Home Habari WASOMI WATAKA TUME KUCHUNGUZA KUZOROTA KWA ELIMU

WASOMI WATAKA TUME KUCHUNGUZA KUZOROTA KWA ELIMU

5240
0
SHARE
JOHANES RESPICHIUS   |

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwashangaa watu wanaosema elimu imeshuka na kuwataka kuacha kuongea kama hawana taarifa za kutosha, baadhi ya wasomi wameibuka na kueleza kuwa ipo haja ya kuundwa kwa Tume maalum ya kuchunguza kuzorota kwa elimu nchini. RAI linaripoti.

Akiwa katika hatua ya mwisho ya ziara yake kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Rais Magufuli alisema hafahamu watu wanaosema elimu imeshuka kama walishawahi kufika chuaoni hapo na kuona Panya anavyofundishwa kuyajua mabomu.

“Unajua hata watu wanaosema elimu imeshuka sifahamu kama wameshafika hapa, kwa sababu kama wangefika hapa wakamwona Panya anajua bomu liko wapi, wasingesema elimu imeshuka.”

Alisema kama Panya anafundishwa mpaka akaelewa, iweje binadamu asielewe na kwamba waalimu wa chuo hicho wanafundisha maka Panya na si binadamu pekee.

“Paka anaelewa akinusa hapa kuna kifua kikuu, anatengeneza mapapai mpaka anatengeneza ‘cross blinding’ kwamba papai lazima lianze kuzaa likiwa na miezi mitano, badala ya kulisubiri miaka mitatu, halafu linazaa matunda mawili matatu, wamefanya hawa watu, hapa kuna vichwa, tuache generalization.”

Aidha Rais alisema ipo haja ya kuelewa ilipotoka elimu yetu kwani kabla ya kufika hapa palikuwa na waalimu wa darasa la saba (UPE) walioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julisu Nyerere na hiyo ilifanyika kwa sababu hapakuwepo na watu wanaoenda kufundisha.

“Baadae ikaja suala la kupelea waalimu, mtu akipata division zero au four, wewe ndio unapelekwa kozi ya ualimu, tulifanya hivyo kwa sababu ya hali halisi ya wakati huo.”

Alisema katika awamu ya nne alifukuza wanafunzi karibu 7000 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambao hawakuwa na sifa stahiki.

“Tumekuja kwenye awamu ya nne iliyopita, mimi nilifukuza karibu wanafunzi 7000 pale UDOM, form four walipelekwa kwenda kuchukua digrii, walipelekwa kwenye awamu ya nne….unaweza kujua tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi.

“Na sisi tumekuja ndio tumeingiza elimu bure, wanafunzi wa shule ya msingi wameongezeka kutoka milioni moja mpaka milioni mbili, inawezekana hii nayo ikaleta madhara baadae, mtu mwingine angeweza akahoji kwamba tungewaacha tu ili wakawe mbumbu watawalike vizuri, kwa hiyo tukaongeza wanafunzi wa darasa la kwanza, tulikuwa tunapoteza wanafunzi milioni moja waliokuwa hawaingii darasa la kwanza kwa kukosa ada, wanafunzi wa sekondari wakaongezeka kwa asilimi 32, ‘No information you have no right to speak’ huna taarifa huna haki ya kusema.

Pamoja na mambo mengine, Rais pia alizungumzia ongezeko la mikopo kwa wanafunzi na changamoto mbalimbali ambazo serikali inakabiliana nazo katika elimu nchini.

Kufuatia kauli hizo za Rais baadhi ya wasomi wameeleza kuwa pamoja na maelezo hayo, lakini bado ipo haja ya kuundwa kwa Tume maalum itakayokuwa na jukumu la kushughulikia kuzorota kwa elimu.

Kuibuka kwa wasomi hao mwendelezo wa hoja na madai mbalimbali yaliyopata kutolewa katika siku za hivi karibuni na marais wastaafu ambao wameshauri kuitishwa kwa mjadala wa kitaifa wa kujadili Elimu.

Alianza Rais mstaafu wa awamu ya tatu nchini, Benjamin Mkapa ambaye alitoa wito wa kufanyika kwa majadilinao ya kitaifa kuhusu mwenendo wa sekta ya elimu nchini.

Mkapa ambaye ni mkuu wa chuo kikuu cha Dodoma (Udom), aliyasema hayo mwezi Machi mwaka huu wakati wa shughuli za kumuingiza kazini mkuu mpya wa chuo hicho.

Kwenye hotuba yake alimesema anashangazwa na matokeo mabaya ambayo yanashuhudiwa kila mwaka kutoka kwa shule za Serikali ukilinganisha na shule binafsi.

Mkapa amesema wakati umefika sasa wa mfumo wa elimu kutazamwa upya ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zinazoikabili sketa hiyo ili kubaini wapi kuna dosari katika kuboresha elimu inayotolewa kwa shule za Serikali.

“Naambiwa kuwa elimu yetu ndio iko chini zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sina hakika kwa kuwa sifahamu, hata hivyo ni muhimu kuwa na mjadala wa kitaifa ambao utakuwa shirikishi bila kujali kada ya raia.” alisema Mkapa.

Rais huyo mstaafu ameongeza kuwa huwa anajiuliza ni kwanini kila matokeo yanapotangazwa na baraza la mitihani, kati ya shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa haukosi shule 8 za binafsi na labda shule mbili zinaweza kuwa za Serikali.

“Hapa kuna tatizo lazima tuuangalie upya mfumo wetu wa elimu ili uendane na mahitaji ya sasa.” aliongeza Mkapa.

“Najua kuna watu watasema nalalamika sana, lakini hapana na mimi ni mwananchi wa kawaida,” alieleza.

Mara baada ya kauli ya Mkapa, mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akiwa mmoja wa wasemaji wakuu wanne kwenye kongamano lililopewa jina la Mageuzi ya Afrika katika Karne ya 21 lililoandaliwa na Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, alilizungjmzia tatizo la Eliumu kwa ngazi ya bara zima la Afrika na kutaka kuongezwa kwa juhudi za maboresho hasa kwenye Elimu ya Msingi na Sekondari.

Kauli hizo za marais wastaafu, ziliwaibua wabunge ambao walishinikiza kuwepo kwa mjadala wa kitaifa, ulioisukuma Seikali kukubaliana na hoja hiyo na kuahidi kulitekeleza hilo mapema.

HHata hivyo mwanzoni mwa wiki hii baadhi ya wasomi wameweka wazi kuwa hakuna sababu ya kulificha tatizo hili la kuzorota kwa elimu, badala yake linapaswa kutafutiwa ufumbuzi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete, alipozungumza na RAI juzi kwa njia ya simu ya mkononi, alisema Serikali inapaswa kuunda Tume maalum ambayo itachunguza mfumo mzima wa elimu nchini.

Alisema kuwa mfumo ambao unatumika wakati huu umepitwa na wakati kwani una takribani 36 baada ya kuboresha na Tume iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu, Jackson Makweta mwaka 1982.

“Nimekuwa nikisema kila mara kwamba ipo haja ya Tanzania kuunda tume ya kitaifa ya kuangalia mfumo wa elimu kwasababu ni miaka zaidi ya 36 sasa tangu kuundwa kwa tTume iliyokuwa na jukumu la kuangalia elimu.

“Tume hiyo ambayo mwenyekiti wake alikuwa Makweta iliundwa mwaka 1982 ndiyo ilikuwa pekee iliyochunguza mfumo mzima wa elimu wa Tanzania, sasa miaka yote hii kweli tunachikifanya tunakaa na kusema kwamba ‘nothing is wrong’ (hakuna tatizo) katika sera hii ya elimu.

“Sera hii haikutanguliwa na tume ya kuchunguza hali ilivyo ya elimu kwahiyo binafsi naona ni muda mrefu sana tangu sera ya elimu iundwe. Kwahiyo tunahitaji tume ya kuchunguza mfumo mzima wa elimu ili kuangalia unavyolingana na mifumo mingine duniani. Tume hiyo itasaidia kuangalia mustakabali wa taifa mbele ya safari… ukiangalia suala la elimu unaweza kusema ipo katika hali nzuri sio mbay, lakini ‘we are in trouble’9tuko kwenye matatizo),” alisema Profesa Mbwete.

Alisema Taifa halijakaa miaka ya kutosha na kutoa nafasi ya wananchi kuchangia jinsi mfumo wa elimu ulivyo sasa na namna unavyoweza kuboreshwa kwahiyo kujiridhisha kwamba kila kitu kiko sawa si kweli.

“Angalia Wakenya tangu wakati wameshaunda tume mara mbili au tatu kwahiyo ni kitu gani ‘special’ kwa Tanzania,” alisema Profesa Mbwete.

PROFESA MPANGALA

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema ubora wa elimu ya Tanzania umeshuka sio kama ilivyokuwa zamani wakati ikiongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na kiwango bora cha elimu.

Aidha alisema kuwa kwa viongozi wapo madarakani hawawezi kusema elimu imeshuka, ni lazima wajitetee.

“Kama alivyosema Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa, kipimo cha ubora wa elimu ni mitihani… sasa kama wanafunzi wana-feli sana wakati kinachofundishwa ni kilekile maana mtaala unaotumika ni mmoja lakini unakuta tofauti ya matokeo ambapo shule za Serikali zinakuwa na matokeo mabaya tofauti na za watu binafsi.

“Katika shule 100 bora, serikali inapata shule sita sasa hapo utasema elimu bado ni bora? Hiyo ni dalili kwamba ubora wa walimu umeshuka hasa waliopo serikalini.

“Sababu ya kushuka huku zinajulikana hakuna haja ya kuanza kuzunguka na mijadala ya kitaifa, kikubwa ni motisha kwa walimu kwa sababu hata shule zilizokuwa zinafanya vizuri sana nazo zimezorota kwani walimu wamekata tamaa, wanaangalia zaidi mambo yao,” alisema Profesa Mpangala.

PROFESA WANGWE

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kupunguza Umasikini (REPOA), Profesa Samweli Wangwe, alisema kinachochangia kuonekana elimu imeshuka ni kutokana na walimu kutotimiza majukumu yao ipasavyo.

Alisema zimekuwapo baadhi ya shule za serikali ambazo bodi za shule zimekuwa zikitimiza majuku yao zimekuwa zikifanya vizuri lakini nyingine ambazo uongozi ni mbaya zimekuwa zikifanya vibaya.

“Kuna walimu wakuu wakiamishiwa shule fulani zinafanya vizuri, akiamishiwa nyingine inaenda inafanya vuziri kutokana na kutimiza majukumu lakini shule nyingine za kiwango kile kile zinafanya vibaya wakati mazingira yote yanafanana,” alisema Profesa Wangwe.

Alisema kuwa jamii inapaswa kushirikiana na walimu kwa ukaribu kuhakikisha walimu wanatimiza majukumu yao na kila mwalimu afuate ratiba nzima iliyowekwa.

Bajeti ya Wizara ya Elimu ya mwaka wa fedha 2018/19 inayotarajiwa kujadiliwa hivi karibuni, inakadiriwa kufikia kiasi cha Sh. trilioni 1.4.