Home Makala WATANZANIA TUMECHELEWA LAKINI MILANGO BADO HAIJAFUNGWA

WATANZANIA TUMECHELEWA LAKINI MILANGO BADO HAIJAFUNGWA

4492
0
SHARE

NA MUDHIHIR M. MUDHIHIR

Watanzania tumechelewa kujitambua kuwa sisi ni taifa huru tunaopaswa kusimama kwa miguu yetu na kujishika kwa mikono yetu. Tumechelewa kujitambua kuwa kuishi kwa kubebwa kama maiti kwa misaada na masharti ya tunaowaita wahisani na wadau wa maendeleo, ni kustahabu kujigeuza mifugo ili tunenepeshwe na kukidhi ubora wa kutoa maziwa mengi, mayai manene na nyama ya kutosha kwa manufaa ya wakubwa.

Nasema Watanzania tumechelewa kujitambua lakini milango bado haijafungwa. Vuguvugu la kupambana na ubadhirifu na utendaji wa kimazoea na kusimamiwa kwa misingi ya uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na watendaji limeibuliwa nchini mwetu na limepamba moto vizuri. Vuguvugu hili ambalo linastahiki kuungwa mkono na kila mmoja wetu ni hatua muhimu katika jitihada yetu ya kujinasua hapa tuliponasa.

Kwa nini mapambano haya ni hatua muhimu? Ubadhirifu ndio mama wa wizi wa rasilimali muhimu na adimu za taifa ambazo ni chachu na kichocheo cha maendeleo ya taifa lolote liwalo. Ikumbukwe kuwa daima mahitaji ya taifa kama ilivyo kwa mahitaji ya mwanadamu uzani wake ni mkubwa kuliko uzani wa rasilimali zinazohitajika ili kugharamia mahitaji hayo. Hivyo wizi wa fedha za umma na ufujaji katika matumizi ni kulipunguzia taifa uwezo wake wa kuwaletea wananchi ustawi wao.

Ubadhirifu ni mama wa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Misamaha ya kodi na ushuru, manunuzi kwa bei za kurusha, kutozingatiwa thamani ya pesa katika miradi ya umma na yanayofanana na haya ni vitendo vyenye nasaba na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Uozo huu nao kwa ujumla wake hupunguza kwa kiwango kikubwa uwezo wa serikali katika kuwaletea raia wake ustawi.

Kwa nini basi balaa la ubadhirifu na kutenda kazi kwa mazoea liwe dondandugu katika nchi yetu? Bila ya kumumunya maneno tatizo hapa ni kukosekana kwa usimaizi makini. Ni vyema tukajikumbusha hapa kuwa usimamizi makini utatokana na uongozi bora. Jambo la kuwekewa msisitizo hapa ni kwamba uongozi bora ni taasisi si mtu. Kipi haramu kwa kiongozi kitokane na miiko ya uongozi si utashi wa mwanasiasa.

Katika mkutano wa Chama cha Kikomunisti cha China na vyama rafiki vya Afrika uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, tulisikia juu ya CPC kusimamia uadilifu na uwajibikaji ambavyo ndiyo siri ya mafanikio ya kiuchumi nchini China. Je, sisi tutavuna nini? Kuimarisha urafiki na China? Kuongezewa misaada isiyo na masharti kutoka China? Kuwa soko la bidhaa za viwanda vya China? Pamoja na yote hayo ni lazima tujifunze kutoka CPC umuhimu wa vyama vyetu kuwa chemchem ya uongozi bora.

Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alisema kwa ukweli na uwazi kuwa yeye angependa kuwasikia mawaziri wakitamka “Serikali ya CCM” na “Rais wa CCM”. Mimi sina shida sana na “Serikali ya Awamu ya Tano” au “Rais wa Awamu ya Tano”. Shida yangu ni iwapo baada ya Awamu ya Tano kumaliza muhula wake, Serikali ya Awamu ya Sita itayaendeleza maadili yanayotukosha wengi leo? Uongozi bora ni lazima umilikiwe na usimamiwe na taasisi.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Chama legelege huzaa Serikali legelege. Ili kazi njema ya Rais Magufuli iwe endelevu, nadharia ya uadilifu na uwajibikaji haina budi ifahamike vyema ndani ya Chama chake kwa kauli ya vitendo. Tunaweza tukatofautiana juu ya namna bora ya kuuendea uadilifu na uwajibikaji, lakini suala lenyewe la uadilifu na uwajibikaji halina budi kuungwa mkono na sisi sote. Ndio tumechelewa lakini milango bado haijafungwa.

Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni makamisaa wa chama kinachokuwa madarakani. Hawa ni wawakilishi wakuu wa Rais katika maeneo yao ya kiutawala na ndio sababu ya kupeperusha bendera katika ofisi zao na magari yao. Hawana budi kuwa na ufahamu wa kina juu ya dhana ya uongozi bora wa mujibu wa tafsiri ya Serikali ya Awamu ya Tano. Naamini bila chembe ya mashaka kuwa hili likizingatiwa tutampunguzia Rais kazi ya kutumbua majipu na vijipu uchungu.

Halikadhalika, viongozi na watendaji wa CCM ili wawe na usimamizi wenye manufaa kwa serikali wanayoiongoza, wanahitaji wawe na ufahamu mpana juu ya dhana ya uongozi bora. Wao ndio chimbuko la wabunge, madiwani, wenyeviti wa serikali za vijiji, vitongoji na mitaa. Kiongozi hawezi kukisimamia asichokifahamu na kukiamini. Mbali na ubunifu, kiongozi ni lazima aonyeshe njia kwa vitendo na yote haya yanahitaji maarifa ya uongozi na si uhodari wa kupiga maneno.

Kiongozi mwenye manufaa si yule mwenye uhodari wa kuporomosha maneno mapya kila uchao. Kiongozi madhubuti ni yule ambae huwa na tafsiri sahihi ya utekelezaji wa ILANI ya chama chake. Kiongozi makini akishatoa maelekezo kwa wasaidizi wake hubakia na dhima ya ufuatiliaji wa utekelezaji na kusaidia kuyatanzua yanayo watatiza wasaidizi wake. Ni lazima kiongozi na wasaidizi wake wawe na dhamira moja.

Kwa namna hii ya uongozi tutajenga uadilifu tunaouhitaji katika kujinasua kiuchumi na kujiletea uhuru wa kweli. Kwa namna hii ya uongozi tutajenga nidhamu ya uwajibikaji na kwa kuazima maneno ya Rais mstaafu mzee Ali Hassan Mwinyi, “Tutawalipa wafanyakazi mishahara kwa kufanya kazi na sio kwa kwenda kazini.” Kwa namna hii ya uongozi tutaudhibiti udhaifu wa kufanya kazi kwa mazoea, na kujenga hamasa ya ubunifu wenye kuleta ufanisi.

Ndio Watanzania tumechelewa lakini milango bado haijafungwa. Tunazo fursa tele katika madini na gesi. Tunazo fursa tele katika maliasili, malikale na utalii. Tunayo nishati ndani ya mkaa ambayo inahitaji kibiriti tu ili moto uwake uivishe kila kilicho kibichi. Ukiwa unaota ndoto na bado umo usingizini si rahisi kutambua kuwa umeota ndoto. Tuamke kutoka usingizini, tuitambue ndoto yetu na tuitafsiri katika vitendo.

Wimbo wa hapa kazi tu ulioanzishwa na Rais Magufuli unahitaji waitikiaji, wachezaji na wachezea ala za muziki. Basi wenye ala za upepo ingieni mzipulize zumari. Wenye ala za mitetemo ingieni myacharaze marimba. Wenye ala za mirindimo ingieni muupige msondo. Na wenye njuga na manyanga ingieni. Watanzania tumechelewa lakini milango bado haijafungwa.