Home kitaifa Yanayoendelea nchini yanashangaza

Yanayoendelea nchini yanashangaza

2685
0
SHARE

Spika Job NdugaiUPEPO wa kiutendaji katika mihimili miwili ya dola unavuma vibaya hali inayoashiria vyombo hivyo muhimu katika nchi kwenda kombo kama masuala ya msingi yataendelea kupelekwa kisiasa.

Dalili zinaonyesha mawimbi madogo ya maji ya upondo yameanza kuliyumbisha Bunge kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine.

Bunge liko kwenye pito zito, pito la kupambana na hoja jadidi za upinzani ambazo zinaonekana kukosa mawaa.

Hali hiyo ya upinzani kujipanga baada ya kuubaini udhaifu wa kiti na kuamua kuja na hoja nzito kila uchwao inaonyesha kulitikisa Bunge ambalo kwa kipindi kirefu linaongozwa na Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye anatajwa na baadhi ya wabunge kuwa ni mkandamizaji wa hoja zinazoigusa serikali.

Kiongozi huyu ambaye hakuna shaka yoyote ni mgeni kwenye masuala ya kibunge, anatajwa kubebeshwa mzigo mzito ambao asipopata wa kumsaidia upo uwezekano wa kumshinda na kupeleka chombo hicho mrama maana tayari upinzani wamejipanga kupiga kura ya kutokuwa na imani nae.

Bunge linaonyesha dalili za kudhoofisha jitihada za makusudi za Rais John Magufuli za kutaka haki na usawa kwa wote.

Hapana shaka yoyote idadi kubwa ya Watanzania wanayo imani ya dhati na Rais Magufuli, ukweli ni kwamba Rais huyu ameonyesha kuguswa na matatizo yanayowakabili wananchi ambao mahala pekee pa kufikisha changamoto zao ni bungeni kupitia wabunge waliowachagua.

Nafikiri Rais hapendi kuuona uonevu, hapendi kuona dawa zikikosekana kwenye hospitali zote nchini, hafurahishwi na hatua ya kukosekana kwa madawati, vifaa vya kufundishia na nyumba bora za waalimu.

Bila shaka anaona haya kupishana barabarani na Watanzania waliochoka na kudhoofika kwa njaa, huku wakiwa hawana uhakika wa malazi na mavazi yao. Ama kwa hakika huyu ni Rais wa watu.

Kwa bahati isiyo mbaya wala nzuri, jitihada na juhudi za Rais zinaonekana kukwama na zinakwama kwa sababu zinakwamishwa na wajanja wachache ambao wanazifurahia maiti za kila siku za wajawazito na watoto.

Wajanja hao wanapata amani ya moyo kushuhudia idadi kubwa ya watoto wa walala hoi wakikalia vumbi kwenye shule za serikali huku watoto wao wakikalia madawati yenye kufanana na viti vya baba zao ofisini.

Wajanja wanafurahia watoto wa wavuja jasho kutimuliwa vyuoni ndani ya saa 24, huku wakijua wazi si jambo rahisi kuwatimua watoto zaidi ya 7000 ndani ya saa 24 na wote wakafanikiwa kuondoka kwa wakati huo.

Inawezekana kuwatimua si kosa, lakini je, msingi wa watoto hao kuwapo hapo walipotimuliwa ni upi?

Sakata hilo la wanafunzi na wahadhiri wao wa Chuo Kiku cha Dodoma (UDOM) inaonekana dhahiri limegubikwa na mtazamo wa kisiasa, wapo wanaodhani maamuzi yao hayo yatawafikisha mbali kimamlaka na wapo wanaotamani kulitumia sakata hilo kujiongezea umaarufu kisiasa.

Makundi yote haya yanaendesha siasa za maji taka kwenye jambo hilo, hatua mbayo ikiendelea kupewa nafasi inaweza kuliteketeza Taifa, kinachoendelea kwenye suala hili ni utamaduni ule ule wa wakubwa wachache kuwashauri vibaya wakubwa wenzao na wakati mwingine kufikiia hatua ya kuwadanganya.

Hebu tujiulize, hawa vijana waliofukuzwa chuoni hapo walijipeleka wenyewe au walipelekwa hapo baada ya matokeo yao ya kidato cha nne kuwabeba kwa (alama A na B) kwenye masomo ya sayansi?

Hatua hiyo ilifikiwa na serikali ya awamu ya nne, ambayo Rais wake wakati huo Jakaya Kikwete aliitaka wizara ya elimu kufanya jitihada za dharula za kupunguza kama si kulimaliza kabisa tatizo la walimu wa sayansi katika shule za sekondari za serikali.

Hapo ndipo mpango huo ulipoanza na wahusika walipata nafasi kulingana na vigezo vilivyowekwa, haraka ikaanzishwa stashahada maalumu ambayo iliyozinduliwa na Rais kwa fedha zilizoombwa bungeni kisheria na Bunge likaridhia.

Wahusika wote waliokuwa na sifa wakapewa dhamana na serikali ili wakimaliza mafunzo yao hayo wakalisaidie Taifa kwenye Nyanja ya elimu hasa kwenye masomo ya sayansi na huko mbele ya safari wakasome shahada ili kuwaongezea weledi zaidi, kwa maana nyingine dhamira ya kuwapa nafasi ya kusoma stashahada ilikuwa ni kuwajengea uwezo.

Serikali chini ya TCU, ikafanya kazi ya kuwadahili na kuwapa ruhusa ya kuingia chuoni, ni ajabu leo hii serikali ya awamu ya tano kwa misingi ile ile ya kudanganywa imeamua kuwadhalilisha vijana wale, pamoja na Rais mstaafu ambaye kwa nia njema aliamua kulisaidia Taifa.

Ni ngumu kukubaliana na kinachotokea, ukweli kinashangaza, inawezekanaje serikali ya watu walewale na Bunge lile lile leo hii linawaona wale vijana ni kama wahaini wasiopaswa kuendelea kuwapo chuono hapo. Ajabu sana.

Nimelijadili suala hili kwa kisana kwa sababu ya uzito wake, hasa ukizingatia wanaopata tabu hii ni watoto wa wananchi wa kawaida ambao waliamini vijana wao wako kwenye mikono salama.

Bahati mbaya katika hali ya kushangaza wamekutwa nay a kuwakuta, jambo la kupendeza ni uwezo na mbinu za wajanja hawa wachache, ambao wanawalazimisha wananchi waichukie serikali.

Kwa makusudi hawatumii weledi na busara zao kuishauri serikali kuwatendea yaliyo mema wananchi wake, badala yake wanafanya madudu ambayo yanawafurahisha wao nna kwa kauli za kejeli wanasema wameshaamua na hakuna wa kubadili maamuzi yao!

Katika kuonyesha matendo yao maovu ya kuendelea kuifarakanisha serikali na wananchi, wameshauri vikao vya Bunge kutorushwa ‘live’.

Hapa ndipo maswali na hoja za serikali kutotaka kukosolewa zilipoanza, kila mwenye kusikia amesikia na mwenye kuona ameona, wakubwa wamekataa kuwapa haki ya msingi wananchi wao kwa hoja kuu ya kukosekana kwa fungu la kurusha matangazo hayo.

Inawezekana hoja hiyo ikawa na mashiko, lakini nachelea kuibariki kwa sababu walijitokeza wahisani waliokuwa na utayari wa kulkipia matangazo hayo ili wananchi waendelee kupata taarifa za mwenendo wa vikao vya Bunge.

Kwa makusudi wakubwa wakaendelea kugoma na badala yake kuibuka na mfumo wao wa kuonyesha shughuli za Bunge kwa muda wanaotaka wao.

Ni kweli serikali ya awamu ya tano haiku tayari kukosolewa hadharani? Kwanini wameamua kuyafungia ndani yanayotokea bungeni  huku wakijua wazi walengwa na wahusika wakuu wa vikao hivyo ni wananchi? Napata ukakasi hapa.

Hilo likiwa halijaisha tayari limeibuka jingine jipya na la hatari zaidi, ambalo linafungua milango ya kuwaaminisha wananchi wengi kuwa Bunge la 11 ni maalumu kwa ajili ya kuitetea na kuilinda serikali na yeyote atakayeikosoa atashughulikiwa. Fikra zangu.

Kwa kudhibitisha hilo, tayari Bunge limewasimamisha wabunge kadhaa wa upinzani ambao waliamua kuipigania jamii ya Watazania ili kupata habari kutoka bungeni.

Hapa tunajifunza nini, kwamba ni kweli serikali haiutaki kukosolewa au Bunge halipendi kusikiliza hoja mujarabu za upinzani?

Ni fikra zangu tu.