Home Latest News WAYAHUDI WAIMARISHA UBAGUZI NDANI YA ISRAELI

WAYAHUDI WAIMARISHA UBAGUZI NDANI YA ISRAELI

4923
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU 


Hivi karibuni Bunge la Israeli (Knesset) limepitisha muswada unaoitambulisha nchi hiyo  kama ‘Taifa la Kiyahudi (Jewish nation state), na kuwaweka njia panda Waisraeli ambao si Wayahudi.

Wako wanaosema kwamba sheria hiyo mpya haibadilishi chochote na kwamba utungaji wake umetokana na msukumo wa muungano vikundi vyenye siasa kali za kizalendo, kujenga hoja isiyo na msingi—imepambwa pambwa tu– kama alama ya sheria.

Baadhi yao wanasema hawaoni umuhimu wowote kisheria—uwepo wa sheria hiyo, isipokuwa kuleta madhara na shauku katika jamii na Israeili itaonekana katika jumuia ya kimataifa kama taifa la kibaguzi, sawa na ilivyokuwa Afrika Kusini kuwatenga na kuwabagua Wafrika.

Wako pia wanaosema kwamba sheria hiyo ya utambuzi wa Iraeli kuwa ‘Taifa la Kiyahudi’ hakubadili chochote—kwa sababu taifa la Israeli tangu kuundwa kwake, limekuwa taifa la kibaguzi—likiwatenga raia wasio Wayahudi—(Wapalesina) kwa vitendo na kisheria, na hata wanaoiunga mkono Israeli wanalitambua hilo.

Haingii akilini kwamba kusudio kuu la sheria hiyo ni utambuzi wa ‘utaifa wa kujiamulia mambo yao’ ni wa kipekee kwa Israeli  na Wayahudi pekee!

Hapa nyumbani wa harakati za kupigania uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alikataa dhana ya ‘Afrika kwa Wafrika tu.’ Wako waliotaka itamkwe bayana katika katiba ya chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kwamba maneno hayo, lakini Nyerere akapinga kwa nguvu zake zote. TANU kikameguka na kikazaliwa chama pinzani cha African National Congress (ANC) kikiongozwa na Zuberi Mtemvu.

Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Nyetanyahu na wanasiasa wa mrengo wa kulia, walikuwa maswahiba wakubwa wa utawala wa Makaburu wa Afrika Kusini, hawataki kujifunza kutoka historia—kwamba katika karne hii, ubaguzi wa aina yoyote ile—wa rangi, asili au utamaduni, ni mambo ya kizamaani (archaic), umepitwa na wakati. Isitoshe, historia inaeleza jinsi Wayahudi walivyoishi kwenye maghetto (Jewish Ghettos—miji au maeneo yao tu) katika karne ya 13 katika nchi za Ulaya ya Kati—Belarus, Lithuania na Moldova na sehemu za Ukraine na Poland.

Katika miji ya Ulaya Magharibi na Kati, kulikuwa na maghetto katika miji ya Roma, Frankurt na Prague.

Kipindi cha giza cha cha Wayahudi katika Ujerumani (miaka ya 1930), walikamatwa kirahisi (kama panya), na utawala wa Adolf Hitler kutoka kwenye maghetto. Walipotambua kosa la kujitenga, wakapaza sauti kwamba watambulike kama sehemu ya jamii katika nchi za Ulaya. Kukazuka hata dhana ya kuondoka Ulaya wakanzishe taifa lao Uganda. Kulazimishwa kuishi kwenye ghetto katika karne ya 19 ilikuwa jambo moja, kujitungia sheria ya kuishi hivyo kwenye karne ya 21, ni jambo jingine.

Leo kizazi cha kina Netanyahu kimesahau historia hiyo, kinataka kujenga miji kwa ajili ya Wayahudi tu!

Wayahudi wanataka kuiambia dunia kwamba wako tayari kwa njia yoyote ile, kuulinda Uyahudi wao katika Israeli kwa nguvu zote hata kama ina maana ya kukanyaga haki za watu wengine ambao sio Wayahudi.

Sheria hiyo haitaji namna Wayahudi watakavyoweza kuhakikisha kwamba ni wao tu wenye haki ya kujitawala (self-determination), jambo ambalo ni kinyume cha misingi ya demokrasia na haki za binadamu.

Wachambuzi wa mambo wanasema sheria hiyo ina mambo yaliyofichwa—inaanda misingi ya ya kutunga sheria elekezi kwa Makama ya Juu—kutoa kipaumbele kwa Waisraeli wenye asili ya Kiyahudi tu. Kwamba Wayahudi ni tofauti na mataifa mengine—kwamba Israeli ni nchi ya kidemokrasia kwa Wayahudi tu.

Sheria hiyo umekwenda mbali zaidi—inaunda maeneo ya kuishi Wayahudi tu, kama Kaburu alivyounda Bantustani—kitu abacho baadhi ya Wayahudi wenye kuona mbali wanapinga. Moja ya misingi ya matatizo ya Israeli ni ujenzi wa ‘kibbutz’ (vijiji vya ujamaa). Wayahudi waliunda kamati za kuwaruhusu wahamiaji waliokuwa wahamia Palestina (1948/49). Kamati hizo ziliwakataa watu ambao sio Wayahudi.

Mahakama ya Juu ya Israeli iliruhusu sheria ya kuunda kamati za kibbutz—uwamuzi ambao wanasheria wanasema unaruhusu kanuni ya kutenganisha makundi ya kijamii.

Ni katika msingi huo, Wayahudi, kwa kadiri wanavyoongezeka, wananyang’anya kwa nguvu za kijeshi ardhi ya Wapalestina mpaka leo. Wapalestina (2.2m), ambao ni raia wa Israeli, hawana sauti na ni kama raia daraja la pili pamoja na Waisraeli wingine ambao kwa asili sio Wayahudi. Kwa sheria hiyo, Wapalestina hawana haki ya kupinga ubaguzi na kudai haki kwa raia wote.

Lakini miaka ya hivi karibuni, pamekuwapo na vikundi vya uwakilishi wa Wapalestina—Katiba ya Kidemokrasia (Democratic Constitution) na Kamati ya Kitaifa ya Wakuu wa Mamlaka za Kiarabu katika Israeli (National Committee for the Heads of Arab Local Authorities in Israel). Vikundi hivi vilitoa tamko ambalo linaitwa Azimio la Haifa. Kwa jumla azimio hilo, linapinga ‘umbo la taifa la Israeli’ lilivyo hivi sasa—jinsi taifa hilo linavyojiona, muundo wa serikari yake, na utambulisho wake wa Kiyahudi (Zionist).

Aidha, sheria hiyo inafuta lugha ya Kiarabu kama moja ya kugha za taifa na kuruhusu makazi kwa jamii zinazozungmza lugha moja ma dini moja.

Wajuzi wa mambo wanasema kwamba sheria hiyo inabadilisha uwiano wa jamii za Kiisraeli na kusababisha utengano kama taifa. Wanasema nchi inaweza kuwa taifa moja, lakini unapoanza kuwabagua baadhi ya watu, unaua utaifa wako. Chini ya sheria hiyo, inatoa mamlaka ya kuunda vijiji vyenye watu wa aina moja kwa misingi ya dini, race au utaifa—jambo ambalo halikubaliki.

Lakini, pamoja na kutungwa kwa sheria hiyo,ni kama hitimisho tu—maeneo mengi—mijini na vijijini ndani ya Israeli yametenganishwa kwa misingi hiyo—maeneo ya Warabu au Wayahudi pekee, ni vigumu kwa Warabu kuchanganyika na Wayahudi katika makazi hata kabla ya sheria hiyo kuwapo. Mwalimu katika Chuo Kikuu cha Hebrew cha Jerusalem, Mordechai Kremnitzer, amenukuluwa akisema kuwa sheria hiyo sasa imelivua ‘mask’ taifa hilo na kuonesha sura yake mbaya na ya kuchukiza.

Sheria huyo pia imewagawa Wayahudi waishio nje—hasa Wamarekani wenye msimamo wa kiliberali—ambao wanaona kama Wayahudi wafuasi wa imani halisi (orthodox), watapewa kipaumbele dhidi yamadhehebu mengine. Rais wa Muungano wa vyama vya Mageuzi ya Dini ya Kiyahudi (Judaism), Rabi Rick Jacobs, anasema sheria hiyo ilikuwa ni tishio kubwa kwa demokrasia na itavuruga uwiano wa Wayahudi waliowengi na Warabu ambao ni wachache, na kukichimbia kikundi kidogo cha Wayahudi wahafidhina (orthodox), na kuwacha pembeni Wayahudi walio wengi. Kiongozi wa mfuko unaounga mkono vikundi vinavyo pigania haki—New Israel Fund, amesema sheria hiyo ni sawa na zaidi ya ukabila mbaya.