Home Habari Wanasoka wetu wazingatie miiko ya soka wafike mbali

Wanasoka wetu wazingatie miiko ya soka wafike mbali

860
0
SHARE

Na MAWAZO LUSONZO

UKWELI ni kama ibada. Ukiamua kusema ukweli, basi usiogope kulaumiwa, kutukanwa na hata kupata dhihaka kutoka upande wa pili.

Lakini pia, ukweli una tabia ya kuishi maisha marefu kuliko uongo. Unapokuwa mkweli, una uhakikakwamba kile ulichosema kitaishi zaidi, kuliko uongo ambao utausema ambao hakika hauwezi kudumu.

Ukiamua kuyachambua maisha ya wanasoka wa Tanzania, lazima umtangulize Mungu akuwezeshe kukupa pumzi ya kuwa mkweli.

Ukitaka kuandika chochote kinayohusu maisha ya vijana wetu maana yake ni kwamba, lazima uingie mpaka kwenye fukwe za vyumba vyao. Uwaambie ukweli, usiogope kulalamikiwa au kulaumiwa maana lawama ni sehemu ya maisha.

Lakini kama nilivyosema hapo juu, kwamba ukweli unauma. Lakini ukitaka kuwa huru, kuwa mkweli.

Wachezaji wa Tanzania, walio wengi kabisa maisha yao yamegubikwa na utata mkubwa.

Uchunguzi wa Mwandishi wa makala haya, umebaini kwamba viwango vya mpira wa wanasoka wengi hapa nchini vimekuwa vikishuka na kumalizika kabisa kutokana na kutozingatia miiko ya uchezaji.

Uchunguzi huo umebaini kwamba,  wachezaji wetu wengi wamekuwa wakibweteka na mafanikio ya muda mfupi wanayoyapata.

Baadhi ya wachezaji kwa mfano, wamekuwa wakiapa kwamba kwa kusajiliwa na Simba au Yanga tutawanaona wamefikia kiwango cha juu kabisa cha mafanikio ya soka hapa nchini.

Wachezaji wetu wakishapata magari, kwao hayo ndio mafanikio makubwa. Hawana malengo tena ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, hawana tena malengo mengine ya kimaisha, lakini pia wanasahau kwamba maisha ya soka yana muda mfupi sana.

Wakati mwingine, ni jambo jema kujifunza kwa mafanikio anayoyapata mtu mwingine. Wachezaji wetu hapa nchini, wangetakiwa kujifunza kwa Mbwana Samatta , Thomas Ulimwengu na Simon  Msuva.

Awali,Samatta, Ulimwengu walisajiliwa na timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),kwasababu walijifunza, wakajitunza pia hadi kuwashawishi miamba hao wa soka katika Afrika kuwapa nafasi katika timu hiyo kubwa.

Leo hii Samatta anang’ara katika klabu ya KRC Genk ya nchini Ubeligiji, Ulimwengu anakimbiza J.S Saoura ya Algeria.

Msuva yeye akifanya mambo makumbwa katika klabu ya Difaa Hassan El Jadida ya nchini Morocco.

Lakini wakati Samatta anazidi kujiimarisha kimaisha, wachezaji wengine wengi wa Tanzania wanapoteza muda kwenye mabaa na makasino huku wakilewa na kubadili wanawake kama nguo.

Ukiyatazama mafanikio ya Samatta unaona kwamba,  mchezaji huyu amejitenga na tabia za wachezaji wengi wa ‘kibongo’.

Samatta ana nidhamu ya hali ya juu, anajali mazoezi na anayapenda maisha yake.

Wakati unamshangaa Samatta kwa nidhamu aliyojiwekea, baadhi ya wachezaji wetu wengine wanashindana kuporana wanawake, wanashindana kulewa na kuyafanya mengine yasiyostahili.

Halafu unashangaa kwanini timu ya taifa haina mafanikio yoyote. Unashangaa nini wakati wachezaji wenyewe wanamaliza nguvu na stamina kwenye miili ya watu wengine?

Bado unashangaa kwanini mchezaji wetu wa timu ya taifa akipigwa chenga moja tu anaanguka na inamchukua muda kuamka!

Haya ndiyo maisha ya wanasoka wetu. Lakini kama nilivyosema huwezi kuwaacha wachezaji wetu waendelee na maisha haya ya anasa bila kuwasema, bila kuwaaambia ukweli.

Huwezi kukubali kuwaona wachezaji wetu wanalewa mpaka usiku wa manane, wanagombea wanawake mpaka kunakucha bado ukafumba macho na kuangalia sinema hizo.

Maisha ya wachezaji hawa kimpira hayawezi kuendelea ikiwa sisi ambao tunatakiwa kuwalea katika maadili, tunakuwa sehemu ya kuwaharibu kimaadili.

Maisha ya mpira ni mafupi, lakini kwa bahati mbaya wachezaji wetu wengi hawajitambui na hawataki kukubali kwamba maisha yao katika soka hayazidi miaka kumi.

Wako ambao wametazama mbali. Licha ya kuwa na vipaji vya kucheza mpira, pia wamejiendeleza sana kielimu. Kwamba mpira utakapomalizika watafanya mambo mengine ikiwa ni pamoja kusaka ajira.

Lakini pia kuna kundi lingine la wachezaji ambao wameanza kufungua miradi mbalimbali, wakijua kwamba baada ya maisha ya mpira kumalizika wanatakiwa waendelee kuishi na familia zao.

 Hawa ni pamoja na wale waliofungua biashara mbalimbali. Hapa nina mifano iliyo hai. Kama mlinda mlango Mohammed Mwameja asingewekeza fedha alizokuwa anapata akiwa Simba katika biashara, baada ya kumalizika mpira angekuwa ombaomba leo.

Lakini Mwameja alifahamu mapema kwamba maisha ya mpira ni mafupi, ndiyo maana leo hii anafanya biashara zake kwa amani na anamudu kuishi na familia yake kwa amani.

Kama Zamoyoni Mogella na Dua Saidi wasingetazama mbali kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kibiashara, leo wangeishi vipi baada ya mpira kumalizika?

Kama Ali Mayai asingejiendeleza kielimu, tena wakati anacheza soka, ni nani angemwajiri baada ya kumaliza soka lake?

Hawa ni wachezaji wenye akili. Wako wengine ambao wamefanya mambo ya maana sana baada ya kuacha soka, wanaishi vema na familia zao na maisha yanasonga mbele.

Lakini pia wako wengine walioishi maisha ya sifa, maisha ya ulevi na uzinzi, leo wamebaki ombaomba wakilalamika kwamba mpira haulipi.

Wengi wao ni wale waliokuwa na majina makubwa katika mpira wa miguu hapa nchini. Ni wale ambao tuliingia uwanjani na kuwashangilia sana kila walipogusa mpira. Tunawatazame leo, tutawahurumia!

Wachezaji wetu wa sasa wangejifunza kwa anguko la baadhi ya wachezaji hao wa zamani. Wangejifunza pia kwa mafanikio ya wachache ambao walitumia akili na kutazama mbele.

Wale ambao leo tunasema kwamba tunawapenda wachezaji hawa vijana, basi mapenzi yetu yawe ya kweli ya kuwashauri mambo ya maana.

Kama kweli tunawapenda tusiwanunulie pombe na kuwakuwadia wanawake. Kama kweli tunataka soka la Tanzania likue, tukiwakuta wachezaji hawa wanafanya mambo ya maana, tuwasute na ikibidi kuwashitaki kwa viongozi wakatwe mishahara kwa kukosa maadili!