Home kitaifa Watendaji Serikalini msimchoshe Rais

Watendaji Serikalini msimchoshe Rais

2932
0
SHARE

NA NASHON KENNEDY

RAIS John Magufuli amehitimisha ziara yake ndefu ya kikazi katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya na katika nchi ya Malawi.

Akiwa katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya, Rais aliambatana na baadhi ya mawaziri katika serikali yake, wakiwemo Naibu Spika wa Bunge Dk Tulia Akson, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Seleman Jaffo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda, baadhi ya manaibu mawaziri, watalaam na maofisa wengine wa serikali.

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Rais aligundua upungufu mkubwa wa kiutendaji, zikiwemo baadhi ya kilichoonekana kama dalili za ufisadi, kutokuwajibika kwa baadhi ya viongozi na watendaji, kukwamishwa kwa makusudi kwa juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo na maisha bora kwa ajili ya ustawi wa maisha yao na utendaji wenye hofu usiozingatia weledi katika nyanja za uongozi, uonevu na vitisho vingi kwa wananchi wanyonge.

Akiwa mkoani Mbeya, Daktari Magufuli alijionea kwa macho jinsi utekelezwaji wa maagizo ya serikali unavyopindishwa waziwazi na watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini na hivyo kusababisha baadhi ya malengo ya serikali ya kuwaletea wanachi wanyonge maendeleo kucheleweshwa.

Uonevu, rushwa, kutokuwajibika na kufanya kazi kwa mazoea ikiwa ni nyenzo haramu iliyotumika kutekeleza kama si kukwamisha juhudi na nia njema ya Rais na serikali yake kuleta mageuzi makubwa katika utendaji wa serikali.

Kwa kuthibitisha hayo, Rais pamoja na mambo mengine, alihoji sababu zilizosababisha mwekezaji aliyebinafisishwa kiwanda cha nguo cha Mbeya (Mbeya Textile) kushindwa kwa miaka 18 kuanza uzalishaji kwa upande mmoja, lakini pia kwa sababu hizo za kutoanza rasmi shughuli za uzalishaji, serikali imenyimwa mapato kupitia kodi kwa muda wa miaka hiyo 18!

Katika kutaka kujua sababu za kubadilishwa kwa matumizi ya kiwanda hicho bila makubaliano stahiki ya serikali, kutoka kuwa kiwanda cha nguo na kuwa  kiwanda cha kuzalisha wanga unaotokana na mahindi ambapo imedaiwa kuwa kiwanda kingenunua kutoka kwa wakulima tani 40,000 za mahindi kila mwaka na hivyo kuwa kiwanda kikubwa cha kwanza katika Afrika Mashariki.

Waziri wa Viwanda na Biashara  Kakunda aliposimamishwa na Rais Magufuli kujibu mashaka ya wananchi na serikali, alionekana dhahiri ama kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu kadhia hiyo au kuficha ukweli halisi juu ya hatima ya kiwanda hicho.

Waziri huo wa viwanda na Biashara hakuwa na majibu halisi hata alipoulizwa la mtego na Rais Magufuli kwamba alitembelea mara ngapi kiwanda hicho, jambo ambalo lilisababisha Rais kumuinua Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila apate kujibu.

Katika majibu ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila, ambaye alionekana kwa kiasi fulani kutoa majawabu ya hoja hiyo na hivyo kumfanya Rais  ampe maagizo Mkuu wa mkoa wa Mbeya  pamoja na Waziri huyo wa Biashara na Viwanda  na vyombo vya sheria na dola kwa pamoja kushughulikia swala hilo katika muda mfupi na kuchukua hatua. Alimgeukia Waziri wake wa viwanda na kumwambia asipochukua hatua katika muda mfupi atachukuliwa hatua yeye pamoja na viongozi walio chini yake, hii ni aibu!

Akiwa katika wilaya ya Rungwe, Rais alihoji juu ya mradi wa maji uliogharimu mabilioni ya fedha za serikali na kushindwa kukamilika kwa wakati. Kwenye hotuba aliyotoa mbele ya wananchi waliokuwa na malalamiko kibao, Rais alisema  katika miradi ya bilioni 117 ya maji, katika maeneo ya mikoa na wilaya alizotembelea, ni kiasi cha Sh bilioni 17 tu cha fedha kilichoonekana kutumika kihalali.

Rais alionyesha mashaka yake juu ya uwezekano wa fedha hizo kutumika kinyume na makusudio ya awali ya serikali au kuibiwa na baadhi ya maofisa wasio waaminifu! Upuuzi huu ni sehemu kubwa ya uchafu wa kiutendaji katika maeneo mengi ya nchi yetu, mbali ya ubadhirifu wa fedha ya umma, lakini pia kutokuwajibika kwa baadhi ya viongozi kulitokeza waziwazi kwenye ziara yake hiyo.

Mifano kadhaa ya kuudhi ilionekana kujitokeza, Mwanamfunzi mmoja wa kike alijitokeza mbele ya Rais na kueleza kwa masikitiko na ujasiri mkubwa alivyokosa msaada wa viongozi wa wilaya na mkoa ili aweze kuendelea na masomo baada ya kukosa ada, jambo ambalo klingeweza kabisa kutatuliwa na viongozi wake wa halmashauri, wilaya na mkoa.

Lakini pia Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi(Chadema) alieleza kwa ujasiri mkubwa jinsi miradi ya maji ilivyokuwa ikifanyiwa hila na baadhi ya viongozi na kuwafanya wananchi wa Mbeya mjini na maeneo mengine kushindwa kupata maji ya uhakika, jambo ambalo lilizua kigugumizi na sintofahamu pale viongozi husika walipotakiwa kujibu hadi kumsababisha Rais kuhoji kwamba miaka yote mradi wa maji haujakamilika ila ulikamilika baada ya yeye kuwasili mjini Mbeya na kuhoji, na hapa namnukuu “ Kwani haya maji yananiogopa mimi,” mwisho wa kunukuu.

Mifano ni mingi, kwani sio nia ya makala haya kuandika kila lalamiko la mwananchi linalotokana na kukosekana kwa uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi, bali msingi wa makala hii ni kuhamasisha kwa upande mmoja na kukosoa kwa nia ya kujenga tabia ya baadhi ya viongozi wanaoshindwa kwenda na falsafa ya Mheshimiwa Rais ya kutenda kwa ufanisi ya hapa kazi tu!

Kwa viongozi hawa wanaokosa ubunifu na uthubutu wakwenda na falsafa ya Rais,  kunazalikana tabia ya kufanya kazi kimtulinga ili kuwahi wakati na muda uliowekwa katika utekelezaji wa mkakati wenyewe na kusababisha kama matokeo, uonevu, unyanyasaji, lugha ya amri isiyozingatia busara na hekima kwa wale kiongozi anaowaongoza na kuzua malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa serikali inaongoza kimabavu, jambo ambalo linaondoa kwenye vichwa  na macho ya watu wa kawaida “nia njema” ya serikali ambayo Mheshimiwa Rais anawahubiria watu mara kwa mara kwamba serikali yake ni serikali ya wanyonge na kimbilio la watu waliokosa haki. Hakika huku ni kuipaka matope serikali , Rais mwenyewe na watendaji wengine waadilifu wanaotenda shughuli za serikali kwa moyo wa kizalendo kwa uadilifu mkubwa! 

Wananchi wengi wa kawaida wasio katika katika kada ya uongozi, wanafikiri vizuri na kupata majawabu ya matatizo tuliyo nayo, na hii inatokana na kauli ya Rais aliyoitoa mjini Mbeya na hapa namnukuu “ Wananchi wana akili sana kuliko hata sisi tunaowaongoza,” mwisho wa kunukuu. Mtu mwenye akili nzuri ya kawaida, anaweza kujiuliza kuwa “ Kama mimi mwananchi wa kawaida nisingelipwa na serikali mshahara, makazi bora, tiba na marupurupu mengine wanayopata viongozi wa serikali, naweza kufikiri vizuri na kugundua tiba ya sehemu kubwa ya matatizo yetu ya kiuchumi na kijamii, ni kwanini na kwa namna gani baadhi ya viongozi wa serikali wenye kuishi kwa kutegemea kwa kiasi kikubwa kodi zetu kupitia seikalini na kupewa usafiri wa uhakika, makazi ya heshima na hata uhakika wa maisha mazuri baada ya kustaafu, wanashindwaje kuwa na majawabu ya matatizo ya wananchi  na hivyo kuwajibika kulipia kwa vitendo fadhila ya serikali inayotolewa kwao?

Viongozi wengi wa serikali wanafanya kazi kwa mazoea, kimsingi hawajishughulishi kutafuta suluhu ya changamoto za maendeleo ya wananchi ambao ndio waajiri wao, badala yake wanaonekana kushughulishwa sana na mambo binafsi, kiasi kwamba hawataki kupimwa kutokana na ufanisi kwenye malengo yaliyowekwa na serikali kwenye maeneo yao ya utendaji, wanafanya kazi kama manamba katika mashamba ya mikonge  nyakati za ukoloni na utumwa wa wafanyakazi, ambapo huviziana kati na baina ya Nokola na manamba ndio ulikuwa mtindo maridhawa.

Utaratibu huu kwa wakati ule ulitegemea nani mjanja kati ya Nokola na Manamba, ambaye angefanikiwa ama kupata ujira mkubwa kwa kazi kidogo au ujira mdogo kwa kazi kubwa, huo ulikuwa utumwa, uonevu, hakukuwa na mizania ya haki kati ya Nokola kama mwakilishi wa tajiri(Kabaila) na mwananchi (manamba).

Kwa bahati mbaya sana fikira hizi na mtindo huu wa kazi umeendelea kuwa katika akili za baadhi ya wananchi ambao kwa bahati mbaya wametokea kuwa katika nafasi za uongozi wa nchi yetu! Huu ni “msiba” mkubwa kwa taifa linaloyasaka maendeleo kwa udi na uvumba ambalo kimsingi liko nyuma ya mshale wa maendeleo yanayokusudiwa na serikali.

Baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kubuni, kuhamasisha na kusimamia maendeleo haya ambayo yanahusisha uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vidogo na vya kati kwa ajili ya kuchakata mazao na kuzalisha malighafi za viwanda katika hatua mbalimbali za utengenezaji wa bidhaa, wanakwaza jitihada za Rais Magufuli ambaye halali na haachi kuelekeza na hata kuwafukuza baadhi yao ambao wameshindwa kujirekebisha maarufu kama “tumbuatumbua,” .

Uongozi wa nchi sio lelemama, tabia za namna hii ziachwe mara moja, kama nilivyowahi kuandika katika moja ya makala iliyopita, viongozi na watendaji wa aina hii wanamchosha Rais wetu, wanadhalilisha taifa letu, wanahujumu juhudi za wananchi za kujiletea maendeleo endelevu, lakini pia ni wachochezi halisi wanaojenga uhasama kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo, baina na kati ya serikali na wananchi wake.

Ni wahujumu halisi wa jitihada za serikali za kujenga alama njema ya uwajibikaji inayoishi (legacy) kwa serikali zijazo, inajenga utamaduni mbaya kwa vizazi na vijana wanaoibukia juu ya dhana ya uwajibikaji wa watumishi wa serikali katika kutekeleza miupango murua ya serikali, hakika watumishi hawa dhahiri wanamchosha Rais Magufuli! Mungu ibariki Tanzania!