Home Makala YA OBAMA, MTENDA AKITENDEWA HUHISI KAONEWA

YA OBAMA, MTENDA AKITENDEWA HUHISI KAONEWA

607
0
SHARE
Rais wa Marekani Barack Obama akiteta jambo na Rais wa Urusi, Vladimiri Putin.

NA YUSUFU LULUNGU


Jirani yetu wa kijiji cha Kogelo nchini Kenya amefura. Ameapa kulipiza kisasi kwa hasimu wake Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Barack Obama ambae ni Rais wa Marekani anaemaliza muda wake, anasema kuwa Urusi ‘ilihujumu’uchaguzi wao mkuu wa mwaka huu.

Lengo likiwa ni kumwezesha Rais mteule Donald Trump wa chama cha Republican ashinde.

Kauli hizo za jirani yetu huyo zinashadidiwa na shirika lake la ujasusi wa nje (CIA). Na tayari FBI nao wameungana na CIA juu ya shutuma hizo. CIA wanasema wana ushahidi mzito kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa ndani wa taifa lao la Marekani.

Shutuma hizo kutoka kwa Obama na ndugu zake CIA zimepewa uzito mkubwa katika magazeti yao makubwa.

Pamoja na magazeti hayo kuipa uzito habari hiyo kama ilivyotolewa zaidi na CIA, hata hivyo hakuna vyanzo vya uhakika vinavyothibitisha uhusika wa Urusi katika ‘kuchakachua’ uchaguzi huo wa Marekani.

Lakini hata hivyo kama tunavyojua Taifa la Marekani ni Taifa lisilo na aibu wala kumuogopa mtu.

Hivi kama ni kweli kuna watu wa serikali ya Kremlin walihujumu uchaguzi huo. CIA wanaweza kweli wasiwataje hadharani au hata kuwakamata ili kuthibitisha madai yao hayo.

Ikizingatiwa kuwa tangu awali na mpaka sasa akina Obama hawajaridhika na ushindi wa Trump.

Kwani wanamuona ni mtu ‘asiyosomeka’ linapokuja suala la mustakabali wa taifa lao.

Kipi kilichohujumiwa?

Tangu kuanza kwa sakata hili watu wengi tunaamini kuwa shutuma hizo zinahusu uingiliaji wa mfumo wa upigaji kura na matokeo.

Kinachotajwa zaidi na Rais Obama pamoja na CIA mpaka sasa ni wizi wa baruapepe.

Wanadai kuwa Urusi iliingilia mtandao wa kamati ya Taifa ya chama cha Democratic (DNC) na mitandao mingine na kuiba baruapepe.

Baruapepe ambazo inadaiwa zilipelekwa kwenye mtandao wa Wikileaks. Kisha wiki chache kabla ya Uchaguzi, baruapepe hizo zikawekwa hadharani.

Hapo ndipo CIA na Obama wanahisi kuhujumiwa na Urusi. Kwamba kitendo cha baruapepe hizo kuwekwa hadharani siku kadhaa kabla ya uchaguzi kililenga kuchafua haiba ya Hilary Clinton na chama chake kizima.

Hatua ambayo inadaiwa ilipunguza imani ya wapigakura kwa Clinton na hatimaye wapigakura kuamua kumchagua Trump.

Kwa wenzetu hao, kitu kinachoitwa kashfa ni jambo lenye athari mbaya sana kwa mwanasiasa na kiongozi yoyote wa umma.

Kwani hupunguza nguvu na kuharibu haiba ya muhusika mbele ya umma. Na ni kitendo chenye ishara ya kuwa muhusika hana au amepoteza sifa ya kiuongozi.

Mfano ni kashfa ya Rais wa zamani wa Marekani Bill  Clinton ambae almanusura aachie                               ngazi mara baada ya kushutumiwa kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Monica Lewinsky. Binti ambae alikuja kupewa nyadhifa muhimu serikalini.

Pia kashfa nyingine ni ile ya hapo mwaka 2012 ambayo ilimkumba aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa CIA ndugu David Petraeus.

Ni kashfa iliyomuhusisha Petraeus kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa na mwandishi wake wa wasifu (biographer) Paula Broadwell.

Kashfa hiyo ilimpelekea ndugu Petraeus kujiuzulu nafasi yake hiyo. Hiyo ni mifano michache tu. Na jambo hilo ni moja ya mambo wanayoyalalamikia sana akina Obama.

Kama nilivyosema hapo juu, ni kuwa hadi sasa hawajasema au kuonesha kuwa Urusi ilihusika vipi na mfumo wa kuhesabu kura. Suala kuu ni baruapepe.

Sijaona la ajabu!

Lakini hata hivyo kama suala ni Urusi kuingilia baruapepe, hilo hata halistaajabishi. Kwani ni suala la kawaida sana katika masuala ya ujasusi. Wala hili halihitaji mjadala mpana sana.

Ni hapo tu mwaka 2013 ambapo jasusi wa zamani wa Shirika la Usalama la taifa la Marekani linalojishughulisha mawasiliano (NSA) ndugu Edward Snowden alifichua jinsi nchi hiyo ilivyokuwa inadukua mawasiliano ya nchi zingine.

Hapa tuliambiwa kuwa alidukuliwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akadukuliwa Ufaransa, Uingereza na kadhalika. Na Marekani iliomba radhi kwa kitendo chake hicho.

Kivipi Marekani itufanye tuone kuwa Urusi katenda jinai kubwa sana kwa kuingilia mawasiliano yake.

Mtenda akitendewa

Lakini tukirudi pale kwenye shutuma za Marekani kwa Urusi. Iweni kweli au niuongo, sioni kama Marekani inapaswa kulalamika sana na kuonewa huruma.

Kwani huu mtindo wa kuingilia mambo ya nchi zingine, ni yeye ndiyo kiranja mkuu. Ni Marekani kupitia shirika lake la CIA ndio waliipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Rais Salvador Allende wa Chile hapo mwaka 1973.

Na kisha kumuweka kibaraka wao JeneraliAugusto Pinochet ambae alikuja kuwa dikteta huku akiua na kutesa wananchi wake hasa wapinzani wake kisiasa.

Twende nchini Iran hapo mwaka 1953, ni CIA hao hao ndio walimpindua Rais aliyechaguliwa kidemokrasia ndugu Mohammad Mossadeqh. Kisha wakamuweka madarakani kibaraka wao ndugu Raza Shah.

Shah ambae nae alitawala kiimla na baadae kupinduliwa na kiongozi wa kiroho  Imam Ayatollah Khomeini hapo mwaka 1979.

Safari bado ni ndefu, twende nchini Panama, huko nako CIA walimpindua na kumuua Rais halali wa nchi hiyo ndugu Omar Torrijos.

Torrijos aliuawa kwa kisa cha kupinga mashirika ya ubepari kufanyakazi nchini mwake. (rejea kitabu kiitwacho Confession of an Economic hitman cha John Perking).

Haya tuache huko ni mbali sana. Twende hapo mwaka 2002 nchini Iraq. Ni Marekani hawa hawa walimpindua na kumuua Saddam Hussein. Kisha kuweka serikali yao.

Ni kupitia hizi hizi propaganda zao, wakajitokeza akina Donald Rumsfeld mbele ya ulimwengu wa kasema  Saddam Hussein alikuwa na silaha za kuangamiza umma (WMDs). Rumsfeld alikuwa ni waziri wa Ulinzi. Ila mpaka leo silaha hizo hazijaonekana.

Ndio maana hata Trump baada ya kusikia shutuma hizo dhidi ya Urusi, amesema zake kuwa “Msiwasikilize hawa watu, ndio wale wale waliosema Iraq ina silaha za maangamizi kwa umma.”

Bila kumsahau Omera Obama nae kwa mtindo wake wa Uongozi wa kuongoza kutoka nyuma (Leading from Behind). Alilitumia shirika la kujihami la nchi za Magharibi (NATO) kuingilia masuala ya ndani ya Libya.

Huko wakamuua Rais Muammar Ghaddaf. Rais ambae alikuwa ni kiongozi halali wa Libya.

Orodha ya vitendo vya Marekani kuingilia masuala ya ndani ya nchi za watu na kupindua, kuua ni ndefu sana.

Na ni jambo la kusikitisha huko kote walikofanya mapinduzi ya kijeshi na kuweka serikali zao. Hali haikuwahi kuwa imara, kiulinzi, kiuchumi na hata kisiasa. Ni majanga kwa wananchi.

Hivyo sakata hili la Urusi lina akisi ule msemo kuwa mtenda akitendewa huhisikaonewa.