Home Habari Wizara ya Viwanda mtihani kwa mawaziri

Wizara ya Viwanda mtihani kwa mawaziri

983
0
SHARE

>>JPM aamua kusimamia hoja za Watanzania, mawaziri watatu wapishana mlangoni

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WIZARA ya Viwanda na Biashara sasa inaonekana ni mtihani, huku kila waziri anayeteuliwa anaonekana kushindwa kusimamia misingi ya Tanzania ya viwanda, hali inayomfanya Rais Dk. John Magufuli kuwabadili wanaoshindwa kwenda na kasi yake.

Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na vilio kila kona kwa wafanyabiashara, ikiwamo wamiliki wa viwanda kukosa ushirikiano na viongozi wa wizara hiyo jambo linalochangiwa na urasimu na kushindwa kufikiwa kwa uamuzi wa haraka.

Hadi sasa tayari Rais Magufuli ameshabadilisha mawaziri watatu katika wizara hiyo, huku akiweka wazi namna wateule wake wanavyomwangusha kwa kushindwa kwenda na kasi ya Serikali yake na kushindwa kutoa matokeo mazuri mbele ya Watanzania.

Mawaziri ambao hadi sasa wameongoza Wizara ya Viwanda na uteuzi wao kutenguliwa ni pamoja na Charles Mwijage, ambaye aliondolewa Novemba 10, mwaka jana baada ya Rais Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua mawaziri wawili na naibu mawaziri wanne.

Katika mabadiliko hayo Rais Magufuli alimteua Japhet Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, akachukua nafasi ya Dk. Charles Tizeba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Pia Rais Magufuli alimteua Joseph Kakunda kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Sasa masuala ya uwekezaji yameundiwa wizara yake – Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya Uwekezaji, ambayo inaongozwa na Angella Kairuki.

Kabla ya uteuzi huo, Kakunda alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na alichukua nafasi ya Charles Mwijage ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Katika mabadiliko hayo madogo ya Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli alimteua Innocent Bashungwa kuwa Naibu wa Wizara ya Kilimo, ambaye Juni 7, mwaka huu aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, ikiwa ni siku moja baada ya Rais kukutana na wafanyabiashara kutoka wilaya zote Ikulu, Dar es Salaam.

Hatua ya kufanyika kwa mabadiliko kwa mawaziri kadhaa katika Wizara ya Viwanda na Biashara ilianza baada ya Mwijage kushindwa kusimamia masoko ya mazao ya korosho na pareto huku wakulima wakiendelea kulalamikia hatua hiyo.

MATARAJIO YA JPM

Akiwaapisha waziri mpya wa Viwanda na Biashara, Bashungwa na Kamishna wa TRA, Dk. Edwin Mhede Juni 10, mwaka huu Ikulu Dar es Salam, Rais Magufuli, ameeleza hadharani sababu 12 zilizosababisha atengue uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere ambaye naye alimwapisha kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Alisema jukumu lake ni kuteua na anapotengua uteuzi wa mteule wake si kwamba anamchukia mtu, bali anataka kuona matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kuwa anapomteua mtu anataka kuona matokeo mazuri.

“Nampongeza Kakunda kwa kuja hapa, huku ndiko kukomaa kisiasa, hizi kazi ni ‘temporary’, lakini ni ukweli kwamba kwenye wizara ‘hakui – push’ ninavyotaka mimi.

“Changamoto za wafanyabiashara, kwani palikuwa na ubaya gani naibu waziri, katibu mkuu, waziri mwenyewe si wangeshapanga mikutano na wafanyabiashara msikililize shida zao, nani aliwakataza?

“Ndio maana wanakuja wanasema hawajawahi kumuona, lakini hata ningewauliza labda (Naibu Waziri Stella) Manyanya wangesema hawajawahi kumuona,” alisema Rais Magufuli.

Alisema licha ya wizara hiyo kuwa na jukumu la kufanya biashara, imeshindwa kutafuta masoko ya mazao mbalimbali ikiwemo korosho iliyokusanywa kwenye maghala.

Alisema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi ilikusanya korosho tani 223,000 lakini Wizara ya Viwanda na Biashara imebangua tani 2,000 tu.

“Zingine wanasubiri mpaka nani ateremke ndio awaambie, sasa mnatakiwa kuuza hizi korosho, wizara inaitwa Viwanda na Biashara ni biashara gani imefanya?

“Korosho zimekaa wakati Tanzania ndio tulikuwa wazalishaji peke yetu, tumesubiri hadi Machi nchi nyingine zikaingia bado hatujauza. Unakuwa na liwizara la kupeperusha bendera barabarani,” alisema.

Rais Magufuli alisema pia licha ya wizara hiyo kuwa na vyombo mbalimbali, lakini vimeshindwa kuonesha uwajibikaji hasa katika kutafuta masoko. 

“Wizara ina vyombo vyote vya kufanya biashara, Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara) ipo pale… ilitakiwa niifagie (wizara) kutoka juu hadi chini,” alisema.

Alisema pia viwanda vingi vilivyobinafsishwa havifanyi kazi, huku vingine vikibadilishwa matumizi akitolea mfano Kiwanda cha nguo Mbeya ambacho kinakusudiwa kubadilishwa kiwe cha kutengeneza pipi.

BASHUNGWA NA POLE

Mkuu huyo wa nchi alisema; “Innocent (Waziri wa Viwanda) inawezekana wamekupongeza, lakini nilifikiri wakupe pole… mimi naangalia haya nikiona hayaendi natengua.

“Jukumu langu ni kuteua ili kukidhi kiu ya Watanzania, na ninapotengua mahali si kwamba wewe nakuchukia, nakupenda tu. Watanzania walionichagua wanataka waone utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.”

TRA NA MAKUSANYO

Akizungumzia TRA, alisema Dk. Philip Mpango alipokuwa kamishna wa mamlaka hiyo, alipandisha makusanyo kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3 hatua iliyosababisha ampandishe cheo kuwa waziri, lakini akashangaa kiwango hicho kubaki hivyo hadi sasa.

“Sasa wengine mnasimamia hapo hapo kana kwamba hiyo ni ‘formula’ ya Mungu, lakini pia tatizo malalamiko ni mengi na hamchukui hatua.

“’Message’ nilizokutumia (Kichere) ni zaidi ya 30, zingine saa 8 usiku, anasema nimepokea mheshimiwa, ukifuatilia hakuna matokeo,” alisema.

Rais Magufuli alisema kero nyingine katika mamlaka hiyo ni makadirio ya kodi yaliyosababisha wafanyabiashara wengine kuamua kukwepa ama kughushi.  

“Haiwezekani mkurugenzi wako anatoa ‘estimate’ za kijinga na wewe upo tu unamwangalia wakati una nguvu, unaona kabisa makusanyo kodi ya ndani yanashuka halafu hakuna hatua.

“Wapo wafanyabiashara mazingira yalikuwa yanawaruhusu kughushi, kakae nao waseme wanaweza kulipa kiasi gani, una mamlaka hata ya kusamehe ‘some percentag’,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wanapakia mizigo kwamba inaenda nchi jirani, wanafika Tunduma wanagongewa mihuri wanarudi kuja kuishusha huku wakati barabarani kote TRA iko.

Suala lingine kwa mujibu wa Rais Magufuli ni urasimu wa kushikilia vifaa bandarini na kusababisha kukaa muda mrefu huku mteja husika akishindwa kufanya biashara.

“Unashikilia vifaa vya kuja kuchimba dhahabu vimekaa zaidi ya mwaka mzima, badala ya kuangalia atakapokuja kuwekeza ataleta ajira na Serikali itapata mapato… utafikiri watu wa TRA wote hawakusoma.

“Na walipokusema siku ile ninakuuliza wala hujui unamwangalia wa nyuma yako, kwahiyo tumekupeleka huko (akimaanisha Njombe) ukisimamia vibaya na kule nako tunakutoa.

“Unafahamu Wahehe ukichukia huwa wanajinyonga, basi nafuu ukajinyonge. Kawaambie ukweli, kuna watu wamebobea ni ‘untouchable’, usicheke na mtu, kakusanye kodi kwa ajili ya Watanzania, bila kodi hakuna nchi,” alisema Rais Magufuli.

Alimtaka kamishna huyo kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi wasio waaminifu na ikibidi kuwafukuza kazi au kuwapeleka mahakamani.

“Kama una wafanyakazi 1,000, 100 au 200 wakiishia kufukuzwa na kwenda mahakamani ‘that is fine’. Kwanza jana (juzi) nilikutumia ujumbe wa mtu mmoja analalamika kabla hata sijakuapisha, kwahiyo nenda ukafanye kazi.

“Kuna makamishna katika mipaka, iko inayofanya kazi vizuri Lusumo anafanya kazi vizuri, lakini Tunduma, Sirari hawafai. Wa Tunduma alikuwa anaratibu kugonga mihuri ya mizigo inayotoka Dar es Salaam kwamba iko ‘on transit’.

“Na wale wa chini watoeni, msiwabembeleze watu wamekula vya kutosha, wengine wapelekeni kwenye wizara zingine wakasome magazeti…mlete hata ‘messenger’ kwenye ofisi yangu,” alisema.

Kuhusu Mkoa wa Njombe alisema una changamoto nyingi na kumataka Kichere kwenda kufanya kazi kuubadilisha.

“Hata viongozi hawaelewani vizuri, kajenge mahusiano nao Njombe ibadilike,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI WA FEDHA

Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, alimtaka kamishna mpya wa TRA kuongeza ukusanyaji wa mapato na kusafisha sura ya mamlaka hiyo.

“Dk. Mhede karibu sana TRA, kuna changamoto lakini mtangulize Mungu. Walipoongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3 tangu wakati ule wastani ule unazunguka hapo hapo kila mwezi, lakini mahitaji ya taifa letu ni makubwa.

“Una kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tunaondoka hapo kwenye huo mnato, jitahidi uongeze hapo walau Sh bilioni 450 nyingine tufike Sh trilioni 1.7.

“Sura ya TRA ina matope kwa maana ya mahusiano yenye mushikeli na wafanyabiashara na walipakosi kwa ujumla, hivyo safisha sura hiyo iwe ni mamlaka ambayo wafanyabiashara na walipakidi wote wanatambua kwamba ni chombo chao ni rafiki kwa Watanzania,” alisema Dk. Mpango.

BASHUNGWA NA TUMAINI KWA JPM

Waziri wa Viwanda na Biashara, Bashungwa alisema ana deni kubwa na kwamba amejipanga kutatua changamoto zilizoko kwenye wizara hiyo na kufikia azma ya nchi ya kuwa na uchumi wa viwanda. 

“Nitaitendea haki hii nafasi kwa kufanya kazi usiku na mchana kutatua changamoto ambazo zitakidhi matarajio yako na Watanzania kwa ujumla,” alisema Bashungwa.

Alisema wizara hiyo ni mtambuka, hivyo watahakikisha wanatatua changamoto za wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo.

“Changamoto nyingi wanazolalamikia ziko kwenye mapungufu ya sera na muundo wa kitaasisi, tutawashirikisha wenzetu wa wizara nyingine kuhakikisha tunakuwa na ‘action plan’.

“Nimekuja kwenye wizara ya viwanda ambayo ni pacha na wizara ya kilimo hivyo, nitaendelea kushirikiana nao ili kupitia mazao yetu ya kimkakati tuweze kuwasaidia wakulima nchini,” alisema Bashungwa.

KICHERE NA SHUKRANI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Kichere alimshukuru Rais kwa kuendelea kumwamini na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu mkubwa.

“Utumishi wangu ndani ya Serikali ulianzia wizara ya ujenzi, fedha na sasa naenda Tamisemi naendelea kupata uzoefu.

“Nashukuru kwa kunipa majukumu ndani ya TRA ambayo nimeyatekeleza kwa miaka miwili, nimejifunza mengi, pale tulipofikia, yeye (akimaanisha Dk. Mhede) asogee tusonge mbele,” alisema Kichere.

DK. MHEDE NA VITISHO

Kamishna wa TRA, Dk. Mhede alisema haogopi kitu chochote bali ataendelea kumtegemea Mungu katika kutimiza majukumu yake mapya.

“Jumamosi iliyopita nilipata shock ya pili baada ya ile shock ya kwanza uliponiteua kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Nimejifunza na nitaendelea kujifunza kwamba majukumu uliyonipatia kuongoza TRA si majukumu madogo, lakini nakuhakikishia siogopi kitu chochote, ninamtegemea Mungu,” alisema Dk. Mhede.