Home Latest News WATUMIAJI WA NISHATI YA UMEME DAR WAFURAHIA HUDUMA

WATUMIAJI WA NISHATI YA UMEME DAR WAFURAHIA HUDUMA

1259
0
SHARE
Anthony Salvatory, akimwandalia mteja wake samaki wabichi

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambayo inajitahidi kuboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme  kwa wananchi wake.

Licha ya changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo Serikali katika kipindi cha hivi karibuni imejitahidi kusambaza huduma hii sio tu mjini bali hata vijijini.

Ili kupata nadharia hali ya upatikanaji wa huduma hiyo katika jiji la Dar es Salaam RAI wiki hii limezungumza na baadhi ya wakazi waishio katika Jiji hilo ambao ni miongoni mwa wanaotumia nishati hiyo katika shughuli zao za kila siku ili kujipatia kipato cha mtu mmoja na Taifa.

Wakizungumzia huduma hiyo namna ya upatikanaji wake na gharama zake kwa nyakati tofauti wakazi hao wanasema Tanesco kwa sasa wanajitahidi kuhudumia wananchi wake hasa wenye umeme tofauti na ilivyokuwa zamani.

Salim Mpemba, ni mkazi wa Manzese ambaye shughuli zake ni kusaga na kukoboa nafaka (mahidi) anasema katika kipindi cha hivi karibuni Tanesco wameweza kufanya marekebisho kwa kubadilisha nyaya za zamani hivyo hakuna tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo hasa katika kipindi  hiki.

“Hapo awali tulikuwa tunapata hasara ya kuunguliwa na mashine zetu hasa Mota ambayo matengenenezo yake sio chini ya Sh. 50,000 marekebisho yake lakini kutokana na ukarabati wa nyaya na kubadilishwa kwa Transfoma katika eneo hili hali sasa ni shwari,

“Licha ya hivyo pia watendaji wa Tanesco ni wasikivu endapo ikitakea tatizo wanafika kwa wakati na kulishughulikia lakini kwa muda wa mwaka mmoja hivi uliopita hali ilikuwa mbaya kwani kulikuwa na tatizo la kukata kwa umeme bila taarifa na wakati mwingine ukirudi unakuja kwa kasi na kwamba itulikuwa tunapata hasara mara kwa mara,” anasema Mpemba.

Aidha, anaongeza kuwa ili kupunguza matumizi ya umeme katika mashine zake anahakikisha pindi anapoziwasha kuna mahindi mengi yanayohitajika kusagwa au kukobolewa kwa wakati huo na kwamba anapomaliza kazi huzima.

Kwa upande wake Anthony Salvatory, ambaye ni mkazi wa Sinza Madukani ambaye anajihusisha na biashara ya kuuza Samaki wabichi na kuku anasema hali ya upatikanaji wa umeme ni nzuri kwa kuwa hununua umeme wa Sh. 30,000 ambapo hupata units 92 ambapo katika biashara yake huweka Kilo 100 za samaki katika friji na kwamba hutumia kwa kipindi kirefu.

“Mimi katika kupunguza matumizi ya gharama za umeme mara nyingi ninapoweka samaki huwa nawasha friji asubuhi hadi saa tano usiku kisha tunazima hadi siku nyingine tena ndio tunawasha,” anasema Salvatory.

Aborabo Abdallah, maarufu Dulla ni kinyozi katika saluni ya kiume iitwayo South Point One, iliyopo kati ya Sinza Kijiweni na Lion, anasema katika ofisi yake matumizi ni makubwa kidogo kulingana na kazi yake kwani humlazimu kuwasha A/C muda mwingi ili kuwavutia wateja wake.

“Katika kipindi cha zamani tulikuwa tunanunua hadi umeme wa Sh 40,000 kwa siku lakini sasa tunachukua wa 20,000 na maisha yanaendelea,” anasema.

Aidha, katika kupunguza gharama wakati mwingine hulazimika kuzima A/C na kuacha kutumia vifaa vingine vya umeme kama ‘Heater’ na vinginevyo.

Anasema changamoto iliyopo katika upatikanaji wa huduma hiyo ni kwamba wakati mwingine kunakuwapo na usumbufu wa upatikanaji wa umeme katika mawakala kutokana na tatizo la mtandao kwani kuna siku unaweza kuzunguka  zaidi ya vituo Sita au Saba umeme haupatikani hivyo ameomba mamlaka husika kuangalia suala hilo.