Home Makala YA SUKARI YATUFUNZE KUKABILI NJAA (2)

YA SUKARI YATUFUNZE KUKABILI NJAA (2)

531
0
SHARE

Nisamehe msomaji wa Kasri la Mwanazuo kwa kuiweka pembeni mada hiyo hapo juu. Nivumilie maana bado sijamaliza kukushirikisha taarifa za simanzi. Natambua siwezi kuzimaliza maana kadri siku ziendavyo, ndivyo mapya hutokea. Mapya haya huambatana na maumivu ya mioyo. Ndio mantiki ya mjadala wangu.

Naona makosa yakirejewa. Wanaoyafanya hawataki kubaini maana ya methali hasa ile isemayo “fumbo mfumbie mjinga, mwerevu keshaling’amua.” Najua leo nitaingia kwenye mada lakini niache nipoze moyo kwanza kwa kukushirikisha fumbo la maisha na uhai wa mama Esther Makene na sasa nirejee kwa nguli katika habari na picha marehemu Mpoki Bukuku.

Mpoki alipenda konyagi yake. Aliinywa kwa umahiri mkubwa. Kila alipoimaliza alipata wasaa wa kutoa matani yaliyoambatana na kuiga sauti za watu mbalimbali. Kuna kipindi tuliwahi kuwa naye katika kazi. Ni kipindi hicho ambacho tulijenga utaratibu wa kula ‘Mkuu wa Meza’ karibu kila siku. Alikuwepo Gwandu Abraham, Denis Msacky, mzee Theofil Makunga akija mara chache chache, marehemu Danny Mwakiteleko, Angetile Hosea na wengine majina yamenikimbia.

Kila ilipofika mchana tuliondoka eneo la MCL na kwenda kutafuta chakula hicho. Mpoki akiwa wa kwanza kunitania kuwa nilitafuna nyama ile kwa hisia. Nikikumbuka nacheka sana. Nikikumbuka napatwa na wajibu wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha aliyotupa sisi na rafiki zetu waliotutangulia.

Katika vyombo vya habari Mpoki alikuwa gwiji katika masuala ya picha. Aliweza pia kuandika na mara ya mwisho nimekutana naye Arusha akiandika zama zile za Nyalandu Lazaro akihudumu Wizara ya Utalii na Maliasili. Pia nilikutana naye ‘The Guardian’ siku moja tukapiga mchapo wa muda mfupi. Kama kawaida hakuficha hisia zake pale alipokutana na mtu anayemfahamu.

Nasikitika kwa kushindwa kumuaga. Namuaga kwa namna hii na kubaki kusema tu alifanya kazi kubwa na imempatia ushindi. Alishiriki harakati nyingi ambazo zilimkomaza na kumfanya kuwa binadamu aliyejaribiwa na kushinda vita. Natambua sasa anapumzika na vita ameachia watoto na familia yake. Mimi ni nani hadi nibaki nikilia kwa uchungu kwa kuwa rafiki Mpoki kaondoka? Sina namna nyingine, ibaki kumshukuru aliyemuuumba kwa kuamua kumchukua.

Siku za mwanadamu hapa duniani ni chache sana. Hili liwe darasa kwa wale wanaodhani ni Miungu hapa duniani. Kila siku inapokatika ndipo ukaribu wa wewe kwenda kukutana na nguvu kubwa iliyokuumba zinakaribia. Je, umejiandaaje kukabiliana na nguvu hiyo siku utakapoitwa?

Ndio maana narejea katika suala la sukari. Tulilivamia bila kujipanga na likaifanya bidhaa hiyo adimu kupanda bei. Kadri muda ulivyoenda tukajikuta tunalikimbia na tumefanya hivi baada ya kuwa tumejeruhi, umiza na kuwatia jakamoyo wafanyabiashara kwa mambo ambayo yalikuwa si makosa yao. Tukawajengea taswira mbaya katika jamii kuwa wanaficha bidhaa hiyo ili ipande bei. Na mwisho naambiwa tukaamua kulikimbia jambo hili kimya kimya baada ya kubaini kuwa mapambano yale yalikuwa sawa na mbingu na nchi.

Taifa ambalo haliamini raia wake na ambalo halikimbilii kutatua matatizo ya wananchi wake, tena ambalo halifanyi hivyo kwa kutumia busara na weledi ni taifa lisilofaa kuwepo katika sura ya dunia. Matatizo ni sehemu ya maisha. Na wale wanaofatilia mambo kwa kina wanabaini kuwa hata chanzo cha uwepo wa dunia yenyewe ni matatizo. Kwa mukhtadha huo, matatizo yapo kusaidia kupunguza ombwe la maisha katika dunia.

Kwa nini sasa tuwe na mfumo wa kujiendesha usiotambua kuwa matatizo ni sehemu ya maisha na kwamba lazima kila anayeishi akabiliane nayo? Kwa nini tuwe na serikali zinazoomba kura kwa lengo la kutatua matatizo na kisha zikishapata madaraka zikimbie matatizo hayo na kuyasukuma kwa wengine? Je, kuwa mfanyabiashara wa sukari ni kosa na je, walistahili hali ile ya kuvamiwa maeneo yao wanakohifadhi sukari kabla ya kuisambaza? Je, wangeamua kuachana na biashara hiyo nini ingekuwa hatma ya nchi?

Wakati nikijiuliza kuhusu hayo tayari wimbo wa upungufu wa chakula ambao upo nchini unashika chati. Kama kawaida kila mtu anaimba beti anazotaka huku hali halisi katika maisha inaonesha kuwa tunao upungufu mkubwa na kama jitihada za kukwamua jambo hili hazitatumia busara basi nchi inaingia kubaya.

Busara ya kwanza ni kukiri kuwa lipo tatizo na busara ya pili ni kukabiliana na na tatizo kwa weledi. Tumeshuhudia matamko kutoka makundi mbalimbali  hadi viongozi wa dini. Tumeshuhudia wananchi wakisema hali ya maisha yao kuwa mbaya kufuatia kupanda kwa bei ya unga. Lakini pia wapo wanahamasisha jamii kuamini kuwa njaa inatengenezwa ili kuipa mtihani serikali. Je, kama watu wa aina hii wapo wamefanikiwaje kupanga njaa ilhali vyombo vya usalama vipo na vinatoa ripoti zake za usalama kila siku?

Je, vyombo hivyo vinasema uongo na kwamba vimefikia hatua ya kutowasilisha hali halisi ya maisha ya watanzania. Naona suala hili la chakula nalo likiingia mkondo wa sukari. Maamuzi yasiyo shirikishi yanaendelea kuliumiza taifa. Tunachelewa sana kukubaliana na hali au kuing’amua hali jambo linalotufanya kukwepesha macho pale hali halisi inavyotamalaki.

Nani atamfunga paka kengele kama tumeamua kuwa na macho yasiyoona na masikio yasiyosikia? Nani aseme sasa kama tumeamua kuwa na midomo inayonyamazisha wengine wasiseme? Kama tumeshindwa kujifunza kwa yale yaliyopita ili tufanye vema kwa haya ya sasa basi tubakie tukitambua kuwa “Majuto ni mjukuu.”

Wakatabahu.