Home Makala Ya Iraq kumrejesha Bush mahakamani

Ya Iraq kumrejesha Bush mahakamani

1712
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Awali kabisa –Septemba, 2013 – Sundus Saleh, mwanamke raia wa Iraq alimburuza mahakamani aliyekuwa Rais wa Marekani George W Bush na Makamu wake Dick Cheney kwa tuhuma za kuivamia kijeshi Iraq na kuendesha vita.

Sundus alidai kwamba kuivamia nchi iliyo huru bila ya Marekani kuchokozwa ni kosa la jinai chini ya Katiba ya Marekani. Shitaka hilo pia liliwajumuisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Condoleezza Rice, Waziri wa Ulinzi Donald Rumsfeld, na Naibu wake Paul Wolfowitz.

Sundus alifungua mashitaka hayo kwa niaba yake na Wairaki wengine katika Mahakama ya Wilaya ya Kaskazini katika jimbo la California nchini Marekani.

Desemba 2014 mahakama hiyo ililitupilia mbali shauri hilo, na katika maamuzi yake ilisema kwamba wakati wanapanga na kuendesha vita ya Irak watuhumiwa walikuwa wanatenda kufuatana na mamlaka za kazi zao. Sundus hakuridhika na maamuzi hayo hivyo akakata rufaa Mahakama ya Rufaa nchini humo.

Katika rufaa yake Sundus alitoa hoja kwamba watendaji hao wa Bush walitenda hayo kutokana na misukumo ya imani zao binafsi kwamba Marekani iivamie Iraq, bila kujalisha uwepo wa uhalali katika sababu za kufanya hivyo na kwamba kimakusudi walisema uongo mbele ya umma pale walipomhusisha Saddam Hussein na  kikundi cha al-Qaeda, na pia kumiliki silaha za maangamizi.

Inder Comar, mwanasheria wa Sundus alieleza kwamba katika kesi dhidi ya wababe wa kivita wa utawala wa ki-Nazi zilizoendeshwa huko Nuremberg, Ujerumani mwaka 1946 (baada ya Vita vya Pili vya Dunia kumalizika) kinga ya ndani (domestic immunity) iliyotumiwa na watuhumiwa (maaafisa wa serikali na majenerali wa Adolf Hitler) haikuruhusiwa kuwa utetezi katika tuhuma za kupanga na kufanya uvamizi wa nchi nyingine.

Alisema: “Vyote walivyofanya Wajerumani katika vita ile vilikuwa halali chini ya sheria za nchi ile, lakini Mahakama ya Nuremberg ilikataa utetezi huo. Hivyo katika kesi hii tunaomba Mahakama ya Rufaa nayo itupilie mbali hoja ya kinga ya ndani.”

Julai 22 mwaka huu Sundus aliomba Mahakama ya Rufaa kutilia maanani, kisheria, sehemu kadha za Ripoti ya Chilcot ambayo inaeleza kwa kina yote yaliyotokea kuelekea uvamizi wa Iraq.

Alisema Mahakama inabidi itilie maanani suala lolote ambalo halina utata na ambalo linaweza likajadiliwa kutokana na uhalali wa kutokuwa wa shaka na usioweza kupingika kiurahisi. Masuala haya ni pamoja na kumbukumbu rasmi kama vile ripoti zilizotolewa na Tume ya Uchunguzi, hususan ile ya Chilcot.

Ripoti ya Chilcot ilitolewa na Kamati ya Uchunguzi ya Iraq, na ilitokana na kamati huru iliyoundwa na Serikali ya Uingereza, na ambayo ilitolewa Julai 6 2016 baada ya miaka sita ya uchunguzi, utafiti na utayarishaji wake.

Zifuatazo ni nukuu nne za Ripoti hiyo ambazo Sundus aliziwasilisha mahakamani kwa ajili ya kutiliwa maanani na mahakama hiyo ya rufaa.

Ibara 24. Mwishoni mwa 2011 Rais Bush aliamua kuja na sera ya kubadilisha utawala nchini Iraq (regime change).

Ibara 68. Tarehe 26 Februari 2002 Sir Richard Dearlove, Mkuu wa Shirika la Kijasusi (Chief of the Secret Intelligence Service) alishauri kwamba utawala wa Marekani ulifikia maamuzi kwamba sera ya uvumilivu kuhusu Iraq haiwezi kufanya kazi na kwamba ilikuwa inaandaa mpango wa uvamizi kijeshi baadaye mwaka huo, na kwamba walikuwa wanafikiria kumpa Saddam Hussein tarehe ya mwisho ya kurudi Iraq kwa wachunguzi wa silaha (za maangamizi) na tarehe hiyo iliwekwa “karibu mno kwamba Saddam asingeweza kuitimiza.”

Ibara 74: Ushauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Jack Straw wa tarehe 25 Machi 2002 ulipendekeza Uingereza na Marekani itoe ‘amri’ ya mwisho kwa Saddam Hussein kuwaruhusu tena wakaguzi wa silaha.

Na hii ililenga kuipatia Uingereza njia ya kuungana na Marekani bila ya kuikumbatia ile sera ya Marekani ya kubadilisha utawala. Kwa mtazamo wa Uingereza hii ilionyesha kwamba sera ya “kubadilisha utawala’ itakuwa siyo halali.

Ibara 89. Sir Richard Dearlove aliripoti kwamba alikuwa kishaelezwa na Marekani tayari ilikuwa imechukua uamuzi wa uvamizi – na kitu kilichobakia ni ‘kwa namna gani’ na ‘lini’ na pia alikuwa ametaarifiwa kumuwekea Saddam kiwango cha ukaguzi wa silaha kuwa cha juu sana kiasi kwamba kiongozi huyo wa Iraq asingeweza kutimiza.

Ripoti pia inajumuisha nakala za maandishi kati ya Bush na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambapo walizungumzia uvamizi wa Iraq mapema tangu Oktoba 2001.

Miezi minane kabla ya uvamizi wa Iraq, Blair alimwandikia Bush akisema: “Ntakuwa pamoja nawe, kwa vyovyote vile.” Na Julai 2002, Blair alimwambia Bush kwamba kumuondoa Saddam Hussein kutoka madarakani utakuwa ‘umelikomboa eneo hilo’ la Mashariki ya Kati ingawa Wairaki wenyewe hawataafiki suala la kuvamiwa.

Ripoti ya Chilcot ilihitimisha kwamba Saddam Hussein hakuwa tishio ilipofika Machi 20, 2003, siku ambayo Marekani na Uingereza zilianza kuivamia Iraq. Aidha ripoti ilibainisha kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa linapendelea kuendelea kwa uratibu na ukaguzi wa silaha za maangamizi.

Aidha Tume ya Chilcot ilitoa hoja za wataalamu wa masuala ya sheria ambao walisema vita ile ilikuwa haramu na ilikuwa ni uvamizi tu dhidi ya nchi huru ya Iraq.

Kwa mfano Philippe Sands alisema: “Waheshimiwa wajumbe wa masuala ya sheria nchini Uingereza pia wanasema bila kigugumizi kwamba vita ile haikuwa halali kabisa.”

Naye Sir Michael Wood alisema: “Utumiaji nguvu dhidi ya Iraq ulikiuka sheria za kimataifa kwamba haukuwa umeidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na haukuwa umeungwa mkono na sheria nyingine zozote za kimataifa.”

Kwa upande wake Elizabeth Wilmshurt aliafiki hayo na kuongeza: “Hali iliyokuwapo haikuhitaji utumiaji nguvu kiasi kile eti katika kujilinda. Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hayakuwa utumiaji nguvu za kijeshi, na hakukuwa na sababu nyingine zozote kisheria.

“Haja ya kutaka kubadilisha utawala haukuwa umetoa ruhusa ya nguvu za kijeshi. Nautazama uvamizi wa Iraq kuwa ni haramu.”

Kikundi kimoja cha wanasheria wa kimataifa akiwemo Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Marekani Ramsey Clark walitoa andishi lao la kisheria kuunga mkono kesi ya Sundus. Clark aliuambia mtandao wa Truthout wakati ule: “Katika kesi hii zaidi ya watu 3.5 milioni wamepoteza maisha yao kutokana na uvamizi haramu dhidi ya wananchi wa Iraq na kuyarudisha nyuma maendeleo yake kwa miaka mingi.

Mkataba uliounda Umoja wa Mataifa mwaka 1945 kwa lengo la ‘kuviokoa vizazi kutoka maafa yatokanayo na vita’ unakataza matumizi ya nguvu za kijeshi ila tu katika kujihami au kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hali zote hizi mbili zilikuwapo kabla ya uvamizi wa Iraq. Iraq haikuwa tishio dhidi ya nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa ilipofika tarehe 19 Machi 2003 na Baraza la Usalama la Umoja huo haukuidhinisha uvamizi.

‘Uhalifu dhidi ya amani’ umetafsiriwa katika Mkataba uliounda Mahakama ya Nuremberg kama ni “kupanga, kuandaa, kuanzisha na kuendesha vita dhidi ya nchi huru, au vita vinavyokiuka mikataba mingine ya kimataifa, makubaliano na maazimio.” Vita dhidi ya Iraq ilikuwa ni uvamizi.

Mahakama ya Nuremberg ya mwaka 1946 iliamua kwamba “kuanzisha vita dhidi ya nchi huru siyo tu ni uhalifu wa kimataifa, bali ni uhalifu mkubwa wa kimataifa kwa sababu tofauti na vitendo vingine vya kihalifu, uhalifu huu unajilimbikiza vitendo vingi viovu katika ujuma wake.”