Home Michezo Kimataifa Wanaotamba Ulaya waliotoswa Afcon 2019

Wanaotamba Ulaya waliotoswa Afcon 2019

2387
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

FAINALI za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019), zimebakiza siku chache kabla ya kuanza kutimua vumbi katika ardhi ya Misri, yanai Juni 21 na kufikia ukomo wake Julai 19.

Kwa sasa, timu zote 24 zitakazotia mguu katika michuano hiyo ya CAF (Shirikisho la Soka Afrika), zinajifua kwa mechi za kirafiki, nyingine zikikimbilia kuweka kambi barani Ulaya.

Kubwa zaidi kipindi hiki ni vikosi vilivyoanikwa na makocha, ambapo imeshuhudiwa baadhi ya nyota wakiitwa kwa mara ya kwanza, huku wakiwapo wachezaji wenye majina makubwa walioachwa.

Katika hilo la wanasoka wenye majina makubwa walioshindwa kupata nafasi ya kuwa sehemu ya vikosi vya timu zao za taifa, wapo hata wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Kelechi Iheanacho (Nigeria/Leicester)

Mshambuliaji huyo aliitwa katika kikosi cha awali cha Nigeria kilichokuwa na wachezaji 25, lakini ameshindwa kubaki ‘top 23’. Iheanacho hajaifungia bao Nigeria tangu alipofanya hivyo mwaka juzi katika mchezo dhidi ya Argentina.

Mbali ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, mwingine ambaye hataongozana na Super Eagles kwenda Misri ni Semi Ajayi anayeichezea Rotherham United ya England.

Kocha wa Nigeria raia wa Ujerumani, Gernot Rohr, ameamua kwenda Afcon 2019 akiwa na kikosi chenye wachezaji wengi waliocheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka jana.

Eagles, mabingwa mara tatu wa michuano hiyo ya Afrika, wamepangwa Kundi B, hivyo watavaana na Guinea, Madagascar na Burundi watakaofungua nao dimba Juni 22.

Gervinho (Ivory Coast/Parma)

Nyota huyo wa zamani wa Arsenal, alikuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita akiwa na kikosi cha Parma, ambapo alifunga mabao 11 na kutoa ‘asisti’ nne.

Hata hivyo, hiyo haikutosha kumpa nafasi katika kikosi cha Ivory Coast kitakachokuwa Misri chini ya kocha Ibrahim Kamara. Isitoshe, mkufunzi huyo aliamua kumchukua straika Wilfried Bony, ambaye amekuwa hana klabu kwa muda sasa.

Pigo ni kwamba Ivory Coast itakwenda Misri ikiwa bila huduma ya beki wake wa kati, Eric Bailly, anayesumbuliwa na majeraha. Nyota wengine wa Ulaya watakaokuwa na kikosi hicho kule Misri ni Wilfried Zaha (Crystal Palace), Nicolas Pepe (Lille) na Serge Aurier (Tottenham).

Faouzi Ghoulam (Algeria/Napoli)

Si jina geni katika soko la usajili barani Ulaya, ikitosha kusema mwaka jana Manchester United waliweka mezani Pauni milioni 40, lakini Napoli walilikataa dau hilo.

Lakini, kuachwa kwake katika kikosi cha mwisho kitakachokwenda Misri kulitokana na ukweli kwamba nyota huyo ameshindwa kurejesha ubora wake tangu alipokaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha.

Hata hivyo, licha ya utitiri wa vipaji uliopo, kikosi cha Algeria kilichowekwa Kundi C, sambamba na Kenya, Senegal na Tanzania, kinatarajiwa kubebwa na staa wa Manchester City, Riyard Mahrez.

Mame Biram Diouf (Stoke City/Senegal)

Kocha wa Senegal, ambaye pia ni beki wa zamani wa Liverpool, Aliou Cisse, ‘amemfungia vioo’ mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United anayeichezea Stoke kwa sasa.

Huku akibeba mastaa wengi wanaocheza Ulaya, wakiongozwa na Sadio Mane wa Liverpool, Cisse hakuiona nafasi ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 31.

Ikumbukwe kuwa ukiacha Diouf, mkuu huyo wa benchi la ufundi aliwakata nyota wengine watatu wanaocheza Ufaransa; Diafra Sakho (Stade Rennais), Cheikh Ndoye (Angers) na Adama Mbegue (Caen).

Admiral Muskwe (Leicester City/Zimbabwe)

Baada ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya Nigeria iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, kocha Sunday Marimo Chidzambwa, alitangaza ‘jeshi’ atakalokwenda nalo Misri.

Muskwe, mshambuliaji wa Leicester City ya Ligi Kuu England, alikatwa, huku nyota wawili maarufu Ligi Kuu Tanzania Bara, Thabani Kamusoko na Tafadzwa Kutinyu, wakiingia katika orodha ya majina 23.

Zimbabwe wameangukia Kundi A, hivyo ili kuvuka makundi na kutinga hatua inayofuata, kwa maana ya 16 bora, basi watakwaruzana na Misri, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).