Home Habari kuu Watanzania watakiwa kusamehe, kuacha kiburi

Watanzania watakiwa kusamehe, kuacha kiburi

374
0
SHARE

Na LEONARD MANG’OHA 

ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo, amesema ili kuwa mawakala wa amani, watu wawe tayari kuwasamehe wenzao kama Mungu alivyowasamehe wao na kuwarudisha katika uhusiano naye.

Alitoa kauli hiyo Jumatano wiki hii katika misa takatifu ya kitaifa ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo (Krismasi), iliyofanyija mjini Mbinga mkoani Ruvuma.

Alisisitiza kuwa watu wataendelea kuwa katika hali ya utulivu, ikiwa watakuwa tayari kuendeleza zawadi ya msamaha miongoni mwao.

Alisema watu wanapaswa kusamehe, kwa sababu kila siku wamekuwa wakisali sala ya kuomba kusamehewa makosa yao kama wanavyowasamehe waliowakosea.

“Tungetengemea kwa sala hii pasiwe na magomvi, pasiwe na ukorofi, pasiwe na ikidi na vivyo hivyo,” alisema Mhashamu Askofu. 

Askofu Ndimbo alisema kuwa, ni dhahiri jamii ambayo watu wake wanaishi kwa kusameheana ni jamii isiyo na vurugu na yenye utulivu, na kwamba pale ambapo hawasameheani utakuta vurugu na mtafaruku.

Alisema watu wanapaswa kusameheana kwa vitendo na kuwa na utamaduni wa kuvumiliana katika maisha yao, na kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kutenda haki.

“Kama Mungu amempa kita mtu utu ambao hautakiwi uharibiwe na chochote, lolote lile ambalo ni kinyume cha utu wa binadamu ni kufuru na chukizo mbele za Mungu. 

“Tutakuwa wakala na vyombo vya amani pale tunapouishi ukweli huu kwamba amani ni tunda la haki, kama nilivyodokeza hapo awali na kama anavyotufundisha Nabii Isaya. 

“Na ikieleweka katika maana pana kuwa kuuishi ukweli huo, ni kuheshimu na kujali uhalali wa vipengele vyote vya mwanadamu, haki ya uhai na haki ya kuishi.

“Tutakapojali haki ya kuishi kwa kila mmoja wetu, tutakuwa katika utulivu, tutakuwa katika amani na tutaishi kwa matumaini, lakini pale tutakapoingilia haki ya mmoja kuishi, haki ya uhai, hapo tunaanza vurugu.

“Na ninapozungumzia haki ya mtu kuishi maana yake ni haki ya uhai wa mtu kutoka kutungwa mimba mpaka pale anapochukuliwa na Mungu mwenyewe. Lakini pia kuwahifandhi wenzetu wasiokuwa na chochote chakula, malazi na mavazi.

“Tunapokosa kufanya vile lazima tusababishe mtafaruku mahala fulani kwa namna fulani, kwa sababu hizi ni haki za msingi za mtu, kula, kulala na kuvaa ni haki za msingi, zinapokosekana tayari unatonesha kidonda mahala fulani na kuleta mtafaruku katika jamii.

Alisema pia ni lazima kuhakikisha kila mmoja anapata haki stahiki ya afya na elimu, na kwamba popote pale panapofumbiwa macho katika maeneo hayo, tutatengeneza matatizo.

“Jamii isiyoelimika ni tatizo, jamii isyokuwa na afya nzuri ni tatizo Taifa, lakini pia kuhakikisha kila mmoja anapata uhuru wa kuabudu, kuwekeza na kujipatia chochote kitu, ili kukidhi maisha, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuchagua viongozi na vinginevyo.

“Hayo yanapokosekana tayari tunatengeneza, tayari tunaumba mitafaruku na migogoro katika jamii. Kwa hiyo kila mmoja lazima afungue macho na kuyaangalia maeneo haya ya msingi ya haki za binadamu, ili kuwa sababu ya kufanya lolote ili wali wasione sababu ya kufanya mtafaruku watu watulie na waishi salama,” alisema Askofu Ndimbo.

Alisema kuwa hayo ndio mambo ambayo watu wenye mapenzi mema na waliopokea upendeleo wa Mwenyezi Mungu wanatakiwa kuyafanyia kazi, na kwamba kwa kipekee hilo linawakuta Wakristo kwa namna ya pekee kama wafuasi wamisionari wa mchungaji na Kiongozi mwema na mkuu wanayesherehekea kuzaliwa kwake.

Alisema kuwa Yesu Kristo ni Mfalme wa amani, kwa sababu ndiye alifanya watu kuweza kupatanishwa na Mungu kwa kuchukua mzigo wote wa dhambi za wanadamu.

Pia aliamuru watu wapatane na kabla mtu yeyote hawajaisogelea altare au madhabahu ya kumwabudia Mungu, na kwamba mpatanishi yeyote ni msaka amani.

Kwa hiyo amani duniani kimsingi ni amani ya mbinguni, uhusiano na Kristo na sisi wanadamu, utulivu na amani katika nafsi ya Yesu Kristo ambaye katika yeye kuna muunganiko na ushirikiano na Mungu nao binadamu na ndivyo tulivyomwomba wakati wa ufunguzi wa adhimisho hili.

Alisema kuwa popote mwanadamu anaposhirikiana na Mungu katika utendaji wake ama kuishi kwake, pana amani na kwamba wakati wowote mwanadamu atakaposhirikiana na Mungu katika utendaji wake, patakuwa na utulivu na mwanatamu anakuwa salama na katika hali ya matumaini.

Alihoji ikiwa Yesu alivumilia na kuleta amani na utapanisho ulimwenguni ambako watu wengi walimkataa, sisi wafuasi wake kwa nini tusiwe tayari kubeba mzigo wowote ule ili kuleta amani na upatanisho ulimwengu?

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk.Frederick Shoo amewataka Watanzania bila kujali nafasi, vyeo na mali walizonazo, kubadilika na kuacha kiburi na mateso dhidi ya binadamu wenzao.

Askofu Shoo aliyasema hayo Jumatano Desemba 25, 2019, katika kanisa la KKKT usharika wa Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro wakati akihubiri kwenye ibada ya Krismasi.

Alisema Yesu aliyefanyika mwili anatambua maana ya mateso na inapotokea binadamu anawatesa binadamu wenzake, anamtesa Mungu.

Amesema cheo kinaweza kumfanya mtu kujisifu na kuwa na kiburi, lakini kwa wale ambao wamempokea Yesu moyoni, kiburi hakipo na hakuna sababu ya kuwa na kiburi wala kujivuna.

“Yesu Kristo akatuguse dhamiri na mioyo yetu, tubadilike, tuache kiburi, tuache kuwatesa binadamu wenzetu na tuache kufurahia kuwatesa wenzetu wasio na hatia, kwani kuna watu wanateseka hata kwenye nyumba zetu na kuna watu wanateswa, sasa baraka ya kuzaliwa Yesu ikatuletee amani,” alisema Askofu Dk. Shoo.