Home Makala Wingi wa benki si nongwa bali…

Wingi wa benki si nongwa bali…

844
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Kwa mujibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, Tanzania inayo mabenki ya Biashara 53. Idadi hii ukiitazama kwa jicho lisiloangalia umuhimu wa sekta hii, unaweza kudhani ni kubwa sana.

Kwa mantiki nyingine, wingi wa mabenki si tatizo na hasa kama yanaingiza mtaji hapa nchini. Kama yanategemea mtaji wa kujiendesha kutoka ndani na kwamba yanakuja yakiwa na mtaji pekee unaoyataka ili yapate leseni basi hapo kuna tatizo.

Kinyume na matarajio ya wengi, sekta ya benki hapa nchini imekuwa ikisuasua na hata pale ilipofanya faida ilikuwa ni vigumu kubainika kwa wengi. Sababu kubwa ya hali hii ni kutokana na hali ya kibiashara wakati nchi yetu ikipata uhuru, hali ya kisiasa wakati huo na hali ya kiuchumi pia.

Mfumo wa nchi yetu haukuhamasisha biashara na hivyo benki zikawa kama sehemu mbadala ya kutunzia fedha. Hata matangazo ya kuhamasisha watu kufungua akaunti yalilenga kuwapa taarifa za kuwaepusha na kupotea ama kupatikana madhara kama moto katika majumba yao, hivyo wakatakiwa kufungua akaunti na kutunza fedha zao.

Benki zilitazamwa kama begi salama la kuweka fedha na hakukuwa na mkakati wa wazi hasa kwa watanzania weusi, kwamba benki ni eneo la kutunza fedha, kutoa mikopo na kufadhili shughuli za maendeleo kwa wananchi. Benki hazikutajwa kama daraja la kuwafanya wananchi wabadili aina ya maisha yao kutokana na kazi wanazofanya au hata kubuni kazi mpya.

Benki kwa mantiki hiyo zikabaki kama eneo la wafanyakazi wa kawaida kupitishia mishahara yao. Kwa lugha nyingine benki zikachukua kazi ya wahasibu. Ni siku za hivi karibuni tu ambapo benki zimeanza kufungua madirisha ya mikopo, mikopo ambayo imebakia na riba kubwa inayowafanya wakopaji wadogo kubakiwa na lindi la umaskini badala ya kuwakomboa kiuchumi.

Sababu zinazotumiwa na mabenki haya kutoza riba kubwa kwa wananchi moja inayoelezwa sana ni kuwa, watanzania hawana nidhamu ya kulipa mikopo na pia ni vigumu kuwapata pale inapotokea wameshindwa kulipa mikopo hiyo. Hali hii kwa namna moja ama nyingine ilikuwa inajenga kutoa adhabu hasa kwa wananchi wenye vipato vya chini sambamba na vile vya kati.

Bima kubwa ikachangia wananchi wengi kuachana na kukopa katika mabenki na hivyo kile wanachokipitishia katika benki kuchukuliwa siku ile ile kinapoingia au kubakiza kiasi kidogo kwa ajili ya matumizi. Tabia hii ikajenga pia suala la wananchi kuzigeuza benki madirisha tu na sio sehemu yao ya kuhifadhi fedha kibiashara.

Siri kubwa ambayo imeibuliwa na Rais Magufuli hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari ni kuwa, mabenki mengi nchini yalianzishwa kwa lengo la kuvizia biashara za serikali. Hoja hii ni mpya lakini nzito katika kudumaza suala la wananchi kukopa katika mabenki.

Siri hii inabainisha kuwa, mabenki yalikuwa na njia nyingine ya kupata faida na kamwe hayakulenga kufanya biashara ya kibenki inayotegemea wananchi wa nchi hii. Ndio maana mabenki mengi yakajikuta yanajazana katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Mengine yameweza kuvuka tu katika miji mikuu ya mikoa. Na mengine yako katika wilaya kwa sababu tu, yamerithi mtandao wa ofisi na rasilimali ambazo zilikuwepo tangu awamu ya kwanza.

Rais Magufuli anasema: “Machifu Executive Officers asilimia kubwa wamekuwa wakifanya biashara na mabenki. Anachukua fedha zile anaenda anaziweka kwenye fixed deposit akaunti za mabenki. tuna mabenki 53. Yale mabenki baadaye yanafanya biashara na serikali kwa kununua treasurer bills. Fedha zimewekwa pale kwa asilimia 8, serikali inakwenda kununua mule kwenye mabenki kwa kukopeshwa kwa asilimia 15 mpaka 16.”

Kutokana na msingi huu, Rais kabaini wazo jema ambalo kwa namna moja ama nyingine limeyafanya mabenki yetu hapa nchini yaliyokuwa yakitegemea biashara na serikali kujikuta hayawezi kutanuka na kwenda nje ya mipaka ya nchi yetu. Ni benki moja tu ambayo imevuka mipaka huku zingine nyingi zikiwa zinatoka nje na hata zile zilizoanzia hapa zikiwa na ubia na watu wa nje.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, ili upate leseni ya Benki ya Biashara unahitaji kiasi cha mtaji wa shilingi bilioni 12, huku pia ukihitaji kiasi cha shilingi bilioni 2 tu kuanzisha benki ya kijamii (Community Bank). Kwa lugha nyingine, mtaji huu ni mdogo kuyafanya mabenki kutanua shughuli zake na kuwafikia masikini. Inahitajika mtaji mkubwa ili uwafikie wanufaika wengi na kwa wingi wao iwe rahisi kurejesha mtaji na faida.

Uganda inayo mabenki 25 huku Rwanda ikiwa na idadi ya mabenki 12. Kenya ambayo inafanya vema katika sekta hii inayo mabenki 42 yenye usajili wa ndani pamoja na mengine 7 yenye uhusiano na mabenki ya nje. Nchi ya Burundi inayo mabenki 10 tu.

Ukitazama takwimu hizo na ukizingatia ni benki moja tu iliyotoka Tanzania na kwenda Burundi unaona picha ya kwa nini serikali imeamua kubana mirija yake ili kuleta ushindani wa kimtaji na kuondoa ubabaishaji. Kwa lugha nyingine, sekta hii licha ya kuwa inaendana na malalamiko ya kukosa biashara za serikali, ilikuwa chini ya mtaji huo tu ambao pia ulikuwa hauna tija kwa watumiaji wa huduma za kibenki hapa nchini. Ukimuuliza mwalimu wa shule ya msingi faida ya mshahara wake kupita benki atakuambia amepunguziwa kadhia ya kusimama foleni katika dirisha la mhasibu.

Kimsingi mwalimu huyo kwa kupitisha fedha yake kwenye benki alipaswa kupata aina mpya ya riba anapotaka kukopa. Riba yenye unafuu kwa kuwa tayari naye anachangia katika maendeleo ya benki husika.

Haya hayafanyiki na huenda ni kutokana na benki kumuona mwalimu huyu kuwa daraja tu la mafanikio yao na kwamba si mteja wanayemtegemea sana. Mteja wao alikuwa ni serikali.

Ukweli unaonesha kuwa mabenki yaliyotegemea serikali yataendelea kupungua mtaji na yataathirika sana si kwa kuwa yalikopesha wananchi wa kawaida walioshindwa kulipa mikopo, bali wananchi walitumika katika sehemu tu ya kiini macho cha biashara hii ambayo Mtanzania mweusi hakuwwahi kufanywa rafiki wake tangu nchi hii ipate uhuru.