Home Makala Kimataifa WAPIGAKURA VIJANA KUAMUA MATOKEO YA UCHAGUZI KENYA

WAPIGAKURA VIJANA KUAMUA MATOKEO YA UCHAGUZI KENYA

1142
0
SHARE

NAIROBI, KENYA

Zikiwa zimebaki siku 48 kabla ya uchaguzi mkuu nchini Kenya Rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta na mgombea wa muungano wa vyama vya upinzani Raila Odinga wanazidi kukabana koo – na kinyang’anyiro sasa ni kura za vijana.

Inakadiriwa asilimia 80 ya idadi ya watu nchini Kenya ni vijana wa kuanzia miaka 35 kwenda chini. Kufuatana na takwimu kuhusu idadi za watu, Kenya inajigamba kuwa na wapigakura vijana wengi zaidi miongoni mwa nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Zaidi ya nusu ya wapigakura 19 milioni waliojiandikisha wanadaiwa kuwa vijana, hivyo ushiriki wao katika uchaguzi wa Agosti 8 utakuwa muhimu na unaweza ukatoa picha halisi ya nani atakayeshinda urais.

Katika miaka ya nyuma baadhi ya wanasiasa wa Kenya wamewatumia vijana katika namna isiyo sahihi. Kuna baadhi walikuwa wananunua kura kutoka kwa vijana waliokuwa hawana ajira yoyote iliyokuwa inaeleweka, hivyo kujiongezea kura zao, wakati wengine walikuwa wakiwachochea vijana kufanya ghasia katika kupinga matokeo.

Na baada ya uchaguzi, vijana hutelekezwa katika hali ya kukata tamaa baada ya kupewa ahadi hewa kutoka kwa wanasiasa. Ajira wanazoahidiwa hazitengenezwi, kozi za kujiendeleza kielimu hazipatikani na gharama za maisha zinazidi kupanda.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, vijana nchini Kenya wanasikika wakisema kwa sauti moja “sasa yatosha.” Sasa wanataka kushiriki moja kwa moja katika maendeleo na utawala wa nchi yao.

Katika mahojiano na Chaneli ya DW wiki iliyopita, baadhi ya vijana wa vijiweni mjini Nairobi walisema uchaguzi wa safari hii utakuwa tofauti.

Wanasema: “Viongozi wa zamani wa siasa ambao wamekuwa madarakani wamekuwa wanatuchukulia sisi vijana kama ngazi zao tu za kupata madaraka, na wakisha kuwa huko juu sisi tunasahaulika kabisa.

“Sasa umefika wakati wa kuwaonyesha wazee hawa kwamba sisi ndiyo tunawaajiri wao. Sisi tutawapigia kura viongozi vijana kwa sababu tumegundua tunawakilishwa na watu wenye umri mkubwa (wazee) ambao hawazielewi changamoto zetu, hivyo tunahitaji watu wa rika letu kupigania masilahi yetu.”

Mpigakura mwingine kijana alieleza jinsi alivyochoshwa na hali ya kutumiwa na wanasiasa hata katika umwagaji damu ili mradi tu watimize malengo yao ya kisiasa.

Hivyo alitoa wito kwa vijana kuchagua viongozi kwa akili, wazihoji ilani na ajenda zao, wazisome vyema na wapigie kura viongozi wenye dhamira njema kwa nchi na siyo ambao wanafanya siasa nyepesi nyepesi tu katika kuhadaa wapigakura.

Utafiti wa karibuni wa Benki ya Dunia unaonyesha kijana mmoja kati ya vijana watano wa umri kati ya miaka 15 na 29 hana kazi. Hivyo vijana wa Kenya wameawania kutumia idadi yao kubwa kwenye sanduku la kura katika kuitengeneza sura mpya ya nchi baada ya uchaguzi wa mwaka huu.

Mchambuzi maarufu wa masuala ya siasa nchini Kenya Naftali Mwaura anasema hajawahi kuona hamasa kubwa miongoni mwa vijana kama katika uchaguzi huu.

Anaongeza: “Rika hili la wapigakura linaweza kubadili mwelekeo wa matokeo, linaweza kuamua matokeo.”

Anasema pamoja na ukweli kwamba wagombea wa umri mkubwa ndiyo wenye pesa na madaraka ya kisiasa, lakini lazima watambue kuna kundi kubwa la vijana ambalo limekuwa likipuuzwa, na ambalo linaona siasa za nchi haziendi katika mwelekeo mzuri na stahiki.

Hata hivyo wadadisi wengine wa mambo wanasema medani ya siasa ilivyo nchini Kenya si tiifu sana kwa idadi yoyote ya vijana kwani kwa ujumla siasa za Kenya zimejaa mgawanyiko wa kikabila na kikanda hali ambayo ni hasi kwa vijana.