Home Latest News YANGA NA HADITHI YA MTUMAI CHA NDUGU…

YANGA NA HADITHI YA MTUMAI CHA NDUGU…

2220
0
SHARE

NA ASHA MUHAJI,

NI aibu tena ya karne kwa klabu kubwa, kongwe, maarufu na yenye rasilimali watu ya kutosha kama Yanga kulia njaa katika zama za sasa za soka linaloendeshwa kisayansi.

Toka mwaka 1935 waasisi wa klabu hiyo walifanya kazi kubwa sana ya kuwekeza kwa kutafuta mtaji wa wanachama na mashabiki ambao kwa kiasi kikubwa sana wamefanikiwa kwani klabu hiyo inadiriwa kuwa na mashabiki wasiopungua Mil 15 nchi nzima.

Hali kama hiyo ya mtaji wa mashabiki ipo pia upande wa pili kwa pacha wake, yaani klabu ya Simba ambayo nayo ina mtaji mkubwa sana wa wanachama.

Hakika hakuna cha kujivunia katika klabu hizo kubwa mbili na kongwe kama mtaji wa mashabiki. Mengi wamefanikiwa kupitia hilo lakini pia wameshindwa kutumia nafasi hiyo vilevile kufanikisha mengi ya kimaendeleo.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na hali ya mbaya ya kiuchumi ndani ya klabu ya Yanga. Hali ambayo hivi sasa inatishia hata ushiriki wa mafanikio ndani ya klabu hiyo kuelekea tamati ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwemo ile michuano ya kimataifa ambapo inashiriki Ligi ya mabingwa barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa aliweka wazi hali hiyo hivi karibuni akidai kuwa inatokana na mgogoro alionao mwenyekiti wao na serikali.

Katika uhalisia wa sasa wa uedeshaji wa klabu hiyo kwa lugha nyepesi unaweza kusema inaendeshwa na jeshi la mtu mmoja. Ndiyo ni jeshi la mtu mmoja kwani mzigo mzima wa uendeshaji timu unamkabili mtu mmoja tu huku wengine wakiwa hawajui hata ufanisi huo unatokana na nguvu ya fedha kutoka wapi.

Jeuri ya fedha ya mtu mmoja iliwafanya mashabiki kujisahau na kushindwa kuthubutu hata kuhoji matumizi makubwa ndani ya klabu ilihali wakijua fika klabu yao haikuwa na uwezo wa mapato yanayokaribiana na matumizi yao.

Pengine ushabiki wa kisoka baina yao na watani zao wa jadi Simba ikiwemo klabu tajiri hapa nchini ya Azam ilisababisha klabu hiyo kujipandisha thamani bila ya kuwa na tathimini halisi  hivyo kuzua mihemko ya kishabiki ambayo mbali ya kuwa na burudani miongoni mwa klabu hizo lakini pia ilizidisha tambo kati yao.

Wakati viongozi wanapandisha matumizi mashabiki na wanachama wengi wanafurahia kwa kuona wanasaidiwa mzigo wa majukumu lakini wakasahau kuwa hilo lina faida na hasara  zake vilevile.

Usajili wa timu kwa maana ya gharama zote anayehusika kujua zitatoka wapi na hata kulipa ni mtu huyo huyo. Kulipa mishahara ya wachezaji, makocha na watendaji wengine wa klabu, gharama za kambi, usafiri na zingine zote za uendeshaji wa timu zinamuhusu mtu huyo huyo.

Msingi mkubwa wa mapato ya klabu nyingi hapa nchini ni kutokana na vyanzo vya mapato ya milangoni kwa klabu kubwa kama Yanga na Simba hazizidi Milioni 400 kwa msimu fedha ambazo hazitoshi hata matumizi ya miezi sita tu kulipa mishahara ya wachezaji na makocha.

Mhasibu anapewa maelekezo ya kulipa baadhi ya gharama lakini hajui hela zinatoka wapi hali kadhalika wakati mwingine hata katibu wa klabu naye hajui ila ana uhakika wa malipo kufanyika.

Athari zinazoonekana kwa sasa kuanzia na Yanga ni kuelekea kuyumba kwa klabu hiyo kwa sababu tu mhimili mkuu wa uendeshaji wa klabu katika masuala ya kifedha yuko katika matatizo.

Wachezaji wa kigeni wakiwemo wazawa wameanza kulalamika kuhusiana na malipo ya mishahara yao. Vicent Bossou raia kutoka …. ameweka wazi kukerwa kutokana na kutopata stahiki yake hiyo. Lakini inadaiwa mishahara ya mchezaji huyo imetumika kwa matumizi mengine ya timu.

Timu ilishindwa kuweka kambi bora kama ilivyozoeleka wakati ikijiandaa na mtani wake yote hiyo ikitokana na athari hizo hizo za kumtegemea mtu mmoja na kusahau kuibebesha klabu mzigo halisi.

Katika mazingira ya sasa hilo ni tatizo kubwa kwa kuwa tayari  athari zimeanza kuonekana ambapo morali imepungua sana ndani ya timu wakati timu ikiwa katika vita ya kuwania kutetea taji lake.

Yanga inatarajiwa kupambana na Zanaco ya Zambia baadaye mwezi huu ikiwa mechi ya pili ya kuwania kufuzu kucheza makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo bila kurekebisha tatizo hilo inaweza kuathiri ushiriki wake.

Ni aibu kwa klabu kubwa kama hiyo kushindwa kujitegemea na badala yake kutegemea fedha za mtu kutoka mfukoni mwake. Nani ndani ya Yanga anayejua fedha zinazotumika zinatoka wapi?

Bila shaka sasa wanachama wa klabu hiyo watajiuliza mara mbili mbili au zaidi ili kupata akili na hata kufanya maamuzi sahihi sasa juu ya mfumo upi unapaswa kutumiwa na klabu yao.

Katika suala hili si Yanga tu bali hata pacha wake Simba kwani nayo inaendeshwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu tu kutegemeana na wahisani.

Kilio wanacholia Yanga hivi sasa ndicho kinachoinyemelea Simba siku zijazo kwani nayo inategemea sana fedha kutoka kwa Mfanyabiashara Bilionea kijana, Mohammed Dewji (MO).

Wanachama warejee tena kuangalia namna bora ya kuziendesha klabu zao bila kuangalia mchango wa mtu binafsi. Wafanye maamuzi sahihi japokuwa wameshachelewa lakini ukweli utabaki kuwa ni heri kuchelewa kuliko kukosa kabisa.

Laiti kama wanachama wote kwa kauli moja wangekubaliana na kupitisha mfumo mpya wa uendeshaji klabu yao kibiashara yanayotokea sasa yasingeiathiri klabu hiyo kwa kuwa ingeendelea kupata fedha kupitia mkataba.

Hapa kuna funzo kubwa kutokana na ukweli kuwa walipatikana baadhi ya wanachama waliopinga mabadiliko hayo na hata kushitaki serikalini pale mmoja wa viongozi wa sasa wa klabu hiyo alipotaka kukopeshwa kwa miaka 10 kwa masharti kadhaa.

Faida ya mfumo wa uendeshaji kibiashara ni kuwa hata pale mmiliki wa kampuni anapofariki bado kampuni itaendelea kuilipa klabu bila kuangalia changamoto zitakazojitokeza.

Lakini funzo kubwa ni pale viongozi wa hizi klabu wanapojiamulia kupandisha thamani ya kimatumizi bila ya kuangalia vyanzo halisi vya mapato vya klabu husika.

Hakuna sababu ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kama huna uwezo wa kukizalisha. Hakuna namna njia sahihi ya kutatua tatizo hilo ni kwa kubadili mfumo wa uendeshaji klabu ili klabu ijipatie mapato yake yenyewe kulingana na vyanzo vyake vya mapato vitakavyokuwa wazi badala ya hisani za watu tu.

Ndoto kufikia mafanikio waliyonayo klabu zilizopiga hatua kwa kutegemea wahisani.