Home Makala WATANZANIA TUMEJIANDAA KWA HILI

WATANZANIA TUMEJIANDAA KWA HILI

979
0
SHARE
Afisa Mtendaji Mkuu wa ACACIA, Brad Gordon

NA FARAJA MASINDE


TAKRIBANI miezi miwili sasa tangu kuwapo kwa sakata la mchanga wa madini (makinikia)unaosafirishwa nje ya nchi na hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na serikali ikiwamo kusitisha usafirishaji wa mchanga huo.

Kutokana na hatua hiyo tayari watendaji mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwamo, Waziri Sospeter Mhongo na Katibu wa Wizara hiyo wameondolewa kwenye nafasi zao kwa kile kilichobainika kuwa ni kushindwa kuwajibika.

Kampuni ya Acacia ambayo ndiyo mmiliki wa makontena hayo takribani 277  ya mchanga yaliyozuiliwa katika bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi kutoka kwenye migodi yake ya Bulyanhulu na Buzwagi iliyoko mkoani Shinyanga, ilitoa malalamiko dhidi ya kamati iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli kuchunguza sakata hilo kutokuwashirikisha ilihali ndio wenye mchanga.

Machi 29 mwaka huu Rais Magufuli aliteua kamati ya wataalamu wanane watakaofanya uchunguzi kwa lengo la kubaini kiwango cha madini kilichomo katika makontena yenye mchanga wa madini yanayokuwa yakishikiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kamati hiyo ilikuwa ikiongozwa na, Profesa Abdulkarim Mruma, mara baada ya kufanya uchunguzi wake ilibaini kiasi cha Sh bilioni 97.5 ambacho serikali ilikuwa inapoteza kupitia mchanga huo wa madini huku ikipendekeza kununuliwa kinu kwaajili ya uchenjuaji wa mchanga huo hapa nchini.

Kufuatia hali hiyo tayari Acacia kupitia kwa mwanasheria wake inatajwa kufungua kesi London, Uingereza dhidi ya serikali ya Tanzania juu ya kile kinachoonekana kuwa ni ukiukwaji wa mkataba.

Uamuzi huo wa Acacia huenda ikaipa wakati mgumu serikali ambayo imekuwa haina rekodi nzuri kwenye kesi za kimataifa.

Kwani licha ya kwamba mchanga huo ulikuwa ukiingizia hasara kubwa serikali lakini ni vyema kutambua kuwa kampuni hii ya uchimbaji madini haikujitunuku kibali au leseni ya usafirishaji na badala yake ilipewa na serikali hii hii.

Takwimu zinaonesha kwamba mchanga huo wa madini umeanza kusafirishwa tangu mwaka 2001 kwa mgodi wa Bulyanghulu na mwaka 2008 kwa mgodi wa Buzwagi jambo ambalo kila mmoja wetu ni lazima akili kwamba tumepoteza fedha nyingi kama taifa ama kwa kujua au kwa kutokujua.

Wakati serikali inaingia mikataba na kampuni hii kiongozi wa wakati huo alikuwa ni, Rais Benjamini Mkapa jambo ambalo lilionyesha dhahiri kuwa alikuwa akifahamu ni kitu gani anachokifanya.

Kuna haja kama serikali kuchukua tahadhari kubwa ili kujiweka kwenye mazingira salama kwani itakumbukwa kuwa imewahi kuteleza kwenye kesi mbalimbali ambazo imekuwa ikifunguliwa kutokana na kuenenda kinyume na mikataba.

Hakuna asiyefahamu juu ya mkataba tata wa Dowans ambao umeigharimu serikali hadi hii leo kutokana tu na kuiburuza serikali mahakamani kwa kukiuka mkataba.

Kama hiyo haitoshi bado kuna anguko jingine ambalo liliikumba serikali ya awamu ya nne lililokuwa likihusu ‘samaki wa magufuli’ ambapo matokeo yake serikali iligalagazwa mahakamani.

Matukio yote haya mawili ni mifano hai ya kuonesha kwamba serikali haina budi kuwa makini hasa linapokuja suala la kutaka kuvunja au kuingilia mkataba ya kimataifa.

Litakuwa ni jambo la busara zaidi iwapo serikali itatoa kipaumbele ya kusikiliza upande wa pili ambao ni wamilikiwa mchanga huo ili kuondoa mtafaruku unaoweza kujitokeza pindi kesi hiyo itakapotinga kortini.

Hata hivyo, usiri wa mikataba na kukosekana kwa kinu cha kuchenjulia mchanga huo na vyote vimeonekana kuwa ni chanzo kikubwa cha serikali kupoteza raslimali zake hizo inazozidai sasa, kwani  kama mikataba ingekuwa na uwazi basi madhira haya leo yasingefikiwa.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akiwa kwenye kikao cha baraza la Mjini Dodoma aliinyooshea mkono serikali juu ya sakata hilo la mchnga na kusema kuwa sheria mbovu ndizo zilizosababisha hali hiyo.

“Kibaya zaidi, CCM wamekuwa wakitumia wingi wao vibaya bungeni kupitisha sheria mbovu kwa sababu hata mwaka 1997, Bunge lilipitisha kwa siku moja sheria mbili za madini chini ya hati ya dharura na mwaka 1998, Bunge lilipitisha sheria nyingine ya madini inaweka utaratibu wa uchimbaji wa madini na kuruhusu wawekezaji kutoa mrabaha wa asilimia tatu ingawa baadaye mrabaha huo ulibadilishwa na kuwa asilimia nne, huku sheria hiyo ikiruhusu mchanga usafirishwe kwenda nje ya nchi.

“Yaani, hata mikataba yetu inaruhusu wawekezaji kupewa misamaha ya madini wakati sheria haisemi hivyo. Kwa hiyo, kinachotokea sasa ni matokeo ya CCM kutufikisha tulipofika,” alisema Mbowe.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuna hatari ya kubwa ya Kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambako mchanga huo ulipatikana, ikafungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.

“Jana nilikuwa nasoma Gazeti la Telegraph la Uingereza ambapo wanasema tatizo si wawekezaji bali ni Waafrika wanaoingia mikataba ya uwekezaji na wanasema kwa mujibu wa mkataba wetu, mchanga sio mali ya Tanzania bali ni mali ya wawekezaji.

“Kwa hiyo, kinachoonekana sasa ni kwamba nchi inaingia katika mgogoro wa kidiplomasia na wawekezaji na kama wakiamua kwenda mahakamani, hatutashinda kesi kwa sababu mikataba tuliisaini vibaya.

“Kibaya zaidi, ni kwamba kesi haitakuwa Kisutu, Kinondoni, Mwanza au Kigoma, bali itafanyika huko huko kwao,” alisema kiongozi huyo wa Upinzani.

Kwa mazingira haya serikali haina budi kuongeza umakini zaidi pindi linapokuja suala la mikataba kwani mara nyingine imekuwa ikiishia kuumbuliwa, je, tumejiandaa ha hili sawasawa?.

Iwapo taarifa hizo za kufungua kesi kwa kampuni ya Acacia dhadi ya serikali zitakuwa kweli basi ni wazi kuwa huenda ikapata kazi kubwa katika kuitetea ripoti yake ya mchanga wa madini kwenye vyombo vya uamuzi vya kimataifa.

Kwani pia kumekuwapo na taarifa zambazo zinaeleza kuwa kiwango cha madini klichomo kwenye mchanga uliozuiwa na serikali ni kinyume na uhalisia.

Kwasasa kila mtu amebaki na msimamo wake kwani wapo wanaoamini kuwa kamati hiyo imemdanganya rais,  huku wengine wakidai kuwa kiwango kilichotajwa ni kidogo ikilinganishwa na hali halisi.