Home kitaifa Wanawake viongozi wapewe nafasi ya kusikilizwa

Wanawake viongozi wapewe nafasi ya kusikilizwa

874
0
SHARE

ANNA HENGA

UONGOZI ni uwezo wa mtu kushawishi kundi fulani la watu, kuwaongoza na kuweza kutimiza lengo lililokusudiwa.

Kiongozi ni mtu anayeshawishi na kujenga watu kuweza kufanikisha malengo yaliyowekwa. Viongozi wanaweza kuwa wanawake au wanaume.

Tunaposema wanawake na uongozi ni kuhakikisha ni wale wenye sifa wanapata nafasi ya uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwemo kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.

Nia ni kuhakikisha wanawake na wanaume wanakuwa na haki sawa katika nafasi za uongozi bila kuwabagua wanawake na pia kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya maamuzi na wanashiriki katika maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Uongozi huu unaweza kuwa katika nafasi za kisiasa, biashara, elimu, viwanda, sayansi na teknolojia na kadhalika.

Ni muhimu kuweka usawa wa kiuongozi kati ya wanawake na wanaume na kuhakikisha kuwa wanapata nafasi sawa za uongozi kama wanaume na kuvunja vikwazo vyote vinavyozuia wanawake kupata nafasi hizo.

Usawa wa kijinsia katika uongozi ni muhimu kwa sababu maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwa na utofauti katika uongozi unaoongeza ufanisi.

Wanawake nchini Tanzania wameendelea kuonekana katika nyanja mbalimbali za uongozi ingawa kwa kiasi kidogo sana. Jamii ya Tanzania bado haijaachana na tamaduni zinazomnyima mwanamke nafasi ya uongozi hata kama ana sifa za kuongoza.

Hata hivyo, Tanzania imeshuhudia mapinduzi makubwa katika uongozi wa wanawake kama Samia Suluhu Hassan ambaye ni Makamu wa Rais wa kwanza tangu tupate uhuru na pia wanawake wengi waliothubutu kuwania nafasi za ubunge kwa kugombea na kunyakua nafasi hizo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibara ya 12 inatoa usawa kwa watu wote bila ubaguzi, ibara za 39, 47 na 67 zinaeleza kuwa mtu yeyote anaweza kuchaguliwa kuwa Rais, Mbunge au Makamu wa Rais bila ubaguzi wowote.

Ibara ya 22 inaelezea kuwa mtu yeyote ana haki ya kufanya kazi, ibara ya 21 pia inatoa haki ya kila mtu kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi iwe moja kwa moja au kwa uwakilishi, ibara ya 78 pia inatoa utaratibu wa kuchagua wanawake wabunge wa viti maalumu. Hii inaamanisha watu wote wanaume kwa wanawake wana haki ya kuchaguliwa kuwa viongozi.

Hapa nchini wanawake bado wako nyuma katika masuala ya uongozi, hii ni kwa sababu nafasi nyingi za uongozi zinashikiliwa na wanaume, wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania lakini uwakilishi wa wanawake bungeni ni asilimia 33 kwa jumla ya wabunge 145, asilimia 9 ni wabunge wa kuchaguliwa majimboni ambao idadi yao ni 25 na 120 ni wabunge wa viti maalum.

Kuna mawaziri wanne tu na manaibu waziri sita, makatibu wakuu watatu na manaibu makatibu wanne. Pia katika nafasi za uongozi katika serikali za mitaa na mikoani wanawake bado wapo nyuma ambapo kwenye wakuu wa mikoa kuna wanawake wanne tu katika mikoa 26.

Hii inaonesha kuwa wanawake katika uongozi bado wako nyuma sana na hakuna asilimia 50 kwa 50 japo kuna wanawake wengi wenye sifa za kuongoza.

Wanawake wanakumbwa na changamoto mbalimbali katika uongozi ikiwemo kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake kuanzia ngazi ya familia hadi ngazi za juu, mila na desturi potofu dhidi ya wanawake kuongoza, ukatili wa kijinsia,, kudharauliwa na kubaguliwa pamoja na kutokujiamini kunakosababishwa na kukandamizwa kwa mwanamke kwa muda mrefu.

Katika kuhakikisha wanawake wanashikilia nafasi za uongozi, kwanza ni kuwaelimisha wanawake na kuwajengea uwezo kujiamini na kuvunja vikwazo vinavyowazuia kuwania nafasi za uongozi, kuelimisha jamii kuachana na mila potofu na kuamini wanawake pia wanaweza kuwa viongozi wazuri.

Vilevile kuhakikisha wanawake wanapata elimu na miundombinu, mifumo inawasaidia wanawake kupata elimu bora, kuwa na wanawake wa kusaidia kufanya maamuzi katika vyama vya siasa na uchaguzi wa kuteua wawakilishi wa vyama kuwa wa haki na unaozingatia usawa wa kijinsia na pia kujenga vyama na taasisi za wanawake zitakazokuwa zikitoa msaada kwa wanawake wanaowania nafasi za uongozi bila kujali itikadi.

Hapa nchini Tanzania, wanawake wamekuwa wakikandamizwa na haki zao kuvunjwa kila siku, kumekuwa hakuna usawa wa kijinsia wa kuzingatia haki za jinsi zote mbili.

Wanawake wamekuwa wasikilizaji na wanaofuata wanaume wakifanya maamuzi hata yale yanayowahusu. Inapotokea wanawake wanasimama na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hukatishwa tamaa kuanzia ngazi ya familia, jamii na kadhalika, hii inawafanya wanawake kutokujiamini na kuona kuwa hawawezi kuwa viongozi.

Wanawake ni viongozi wazuri sana na wanatakiwa kupewa nafasi, tunaona mifano ya wanawake mahiri nchini Tanzania ambao wamesimamia vyema nafasi zao za uongozi walizoaminiwa.

Mfano Samia Suluhu Hassan, aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika, Getrude Mongela, aliyewahi kuwa Spika wa kwanza mwanamke, Anne Makinda ambaye alifanya vizuri katika muda wake wa uongozi.

Wengine Bibititi Mohamed mwanamke ambaye alikuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa nchi ya Tanzania na kusaidia kupatikana kwa uhuru, aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Asha Rose Migiro.

Vilevile kuna mawaziri kama Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ), Joyce Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia) ambao wanasimama vema nafasi zao.

Lakini pia kuna wanawake katika nyanja nyingine za uongozi wakiwemo wakurugenzi wa mashirika mbalimbali na wa makampuni makubwa ambao wanafanya vizuri sana katika nafasi zao.

Jamii zinatakiwa kuachana na mila potofu zinazotafsiri wanawake kama dhaifu na hawafai kuwa viongozi na kuwapa nafasi wanawake kuanzia ngazi za jamii hadi za kitaifa.

Ni wakati sasa wa kuhakikisha ile asilimia 50 kwa 50 inafikiwa kwa kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali kuanzia elimu.Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Anapatikana kwa namba; 0765 471 006.