Home kitaifa Wanaotishia kupoteza uhai wa watu kwa ushirikina wachukuliwe hatua

Wanaotishia kupoteza uhai wa watu kwa ushirikina wachukuliwe hatua

883
0
SHARE

DK. HELLEN KIJO BISIMBA

NIMEFUATILIA taarifa zilizosambaa wiki iliyopita ikionyesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dk. John Magufuli anatabiriwa kuendelea kuwa Rais mwaka 2020.

Kwanza nilijiuliza iwapo huu ni utabiri au ni  jambo linaloonekana dhahiri kutokana na viashiria vingi vya hali ya siasa nchini. Tumesikia kuwa kwa mujibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais aliye madarakani  hupewa fursa ya kuendelea kuwa mgombea hadi amalize vipindi viwili.

Pia kuna chama cha upinzani ambacho kimempendekeza kuwa mgombea wake, kwa hiyo hata chama chake wasipompitisha tayari ameshapitishwa na chama kingine yaani TLP (Tanzania Labour Party). Nimekumbuka pia Rais wetu huyu ilisemekana kuwa ni chaguo la Mungu na hili lilisemwa na Rais aliyemwachia madaraka (Jakaya Kikwete) na hata   viongozi mbalimbali wa dini zetu hapa nchini.

Sasa hivi mijadala ni mingi kuhusu urais  katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020. Wapo wanaosema Rais                                            Magufuli ndio chaguo la Mungu na ndiye atakayeendelea kuwa Rais. Wakati huo huo wapo watu wanaoonyesha kuwa nao wangeupenda huo urais na wala si wa vyama vya upinzani bali ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kauli hizi zimeleta mijadala kwani wapo waliosema wazi kuwa haiwezekani mtu mwingine ajaribu kutaka kuwa Rais kwa vile ni mila ya chama hicho tawala, kuwa Rais aliye madarakani ndiye hutetea kiti chake hadi amalize muda wake yaani mihula miwili.

Wengine wamehoji iwapo huu utamaduni unalindwa na sheria au umeshakubalika kuwa sheria kutokana tu na jinsi ambavyo imekuwa hivyo tangu mwaka 1995.

Jambo lililonifanya nijiulize maswali ni pale nilipoona kwenye vyombo vya habari kuhusu taarifa kutoka Simiyu kuwa wamekusanyika waganga wa jadi 900 kutoka Gombushi Bariadi na katika kusanyiko lao hilo, wametoa onyo kwa mwana CCM yeyote atakayethubutu kuchukua fomu ya urais mwaka 2020, eti watampoteza.

Nilisoma hii taarifa mara mbilimbili kuwa ni kweli au ni mchezo wa kuigiza. Hatimaye nilijiridhisha kuwa ni taarifa iliyoandikwa kwa kile kilichotokea na hata picha nikaziona.

Yaani hawa waganga wa jadi wameibukia kwenye siasa za hiki chama tawala au nao pia ni wana chama wa chama hiki tawala na wameona kuwa upo uwezekano wa mwana  CCM kuchukua fomu dhidi ya Rais ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa chama hicho. 

Nilivyoangalia hili tishio nikaona kuwa hawa waganga wanawatisha wale wana CCM waliozungumzia suala la kuutaka huo urais mwaka 2020.

Ipo mijadala imeendelea baada ya tishio hili. Kuna watu wamehoji iweje Rais huyu  mcha Mungu anayeombewa kila wakati makanisani apewe ulinzi na hawa waganga wa jadi? Katika majadiliano hayo wapo waliosema kuwa huyu ni Rais wa wote hata hao waganga wa jadi ni raia wake hivyo wana haki ya kumlinda Rais wao dhidi ya watu wanaotaka kunyemelea kiti chake.

Kuna mwingine nimeona ameandika kuwa hawa waganga wamedandia treni kwa mbele kwani tayari utabiri ulishatolewa na viongozi wa dini kuwa Rais huyu ni chaguo la Mungu na ndiye atakayekuwa Rais  mwaka 2020.

Hii mijadala hainipi shida sana, tafakari yangu ni hilo tishio lililotolewa na pia ni  huo ulinzi anaotaka kupewa Rais kwa watu kutishiwa kuwa watatoweshwa. Tishio la aina hii naliona ni kinyume cha sheria. 

Je, si kuingilia haki walizo nazo wana CCM kama raia huru wa Tanzania?  Ninavyofahamu kila mwanachama wa CCM mwenye sifa zinazokubalika kikatiba na kisheria ana haki ya kuchukua fomu kama anataka kugombea nafasi ya urais.

Kwenye demokrasia hii ndio haki. Iwapo watu wa chama hicho wanampenda sana huyu Rais ambaye naye ana haki ya kutetea nafasi yake, nadhani wakati wa mchakato ndani ya chama ndipo wampinge mwingine yeyote kwa kutompa kura wakati wa kura za maoni.

Nilitegemea viongozi wa chama hasa katibu mkuu wa chama hicho awasaidie hao waganga kwa kuwaelewesha utaratibu. Iwapo huo si utaratibu waeleweshwe pia kuwa utaratibu wao hauruhusu mtu kuchukua fomu kwa vile aliyeko madarakani ndiye anayepita bila kupingwa hadi kipindi chake cha pili.

Hata hivyo nimeona ushabiki mkubwa hata wa viongozi wa kisiasa kwenye hili suala, nakakumbuka utafiti uliotolewa miaka ya hivi karibuni ukisema Waafrika ni washirikina pamoja na kuwa wanaonekana ni wacha Mungu.

Tanzania tulionekana ni vinara katika utafiti huo tukiwa na asilimia za juu za watu wa nchi yetu kuamini kwenye ushirikina. Niliposoma utafiti ule sikuuamini nikasema hawakuchukua sampuli zao vizuri. Hili suala la hawa waganga 900 katika eneo moja wanazungumzia kuroga na kumpoteza mtu limenionyesha huenda huo utafiti ukawa wa kweli.

Ndio maana naona kwa tishio kama hili linaweza kweli kuwafanya watu waogope kuchukua fomu wasije wakapotezwa. Na hapo ndipo nilipoona pia ni Tanzania ambapo mtu aliye chaguo la Mungu na sio miungu anaweza kupewa ulinzi na waganga wa jadi kwa tishio la kuroga mtu na watu wakaona imekaa sawa.

Kwa watu wanaomwamini Mungu uganga wa aina hii ni kinyume cha imani yao pamoja na kuwa wachawi wanasemekana wapo kama walivyoonekana katika kitabu cha biblia cha Kutoka mlango wa 7. wachawi wa Farao wa Misri.

Pamoja na kuwa ipo haki ya watu kutembea na imani zao, hawa wanaotishia kupoteza watu ikiwa ni kumpatia Rais kinga dhidi ya ushindani uliopo kisiasa naona si sahihi na ilibidi ama waeleweshe kama si kuchukuliwa hatua.

Na kwa wale waliotoa utabiri wa chaguo hili la Mungu nao walipaswa kuwa na la kusema katika hili. Pia wale wanaoongozwa na sheria wala si dini au imani za kishirikina  nao walipaswa kutoa mwongozo katika hili.

Iwapo kweli kipo chama kinachowakosesha wanachama wenye nia ya kugombea kwa sababu zisizo za kisheria nao wanapaswa wasaidiwe kufuata sheria na kusimamia haki walizo nazo wanachama.

Na iwapo ni kanuni za chama lakini wanachama wa chama hicho hawaziafiki ni wajibu wao kuweza kuzirekebisha ili ziendane na matakwa ya sheria na haki walizo nazo kama wanachama na kama raia. Tanzania ni nchi ya kidemokrasia hili lisiwe ni kwa maneno yaliyoandikwa kwenye Katiba liwe ni kweli watu wawe na haki ya kuishiriki demokrasia kwani demokrasia ni watu na si mifumo tu.