Home Makala WATANZANIA MSIMSINGIZIE MUNGU

WATANZANIA MSIMSINGIZIE MUNGU

810
0
SHARE

download

NINAANDIKA tena, nadhani leo itakuwa mara ya tatu, ya nne au zaidi. Ninaandika nikiwa najua fika kwamba mitandao hii husomwa na watu wa namna zote (sina hakika na wehu), ninajua wako wanaosoma ambao ni watumishi wa mamlaka mbalimbali za Serikali hapa nchini kwetu, namaanisha polisi (hasa wa usalama barabarani), watumishi wa wizara yenye jukumu la kusimamia elimu, mawaziri, wabunge na yamkini hata Rais Magufuli na wasaidizi wake mbalimbali.

Kuna majanga ya asili katika jamii yoyote, lakini kuna majanga mengi yanayotokea hapa kwetu ni ya kujitakia, mniwie radhi kwa kusema hivyo. Niliwahi kusema huko nyuma kwamba miongoni mwa majanga au matatizo ya nchi ambayo ni ya kujitakia, ni ugonjwa wa kipindupindu!

Lakini lipo jingine la ajali za barabarani (baadhi), ajali zinatokea kwingi duniani, lakini kwa hapa kwetu nyingi tumeziandaa bila kujua kwamba tumeziandaa au kuziandalia mazingira ya kutokea. Kwa mfano, angalia ubovu wa barabara zetu, angalia upana wa barabara zetu, angalia utaratibu wa kusafirisha abiria na mizigo na umbali wanaoutumia madereva wetu nk.. Aliwahi kuandika sana kaka Mimi Mwanakijiji kuhusu majanga ya kujitakia!

Lakini hapa siongelei hayo, naongelea usafirishaji wa watoto wetu wa shule! Kuna magari yanaitwa ‘school bus’ au ‘school van’, kwa Kiswahili tunayaita magari au mabasi ya shule. Kwa ujasiri kabisa nasema tuna usafirishaji holela na wa hovyo sana wa watoto wetu, hovyo kabisa ‘and it seems like no one cares’! Tumezoea matatizo, tumezoea misiba, tumezoea kumwangushia Mungu jumba bovu, kwamba yeye ndiye anayetwaa……ujinga huu umekomaa na kufika kiwango cha upumbavu na unafiki!

Watoto wetu bado wanapandishwa kwenye magari aina ya Toyota Noah wakiwa wamebanana humo, wamerundikana humo kama mizigo na yanapita barabarani mbele ya askari wetu wa usalama barabarani, ‘no one cares’!

Nimewahi kusimamisha daladala fulani ilibeba wanafunzi kupita kiasi, niliona huruma sana japo mwanangu hakuwamo mule, ilibidi nichome mafuta niende mpaka shule husika, nikimweleza mkuu wa shule hiyo kitendo hicho si kizuri, japo alinijibu jeuri akinihoji mimi kama nani?

Asubuhi hii nimekutana na Noah nyingine imewekwa ‘Tinted’, kilichofanya nijue kuwa kuna wanafunzi mule ni kwa sababu alikuwa anapakia, ndugu zangu inatisha, wakati anaondoka nikapaki gari pembeni na kumsimamisha dereva, alichonijibu ni jeuri tupu!

Natoa wito kwa Serikali, ilipe uzito jambo hili, yatakuja kutokea matatizo, kutakuja kutokea vifo (si uchuro, wala si utabiri au unabii), halafu kuanzia wananchi, Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali tujivike koti refu, kubwa jeusi la unafiki tupaze sauti zetu tuseme Bwana ametoa na Bwana ametwaa, ‘anyway’, labda bwana kifo, bwana ujinga, bwana uzembe, bwana upuuzi na mibwana mingine inayoishi Afrika tu na hasa Tanzania! Tuchukue hatua!