweke vyema kuwa wanasiasa kuhama vyama vyao hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla si jambo geni  bali ni  kama desturi na tamaduni za kisiasa katika kuendesha ushindani wa itikadi ndani ya ulingo wa siasa.

Wanahojenga hoja kuwa sasa Tanzania inakosa mwelekeo kisiasa wanakosea aidha hawajui vyema siasa au ni wagumu katika kufatilia siasa za ndani na nje ya taifa letu.

Siasa ni ushindani wa hoja na itikadi madhubuti yenye misingi imara ya maendeleo, mchanganyiko huu uzalisha kitu kinachoitwa ilani ya chama ambayo usimama kama nguzo imara ya kwenda kubadilisha maisha na maendeleo ya Watanzania.

Uimara wa itikadi, falsafa na ilani ndio ushawishi unaoweza kuvutia watu kwenda upande wa pili kisiasa na wala si dhana ya uchawi bali ni uhalisia wa mipango na mikakati ya chama husika.

Hoja inayoweza kujengwa hapa na ikaonekana kuwa na mashiko ni je wahamihaji hawa  ni mtaji kisiasa, au nuksi na mizigo kwa chama, hoja hii lazima ijibiwe kimantiki na kuzingatia hulka na historia  za wanasiasa wetu wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla.

Kabla ya kujenga hoja juu ya dhana hii kwanza tuangaze maana ya neno nuksi,  kuitwa “nuksi” kunaweza kuibua sintofahamu kutokana na maana ya tafsri iliyo ndani yake, mitaani vijana mabibi kwa mabwana utwangana makonde kisa kubatizwa neno nuksi.

Bila shaka katika ulingo huu wa siasa hakutakuwepo na ngumi wala makonde ya aina yoyote, maana hapa hoja ujibiwa kwa hoja na tunajaribu kulinda misingi ya utaifa wetu kupitia kukosoana na kuelimishana.

Nuksi si neno geni miongoni mwa jamii ya Watanzania ni neno ambalo limekuwa likitumiwa mara nyingi katika shughuli zetu za kila siku, Maana ya nuksi ni hali ya kutokuwa na bahati ya maisha au kutofanikiwa kabisa katika kila jambo unalolipanga kulifanya.

Kwa mila zetu za kiafrika mfano Wahaya  Mwenye nuksi  wa umuita ( aina omukosi), mtu huyu ni balaa  na anaweza akawa chanzo cha matatizo katika ngazi ya familia na ukoo kwa ujumla, Mtu wa namna hii uogopwa na kukimbiwa kabisa kwa maana ni balaa na janga kwenye jamii.

Kwa sasa neno hili limeshika hatamu kwenye mijadala ya kisiasa hapa Tanzania kutokana na wimbi la hamahama linaloendelea hapa nchini, CCM imeendelea kupokea wanachama wapya wanaohama vyama vyao vya awali kwa mantiki ya kuunga mkono jitihada za serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na uchapakazi wake katika sekta ya maendeleo.

Wahamiaji wa kisiasa wanayo hoja kuu yenye mashiko, ni kweli JPM amefanya mapinduzi ya kimkakati katika kuhakikisha maendeleo ya vitu kwa maslahi ya watu yanafanikiwa na sasa matokeo yanaonekana na ili halina mjadala wa ubishi wowote.

Hoja iliyopo mezani hapa ni je Wahamiaji hawa ni nuksi kwa chama au watu wenye tija kwa misingi ya maendeleo ngazi ya chama na taifa kwa ujumla. Tujenge hoja katika nadharia mbili nyeti  kudadisi dhana ya unuksi na utija wao ndani ya chama na taifa.

Mosi, kundi hili limegawanyika katika sehemu kuu mbili,  moja  wapo wanasiasa  wahamiaji wenye nia njema na Chama Cha Mapinduzi CCM, Kundi hili linayodhamira ya kweli katika kuhakikisha jitihada za maendeleo kupitia chama na serikali zinafanikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa, kundi hili lipo tayari kushinda njaa na kukosa chochote ili mradi tu maendeleo  kwa umma yapatikane.

Tabaka hili la wahamiaji ni matokeo ya kundi la wanyonge waliokuwa ndani ya vyama vya upinzani waliobanwa kifikra pale walipoonyesha nia ya kuunga mkono maendeleo ya kitaifa, Kundi hili linaundwa na misingi yenye dhana ya kutopinga kila kitu kwa kisingizio cha upinzani bali uzalendo kwanza.

Kundi la pili linaundwa na watu ambao unaweza kuwafananisha na samaki aina ya nguva, nusu mtu nusu samaki, kundi hili si jema kwa ustawi wa chama kwa maana ni kundi linalokuja kwa maslahi binafsi ikiwemo kutafuta vyeo na nafasi za uteuzi.

Kundi hili linaweza kuwa chanzo cha nuksi ndani ya chama na hivyo kuibua sintofahamu ya hapa na pale, ni kundi ambalo linapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu katika kuhakikisha misingi ya chama inaimarishwa na kulindwa. Aidha ni kundi lenye vimelea vya “Kujipendekeza” ieleweke kuwa tabaka lenye watu wa kujipendekeza kwenye jamii ni baya na uzalisha misigano na migogoro isiyokuwa na mwisho.

Tukijenga hii hoja tuinyumbue katika dhana ya  mtazamo wa muda mrefu, Kwa jinsi gani  nadharia ya wahamiaji hawa ni sehemu ya nuksi na mzigo ndani ya chama; na fafanua.

Wahamiaji hawa wa kisiasa wanaweza kuwa chanzo cha migogoro endapo tu watakosa walichokikusudia ndani ya chama, si wote wenye nia njema  na falsafa,  itikadi na misimamo  ya chama walipo hamia bali wasaka tonge na wenye tamaa za madaraka  na kutanguliza maslahi yao kwanza bila kutanguliza maslahi ya umma. Kundi la namna hii ni nuksi na mzigo kwa chama.

Tunaweza kupata ukweli wa hoja hii kutokana na historia zao  kisiasa kwa kujiuliza maswali kadha wa kadha, Mfano; Je watu hawa wana misimamo ya hoja au ni makasuku wa hoja?

Je ni wazalendo kwa taifa lao? Au kweli wameguswa na jitihada za Rais Dkt. Magufuli katika kuwaletea maendeleo Watanzania au ni wanafiki tu na mamluki wa kisiasa.

Hizi si hoja za kubeza bali ni mambo ya msingi katika kuhakikisha chama kinakuwa salama na kustawi kwa maendeleo ya umma, ni wajibu wetu sasa kifikiri kwa makini tunaweza kupata majibu juu ya kundi hili ambalo kwa lugha nyepesi limevaa ngozi ya kondoo kumbe ndani ni fisi.

Hata hivyo siasa zetu zimekuwa na wanasiasa wenye hulka za kufata upepo kama bendera na wasio na hoja mbadala katika kulinda maslahi ya chama na itikadi zake, ndo maana napata ukakasi kuamini baadhi ya wanasiasa wanao hama vyama vyao kwa kisingizio cha kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli.

Si kosa kuunga mkono jitihada za Rais, bali wengine wanatumia hoja hii kama sehemu ya kwenda kuvuruga na kuharibu mifumo ya kimaendeleo, ni jukumu la Dkt. Bashiru ambaye ni Katibu Mkuu wa chama cha CCM,   msomi na mwana ujamaa ambaye anaishi kwa kuamini kile anachokiamini kuwa makini na ujio wa wahamiaji hawa katika kuhakikisha chama kipo mikononi salama.

Kwa mantiki ya wazi wote wanaojitambulisha kama wahamiaji wa kisiasa wapokelewe kwa maana ni mtaji kisiasa lakini ni vyema intelejensia ya chama ijikite kuwamulika na kuwabaini wale wote wenye nia ovu ikiwa ni pamoja kuja na agenda ya uchonganishi na usaliti wa hapo badae ndani ya chama.

dmutungid@yahoo.com , 0717-718619