Home Latest News WATANZANIA TUCHANGAMKIE FURSA MOROCCO

WATANZANIA TUCHANGAMKIE FURSA MOROCCO

4878
0
SHARE

NA MOSES NTANDU                           |                         


Serikali ya Ufalme wa Moroco, kupitia ubalozi wake nchini imeamua kupanua wigo wa mahusiano na Serikali ya Tanzania, ili kuhakikisha wainanchi wa nchi hizi mbili wananufaika kiuchumi.

Haya yanabainika katika harakati zinazofanywa na Taifa la Morocco katika utekelezaji wa miradi kadhaa ya kimaendeleo hapa nchini, huku wakiboresha pia ushirikiano wa kisiasa ambao kwa sehemu kubwa huleta utashi wa ushirikiano wa kiuchumi.

Ubalozi wa Morocco nchini, umeamua kusimamia na kutekeleza ahadi kadhaa ambazo serikali yao ilizitoa kwa tanzaanaia kupitia Mfalme Mohamed VI.

Kwa kawaida Morocco huadhimisha siku ya uhuru kila Julai 30. Balozi wa Morocco nchini Tanzania, Abdelilah Benryane kwa mwaka huu wa 2018, ameitumia siku hiyo kama sehemu ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili Tanzania na Morocco.

Balozi huyo aliandaa hafla ambayo iliyowakutanisha watu wa kada mbalimbali za kielimu, afya, uchumi, mazingira na nyinginezo nyingi ili kukutana na maafisa wa ubalozi huo na kujadili ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, huku wakisherehekea siku ya uhuru wa taifa hilo hapa nchini, hafla iliyofanyika Julai 30 mwaka huu katika makazi ya balozi huyo hapa jijini Dar es Salaam.

Ni dhahiri Morocco inatekeleza kwa vitendo ahadi zake zilizotolewa na mfalme wa taifa hilo Mohamed VI alipozuru nchini mwishoni mwa mwaka 2016 na kuahidi kujenga msikiti wa kisasa na kiwanja cha mpira wa miguu cha kisasa huko mkoani Dodoma ahadi ambazo zinatekelezwa kwa kasi inayostahili na zipo katika hatua nzuri za utekelezaji kwa mafanikio makubwa.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli, alitembelea na kukagua ujenzi wa msikiti wa kisasa unaojengwa kwa msaada na serikali ya Morocco katika viwanja vya Bakwata Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi.

Pia maendeleo ya kuanza ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu cha kisasa huko Dodoma nayo yapo katika hatua nzuri mara baada ya kufafanuliwa kuwa taratibu zote za kiufundi zinaendelea ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa eneo la ujenzi wa uwanja huo, upembuzi yakinifu na wa kina kufanywa na wataalamu kutoka nchini Moroco.

Katika kuhakikisha kuwa mahusiano ya mataifa haya mawili yanazidi kuimarishwa ubalozi wa Morocco nchini umekuwa ukiandaa mikakati kadhaa ya kuendelea kuimarisha na kuzidisha mahusiano zaidi kwani hivi karibuni serikali ya Morocco iliandaa ziara ya ujumbe mkubwa ukiongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai kutembelea nchini Morocco kwa ajili ya kuimarisha mahusiano zaidi ya kibunge na kisiasa ujumbe ambao bado upo nchini Morocco hadi sasa.

Hali hii inadhihirisha dhamira ya kweli kutoka kwa taifa hili kuimarisha mahusiano yake na taifa letu, pia balozi Benryane amekuwa akikutana na wafanya biashara wakubwa hapa nchini ili kuhakikisha kuwa fursa za kibiashara baina ya mataifa haya zinafunguliwa na kutumika ipasavyo ili kuinua na kuboresha uchumi wa mataifa haya mawili.

Kuna kila sababu ya vikundi mbalimbali vya kiuchumi na hata wajasiriamali kutoka hapa nchini kunyanyuka na kutumia nafasi hii kutafuta na kuangalia miradi mbalimbali na fursa za kiuchumi zinazoweza kupatikana nchini Morocco ili kuzitumia kwa mstakabali wa maendeleo ya mataifa haya mawili jambo ambalo litakuza na kuinua uchumi wetu wa Tanzania na kufikia malengo ya uchumi wa kati wa viwanda.

Morocco ni taifa ambalo limepiga hatua kubwa katika sekta za nishati mbadala ambayo kwa sasa inahitajika kwa kiwango kikubwa sana katika taifa letu ambalo linatekeleza sera ya kujiinua na kufika katika uchumi wa kati wa viwanda ambapo suala la nishati ni muhimu sana kukuzwa.

Miundombinu ya reli, ujenzi, gesi, uvuvi, kilimo, elimu na afya ni sekta ambazo zimepiga hatua kubwa sana kwa taifa la Morocco ambazo taifa letu tukiimarisha mahusiano katika nyanja hozi na kutumia fursa ya kushirikiana na taifa hilo tunaweza kupiga hatua kubwa sana kwani wezetu wamepiga hatua kubwa na tunaweza kujifunza mengi kupitia wao.

Hii ni fursa muhimu sana kwa taifa letu ambapo makundi mbalimbali ya kiuchumi yanapswa kuitumia ili kuhakikisha yanapata miradi kadhaa ya uzalishaji mali ikiwa ni ama kupata fursa nchini Morocco za miradi mbalimbali au kupata wawekezaji kutoka nchini Morocco kuja na kuwekeza katika sekta hizo hapa nchini.

Serikali ya awamu ya tano hapa nchini imekuwa ikisisitiza mahusiano ya kiuchumi na mataifa mbalimbali kwa watanzania mmoja mmoja na hata vikundi mbalimbali vya kiuchumi na kijamii kujihusisha na harakati za kimaendeleo ili kuhakikisha kuwa sera ya kuingia katika uchumi wa kati wa viwanda inafanikiwa. Hivyo basi kuna kila sababu ya watanzania kutumia fursa hii iliyojitokeza kutoka kwa serikali ya ufalme wa Mohamedi Vi wa Morocco.

Uchumi wa kati wa viwanda utafikiwa ikiwa wananchi watakuwa na nia ya dhati kwa kushirikiana na serikali yao kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kishiriki na kujifunza mengi kutoka kwa wenzetu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi kama taifa la Morocco kwani wamepiga hatua kubwa sana katika nyanja nyingi za kiuchumi.

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi na mtafiti kutoka katika Kituo cha Afrika cha Mahusiano ya Kimataifa (African Centre for International Affairs – ACIA) nchini Tanzania, anapatikana kwa simu namba 0714 840656 pia kwa baruapepe mosesjohn08@yahoo.com