Home Makala Kimataifa Ya Sudan, Algeria yanatoa somo kubwa la demokrasia

Ya Sudan, Algeria yanatoa somo kubwa la demokrasia

1775
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

Katika kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita Bara la Afrika limeshuhudia viongozi wa nchi mbili wakiondolewa madarakani kutokana na kile kilichoonekana nguvu ya umma – maandamano yasiyosita ya  wananchi wake.

Nchi hizo ni Algeria na Sudan ambazo sasa hivi waliokuwa viongozi wake wawili ving’ang’anizi wamesalimu amri na mmoja wao yuko gerezani – katika gereza lile lile alilokuwa akiwafunga wapinzani wake.

Lakini kuna kitu kipya kinajitokeza katika mageuzi haya ya utawala ambayo siyo ya kidemokrasia kwa tafsiri yoyote ile – kwamba siyo tu wananchi hao wamedai kuondoka kwa viongozi wao – bali pia waondoke na maswahiba wao ambao wametanda katika ngazi za juu za tawala zao. Kwa maneno mengine – kama msemo mmoja wa Kingereza – wanataka “kuufuta ubao kabisa” “to wipe the slate clean.

Nchini Sudan kwa mfano wananchi wamekataa kata kata kwa jeshi la nchi hiyo kutaka kutwaa madaraka wakitaja historia ya nchi yao ya viongozi wa jeshi kuwa na tabia ya “kujizaa” na wao pekee kutoa watawala.

Madai ya namna hii ya kufuta kabisa mabaki ya utawala ambao wameamua kuuondoa umejitokeza hata katika utawala wa kiraia wa Algeria ambako wananchi wanadai chama tawala cha NLF (National Liberation Front) kilichopigana vita ya ukombozi wa nchi hiyo kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa miaka ya 50 na 60, kimekuwa madarakani kwa takriban kipindi chote tangu kujikomboa.

Hivyo wananchi wameona kwamba kimeota mizizi ya mengi maovu – hususan katika utawala mbovu, ufisadi uliokithiri kutokana na kulindana, ukosefu wa ajira kwa vijana, na kutojali wananchi hususan hali zao ya kiuchumi.

Hivyo kigezo kikuu ambacho viongozi walikuwa wakikitumia kwamba chama hicho ndicho kiliwakomboa wananchi na hivyo kina uhalali wa kuchaguliwa tena na tena – kilitupiliwa mbali na wananchi hao. Kwa maneno mengine ilikuwa kauli kwamba ushindi wake kupitia sanduku la kura katiuka kila uchaguzi ulikuwa wa ghilba tu.

Hali ya namna hii pia inaweza kuwa inakinyemelea chama cha ukombozi cha Afrika ya Kusini – African National Congress (ANC) ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 25 sasa, na ambacho katika miaka ya karibuni kimekuwa na misuguano mikubwa ndani ya uongozi wake, hali ambayo ilijionyesha dhahiri miaka miwili iliyopita “kung’olewa” kwa aliyekuwa kiongozi wake Jacob Zuma na hapo hapo kuondolewa kama rais wa nchi.

Mageuzi haya yalionekana kuwa na sura ya kidemokrasia kwa sababu tu yalisukumwa na kikundi kimoja cha uongozi ndani ya chama hicho hicho. Vinginevyo jitihada zote kupitia Bungeni kwa mujibu wa katiba ya nchi zilishindikana – huenda sababu ni kwamba zilikuwa zinasukumwa na vyama vya upinzani.

Na kwa upande wa mageuzi ya kiutawala nchini Zimbabwe miaka miwili iliyopita, aliyeondolewa ni kiongozi wao aliyekuwa madarakani kwa miaka 39 – Robert Mugabe kupitia usaidizi wa jeshi la nchi hiyo.

Yaani jeshi lilitumiwa na kundi moja katika chama tawala cha ZANU-PF kumng’oa Mugabe, ambaye baadaye kulithibitishwa na Bunge. Baada ya hapo akashika Rais wa mpito (aliyewahi kuwa makamu wa Mugabe – Emerson Mnangagwa) hadi uchaguzi ulipofanyika, zoezi lilifanywa chini ya usimamizi wa utawala wa chama hichi hicho cha ZANU-PF na ambao Mnangagwa alishinda.

Hakuna kilichobadilika kwa manung’uniko ya wananchi wengi ambao wanatarajia mambo kuwa yale yale. Ukiachilia mbali kuondolewa kwa vigogo wachache waliokuwa maswahiba wa karibu wa Mugabe, safu kuu ya kiutawala wa ZANU-PF ilibaki, huku kwa mbali jeshi likiratibu yote yanayotendeka. Jeshi la Zimbabwe siku zote ndiyo limekuwa mlinzi mkuu wa utawala wa ZANU-PF.

“Mabadiliko” ya aina hii ndiyo wananchi wa Sudan (waandamanaji) wanayakataa – kwani wao wanataka vigogo wote waliokuwa na uhusiano na Bashir pamoja na maswahiba wake wa kijeshi waondoke kabisa kwenye utawala – na wawajibishwe kwa matendo yao..

Nchini Congo DRC nako mapema mwaka huu kulifganyika uchaguzi wa kumchagua rais mpya baada ya king’ang’anizi Joseph Kabila hatimaye kukubali kukaa kando. Lakini matokeo ya mabadiliko haya, ingawa kwa kiasi fulani yalionekana ni ya kidemokrasia, kiuhalisia hayajaleta mabadiliko yoyote.

Kutokana na chama chake cha UDSP kupata viti vichache Bungeni rais mpya Felix Tshishekedi hawezi kuchagua waziri mkuu, ambaye lazima atatokana na chama cha Kabila cha PPRD. Aidha magavana wa majimbo wengi zaidi waliochaguliwa ni wa chama hicho cha Kabila. Kwa hali ya namna hii ni kama vile nchi hiyo itakuwa bado inaongozwa na Kabila.

Na hapa kwetu tunajivunia hazina kubwa miongoni mwa nchi za eneo hili la Afrika, hazina ya kuachiana madaraka kwa viongozi na kuheshimu ukomo wa vipindi kwa mujibu wa katiba. 

Ni mwaka jana tu Rais John Magufuli alifanya mkutano na viongozi wakuu wa nchi wastaafu pamoja na waliokuwa maafisa wengine wa ngazi za juu kutoka mihimili yote mitatu – tukio ambalo kwa lugha yoyote ile lilikuwa la kihistoria hapa nchini kwani si tu kwamba lilionyesha utamaduni huo wa kuachiana madaraka, lakini pia kukumbukana na kuombana ushauri.

Kwani katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine viongozi hao wastaafu walitoa yao ya moyoni kuhusu uendeshaji wa nchi – baadhi yao wakitilia mkazo katika kurekebisha mambo yanayoonekana kutokwenda vizuri na kusifu mambo yanayokwenda sawa.

Hata hivyo kwa mtazamo wa haraka haraka mtu anaweza akafikiri kwamba kuachiana madaraka kwa namna hii kunaonyesha ukomavu wa demokrasia ya kweli inayofanya kazi kisawasawa na inakataza mtu mmoja kutawala milele. Kutawala milele, kama nilivyoonyesha hapo juu, kupo katika baadhi ya nchi jirani zetu na kwingineko Barani Afrika, nchi ambazo bila shaka ndiyo zinatumika kama mfano katika kuujenga mtazamo huo wa hiyo ‘hazina tunayojivunia.’

Mara kwa mara hoja inayojengwa hapa ni kwamba mtu mmoja kutawala kwa muda mrefu hatimaye huchokwa na wananchi na huishiwa mawazo ya kuendesha utawala na kuleta maendeleo.

Hata hivyo utamaduni nchini mwetu wa kuachiana madaraka hautokani na ukomavu wa demokrasia kwa sababu kinachotawala hapa ni chama kile kile kimoja kilichopo madarakani tangu uhuru zaidi ya nusu karne iliyopita – nacho kinaweza kuchokwa – yale ya Algeria –  iwapo viongozi hawataweka umuhimu wa  hawatachukua tahadhari mapema – hususan katika upanuzi wa nyanja ya siasa na demokrasia, uhuru wa kutoa mawazo na kadhalika.