Home Habari WATU 200 KUJADILI TATIZO LA MAJI NCHINI

WATU 200 KUJADILI TATIZO LA MAJI NCHINI

1668
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA


JUMLA ya wadau wa maji 200 wanatarajiwa kukutana wiki hii, jijini Dar es Salaam kwenye kongamano maalum lenye nia ya kujadiliana fursa na namna sahihi ya kukabiliana na changamoto iliyopo kwenye sekta ya maji.

Kwa miaka mingi sasa, Tanzania ni moja ya mataifa mengi barani Afrika ambayo inakabiliwa na uhaba wa maji kwenye maeneo mengi, mijini na vijijini.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo mapema wiki hii alitoa taarifa inayohusu mkutano huo.

Taarifa ya Prof. Kitila imebainisha wazi kuwa pamoja na mambo mengine kongamano hilo, pia litajadili namna sekta binafsi itakavyoweza kushiriki kikamilifu katika sekta ya maji nchini.

Kongamano hilo litaibua hamasa kwa wakandarasi wa ndani kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maji na matumizi ya vifaa vya ndani katika ujenzi wa miradi na utoaji wa huduma ya maji kwa ujumla.

Washiriki wakuu katika kongomano hilo watakuwa ni  baadhi ya viongozi wa Serikali, Makandarasi, wazalishaji wa viwandani, wataalamu washauri, Shirikisho la Viwanda na Kilimo Tanzania  (TCCIA), wafanyabiashara, wahandisi na wahandisi washauri.

Katika kongomano hilo, mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa, kisha maazimio yataandaliwa na kufikishwa mahali husika kwa kila ngazi.

Matarajio ni kuongeza idadi ya kampuni binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya maji, kuongeza ubora wa kazi na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini.

Vilevile kongamano hilo linalenga kuongeza mchango wa sekta ya maji katika pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa kongomano hilo ni muhimu kwani bado tatizo la maji ni kubwa na kunahitajika mbinu mbadala ili kukabiliana nalo.

Mtaalamu wa Umwagiliaji kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Andrew Tarimo, alisema jamii inapaswa kuelewa kuwa maji ya juu ya ardhi tuliyonayo si mengi kama wengi wanavyofikiri kutokana na kupungua kwa kina cha maji karibu katika vyanzo vyote kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu.

Ili kuhakikisha kilimo cha uhakika cha umwagiliaji ni vema kufahamu kiwango cha maji kilichopo ardhini ambacho kinaweza kutumika kwa umwagiliaji na si maji yanayotiririka.

Alisema kutegemea maji kutoka vyanzo kama vile Ziwa Viktoria, kunahitaji gharama kubwa kuyasukuma kwenda katika maeneo ya uzalishaji, lakini kutumia maji yanayopatikana ardhini ni njia rahisi na nafuu inayoweza kuleta tija.

“Ni lazima tuwekeze kwenye ‘ground potential water’ na kuwapo kwa usimamizi wa maji, katika maeneo mengi utaona ni jinsi gani watu wanachimba visima karibu na vyoo bila kuzingatia sheria. Siamini kuwa wanapata ushauri wa kitaalamu,” alisema Profesa Tarimo.

Alisema kwa sasa mvua zimepungua katika maeneo mengi nchini na zilizopo  huanza kwa kuchelewa na kumalizika kwa wakati ule ule kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Alitolea mfano Wilaya ya Mbarali kuwa wananchi wa eneo hilo walikuwa wakiotesha mpunga kuanzia Novemba na walitegemea zaidi mvua za misimu, lakini kwa sasa hali imebadilika ambapo wakulima wamekuwa wakichelewa kuotesha mpunga na kulazimika kuchimba visima kumwagilia mashamba yao.

Alisema Tanzania inaweza kujifunza kutoka nchi zisizo na mvua nyingi kama vile Afrika Kusini ambayo hukabiliwa na uhaba mkubwa wa mvua.

“Wastani wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hiyo ukitoa mji wa Cape Province, ni milimita 400 kwa mwaka, wakati maeneo yanayopata kiasi kidogo zaidi cha mvua nchini (yaani mikoa ya Dodoma na Singida) wastani wake wa mvua kwa mwaka ni mm 600, lakini wenzetu wamefanikiwa kwenye kilimo.”

Alisema wakulima wengi wanafikiria kuwa kuendesha kilimo cha umwagiliaji ni lazima kuwa na mabwawa makubwa ambayo ni gharama kuyajenga, tofauti na ujenzi wa  mabwawa madogo.

“Nchi kama Zimbabwe ina mabwawa madogo zaidi ya 5,000 huku Afrika ya Kusini yakiwa ni zaidi ya 500,000 ambayo hutumika katika kilimo cha umwagiliaji.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi, alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa viwanda, mahitaji ya maji yataongezeka hasa katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika sekta hiyo.

“Kukosekana kwa maji ya kutosha kutasababisha bidhaa zinazozalishwa viwandani kuuzwa kwa bei ya juu, hii itasababisha wazalishaji kushindwa kumudu ushindani katika soko dhidi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi. Vile vile kutokana na viwanda vingi vinavyojengwa hutegemea malighafi za kilimo ni wazi kuwa maji yatahitajika kuwezesha kilimo endelevu kisichotegemea mvua ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha.

“Kwa mfano kiwanda kimoja cha mkonge kinatumia kati ya lita 36,000 hadi 50,000 kwa saa moja, hivyo ni lazima kuwepo mipango thabiti ya matumizi ya maji ikiwamo kurudisha maji yaliyokwisha kutumika ili yatumike tena.”

Ipo haja kwa kongamano hilo kuangalia umuhimu wa kuvuna kitaalamu maji ya mvua ili yaweze kutumika kwa muda mrefu kwenye matumizi ya binadamu na umwagiliaji.