Home Habari Waziri wa Kikwete afunguka

Waziri wa Kikwete afunguka

2613
0
SHARE

>>Aelezea ugumu wa uwaziri

>>Mawaziri wengi hawajui kukusanya mapato wanajua kutumia tu

NA GABRIEL MUSHI

Aliyekuwa Waziri wa zamani wa fedha katika ungwe ya mwisho kwenye Serikali ya awamu ya nne, Saada Mkuya amebainisha namna nafasi hiyo ya uwaziri ilivyokuwa ngumu katika kipindi chake. RAI linaripoti.

Mkuya ambaye ni mwanamke wa pili kutoka Visiwani Zanzibar kuiongoza wizara ya fedha katika kipindi cha uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, alisema licha ya kufanikiwa kuongoza vema wizara hiyo, kulikuwapo na mkururo wa matukio muhimu yaliyohitaji matumizi makubwa ya fedha.

Katika mazungumzo yake na RAI wiki hii, Mkuya ambaye pia ni Mbunge wa Waelezo (CCM), alisema nafasi hiyo aliitumikia katika kipindi kigumu cha mageuzi kuliko mawaziri wote.

Aidha, alisema hatosahau vurugu za wafanyabiashara waliokuwa wakipinga matumizi ya mfumo mpya wa mashine za kielektroniki wa ukusanyaji kodi (EFD).

Pamoja na hilo alisema kilikuwa ni kipindi kigumu kwa sababu Taifa lilikuwa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, uandikishaji wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR) na uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

“Kilikuwa kipindi kigumu, kwa sababu tulikuwa tunaelekea kwenye chaguzi mbili, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Lakini pia ndani yake kulikuwa na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, uanzishaji wa matumizi ya mashine za kielektroniki katika kupiga kura, kukamilisha mchakato wa Katiba mpya. Hayo yote yalikuwa yanahitaji fedha.

“Ingawa tulikuwa tunapanda katika ukusanyaji wa mapato, ila matumizi yalikuwa makubwa, kwa sababu kuna mishahara ya watumishi na ulipaji wa deni la Taifa, ujenzi wa miundombinu kama vile airport terminal III, ujenzi wa madaraja  makubwa, ujenzi wa mradi wa umeme wa Kinyerezi II. Pia tulikuwa tunakusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR.

“Hakika ulikuwa ni wakati mgumu kwa sababu lazima ukusanye fedha, ili yote hayo yasonge mbele, ila nashukuru Mungu tulifikia pazuri na sasa Rais John Magufuli ameweza kutekeleza malengo mbalimbali tuliyoyaandaa kama vile ununuzi wa ndege,” alisema.

Alisema kwa nafasi ya uwaziri wa fedha ni ngumu kutumikia wananchi moja kwa moja ndio maana wateule wengi wa nafasi hiyo huteuliwa kwa malengo ya kutumikia Taifa.

Mkuya ambaye alianza kutumikia nafasi ya Naibu Waziri wa Fedha kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 alipokuwa waziri kamili, mbali ya kuwa na uzoefu katika wizara hiyo alishtuka apopatiwa taarifa za uteuzi wa uwaziri katika wizara hiyo.

“Kwanza nilishtuka, licha ya kwamba nilikuwa Naibu Waziri wa Fedha, ila ni kitu ambacho kilikuja ghafla, niliwaza sana. Hata ile nafasi ya Naibu Waziri nilishtuka kwa sababu niliwaza nitaongea nini bungeni. Nilikuwa sina habari ndio kwanza nilipigiwa simu.

“Lakini namshukuru Mungu tulifanya kazi vizuri na Dk. Mgimwa (Mwenyezi Mungu amrehemu) nilipata uzoefu mkubwa ndani ya ile nafasi kwa kujibu maswali bungeni pamoja na mambo mengine. Ila kuwa waziri nilishtuka zaidi ilinipa hofu kubwa si kwa sababu mwanamke ila ni vipi nitaweza kushibisha matarajio ya watu,” alisema.

Hata hivyo, alisema moja ya changamoto kubwa ilikumsibu na muda mwingine kukukwamisha katika utekelezaji wa majukumu yako kama waziri wa fedha, ni uhamasishaji wa matumizi ya mashine za EFD.

“Kubwa ilikuwa ni matumizi, na mahitaji ya dharura ambayo fedha zake hujazipangia kama vile maafa na mengine. Ila kitu ambacho tunaweza kujivunia ni uanzishaji wa EFD, uanzishaji wa mfumo huu ulikuwa unakataliwa sana na wafanyabiashara, ilibidi nitembee kwenda Kariakoo kuzungumza na wafanyabiashara, walikuwa wanaandamana, wanafanya makongamano kupinga matumizi ya EFD,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa nafasi ya waziri wa fedha huaminika kuwa kazi yake ni kukusanya fedha huku mawaziri wengine jukumu lao likiwa ni kuzitumia pekee jambo ambalo si kweli.

“Unajua waziri wa fedha anatazamwa kama anakusanya mapato, lakini pia mawaziri wengi walikuwa hawajui suala la kukusanya mapato ni jukumu la pamoja, wao walichojua ni matumizi tu. “Changamoto ilikuwa ni kwamba kama hamuendi pamoja, ndio tatizo kwa sababu hata wao wanatakiwa kukusanya kodi kama vile kwenye masuala ya ardhi na utalii. Lakini walikuwa wanamtegemea Waziri wa Fedha pekee. Hapakuwa na waziri ambaye anahamasisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya EFD.

“Lakini sasa tunashukuru limepita na kukubalika, utake usitake utatumia. Na hili ni jambo zuri sana katika ukusanyaji wa mapato ya serikali,” alisema.

… wanasiasa wanapotosha kuhusu ukuaji wa uchumi

Kutokana na kuwapo kwa malalamiko kuhusu hali ngumu ya maisha huku serikali ikidai uchumi umekuwa, Mkuya alisema ipo haja ya kuwaelimisha wananchi kuhusu hali hiyo.

Alisema  mageuzi mengi yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tano yatachukua muda kwa wananchi kuyazoea.

“Kwa mfano, sasa serikali inakusanya mapato ila inawekeza kwenye miundombinu ya kiuchumi, miundombinu hiyo ikishasimama mwananchi ataitumia kuboresha maisha.

“Hali hii ni kawaida, lazima wananchi waitambue. Kuna masuala ya madini, gesi, usimamizi wa rasilimali za nchi, haya ni mageuzi makubwa sana lazima mwananchi atasikitika,” alisema.

Alisema asilimia kubwa ya wananchi na wanasiasa wanachanganya kuhusu ukuaji wa uchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja kwa kupima kwa muda mfupi.

“Kwamba tukisema uchumi umekua kwa asilimia 7, kila mwananchi au wanasiasa wanataka waone kuwa wananchi wanapesa, upimaji huwezi kulinganishwa na wananchi kujazwa mapesa.

“Ukuaji wa uchumi unapimwa kutokana na thamani ya huduma na bidhaa tunazozizalisha katika kipindi cha mwaka mmoja. Kwa mfano, Januari mpaka Disemba, ni kiasi gani cha bidhaa na huduma kilichozalishwa sasa ile thamani yake ndio tunapima kutokana na shughuli mbalimbali kama kilimo, huduma za fedha, ujenzi, huduma nyingine nyingi ambazo tumezalisha katika kipindi kile,” alisema.

Alisema uchumi wenyewe unatakiwa kuakisi kwa wananchi kwa kupitia upatikanaji wa huduma muhimu kama vile ujenzi wa miundombinu, uboreshaji wa huduma za elimu, maji, afya na upatikanaji wa pembejeo ili mwananchi aweze kufaidi huduma hizo.

“Sasa watu wanapima katika kipindi kifupi na kulinganisha na fedha zilizopo katika mifuko yao. Ni vitu ambavyo vinahitaji mwamko wa elimu, ili kutumia fursa zilizopo kujiongezea kipato.

Sasa tupo katika mageuzi ya viwanda. Ili tuweze kuuza zaidi nchi za nje kuliko kununua  zaidi,” alisema.

Itakumbukwa kuwa katika uongozi wa Rais Kikwete, ulitoa nafasi kwa wanawake, kwani katika awamu yake ya kwanza, alimteua Zakhia Meghji kuiongoza Wizara ya Fedha (2006 hadi 2008) huku Mkuya akishika wadhifa huo kuanzia 2014 hadi 2015.