Home Habari Ya Lugola, Simbachawene wateule wakosapo uzalendo na uweledi

Ya Lugola, Simbachawene wateule wakosapo uzalendo na uweledi

801
0
SHARE

Joseph Mihangwa

“MFUA bati na shaba au mhunzi wa chuma/hutuma nguvu si haba, ajabu ukitizama, lakini wafua fedha na wahunzi wa dhahabu ni mafundi mfawadha, kazi zao taratibu. Kadhalika kazi zao bora, watenzi wake wapole na watu wenye busara, wachache wa makelele.”(Shabaan Robert).

Utenzi huu kwenye shairi “mfua bati” katika kitabu “kielelezo cha fasili” cha Shabaan Robert, unatutahadharisha kwamba matumizi ya nguvu kubwa katika uongozi, utawala au utendaji kazi hayana tija wala ufanisi, bali kazi zilizo bora hutendwa na watu wenye uweledi, makini na walio na busara, ambao hawana makelele.

Kwenye fani ya sheria kuna tawi linaloitwa Sheria ya Utawala au kwa lugha ya kigeni “Administrative law” ambayo kimaudhui na kimantiki “Adminstrative Law” ni sehemu ya Sheria ya Katiba.

Ndani ya Sheria ya Utawala kuna vipengele kama vile “mchakato wa utawala (administrative process), kazi za Serikali (the functions of Government), Taasisi za Kiserikali (The Organs of Government), mgawanyo wa madaraka na vingine.

Wale waliopitia madarasa ya sheria wanajua jinsi ilivyo vigumu kutenganisha matawi mawili haya ya sheria hata kama ni kwa kukesha kumsoma kwa kurudia, yule mwandishi mahiri juu ya matawi hayo, de Smith, katika kitabu ambacho hakuna mwanafunzi wa sheria ambaye anaweza kusema hakukisoma “Constitutional and Administrative Law”, hivi kwamba wanasheria wengi wanaishia kufafanua kifupi tu kuwa (Administrative Law) ni “kanuni (rules) zinazotambuliwa na sheria na zenye kuhusika na kuratibu (to regulate) utawalaji (sio utawala) wa Serikali”.

Tofauti na sheria ya katiba ambayo imejikita zaidi kwenye mfumo wa Serikali na haki, wajibu wa raia na haki za binadamu; sheria ya utawala, katika utekelezaji wake lazima ijibu angalau maswali yafuatayo na kwa mtawala pia anapotekeleza majukumu yake ya Kiserikali: Je, maamuzi yanayofanyika (anayofanya) ni ya kitungaji au si ya kitungaji sheria?; ya kimahakama au si ya kimahakama?.

Je, maamuzi hayo yanahusu matumizi ya madaraka ya kisheria au utekelezaji wa wajibu? Ni aina gani ya mamlaka ya kiutawala inayofanya maamuzi? Je, mamlaka hiyo ifanye maamuzi baada ya kusikiliza au inawajibika kwa sikilizo lingine kabla ya uamuzi wa mwisho au inaweza kutoa uamuzi bila kusikiliza kabisa? Je, uamuzi huo unaweza kukatiwa rufaa au marejeo na kama ni hivyo, taasisi gani yenye mamlaka ya rufaa au usimamizi?

Haya ni maswali muhimu na ya msingi kwa watawala, wakati na wale wenye mamlaka leo, kipindi ambacho hatua za kiutawala na maamuzi yanagusa maeneo mengi ya maisha ya raia katika dunia ya utandawazi na kiu ya demokrasia na utawala bora.

Uzuri, kwa watawala, wakati maswali tajwa hapo juu yanapata majibu pia katika katiba makini za nchi, misingi ya utawala bora na utawala wa sheria inapaswa kuwa “misahafu” na kitendea kazi kwao wakati na baada ya kushika madaraka kabla ya mengine yote, kinyume chake ni kukubali kupokea madaraka kwa viapo vya gheresha na kwenda kuzurura.

Na hili ni tatizo kubwa hapa nchini leo kwa wateule wengi kuegemea propaganda za kisiasa na vyama badala ya kutawala, kama tutakavyoona hivi punde.

Kwa manufaa ya wale wasiojishughulisha kujua mipaka yao ya madaraka bali “kukimbilia madaraka” pekee kwa kujipongeza na kupongezwa kwa “kuula” bila kujali au kuelewa uzito wa madaraka yao, hapa ni ufafanuzi juu ya mfanano na tofauti pia ya matawi ya Sheria hizi mbili: Kwanza, Sheria ya Katiba haitofautiani kimsingi na Sheria ya Utawala; chimbuko lake zote ni moja na zote zinahusu kazi za Serikali na ni “Sheria za Umma”.

Tofauti pekee inayozigawa ni ile kwamba Sheria ya Katiba inajihusisha na mfumo pamoja na kazi za Serikali imetulia (at rest), wakati Sheria ya Utawala inahusika na huo mfumo na hizo kazi mbioni katika utekelezaji (in motion). Wakati Sheria ya Katiba husisitiza na kusimamia haki za mtu binafsi, Sheria ya Utawala inaweka mkazo juu ya mahitaji ya umma, namna na utaratibu wa kuyafikia na utekelezaji wake.

Wakati wa sherehe za kuapisha mawaziri na mabalozi wapya hivi karibuni Ikulu, jijini Dar es Salaam, nilivutiwa na tamko la kifasaha la mmoja wa wateule hao mbele ya Rais, Dk. John Magufuli, katika kuahidi kutekeleza majukumu yake mapya.