Home Burudani Zaiid afunguka alivyopokea urithi kutoka kwa Zavara

Zaiid afunguka alivyopokea urithi kutoka kwa Zavara

865
0
SHARE

NA JEREMIA ERNEST

MAJI hufuata mkondo ndivyo unavyeweza kusema ukifuatilia historia ya rapa Abdullah Mnete maarufu kama Zaiid, aliyerithi kufanya muziki kutoka kwa mjomba wake  Ramson Zavara, miongoni mwa waasisi wa Bongo Fleva kupitia kundi la Kwanza Unit lililowika miaka ya 1992.

Kama hiyo haitoshi, Zaiid aliyefanya vizuri mwaka juzi na wimbo Wowowo, amefuata nyanyo za kaka yake Sudi Mnete ambaye alikuwa mwanamuziki kabla ya kutimkia Ujerumani kuwa mtangazaji wa kituo cha habari, Deutsche Welle.

Katika mahojiano aliyofanya na RAI, Zaiid anasema alianza kuimba kwa kuchana mistari wakati akiwa shuleni kwa siri siri, bila kumshirikisha mtu kwa sababu mjomba wake (Zavara) alikuwa mtu anawaelewa wasanii ambao wamejikita zaidia katika masomo.

Anasema siku moja aliamua kuvunja ukimya na kumwambia mjomba wake juu ya mapenzi yake kwenye muziki na kwa bahati nzuri, Zavara ilikuwa upande wake, akampa ahadi ya kumsaidia zaidi kwa kumletea vitabu na maandiko mbalimbali yanayohusu muziki wa Hip hop ili asome na kuongeza maarufa zaidi.

“Nilisoma na kusikiliza baadhi ya kanda za wasanii wa mwanzo wa Hip hop.  Nilielewa na kuzidi kupenda muziki huu. Nilitumia muda wa mwaka mmoja kuuelewa kiundani na kuanza kufanyia kazi kile nilichojifunza,” anasema Zaiid.

Anaongeza kuwa baada ya kumaliza kujifunza alianza kufanya mazoezi wakati huo, mjomba wake akiagiza vifaa vya studio kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kufungua studio ya nyumbani.

“Vifaa vilifika na nikaachiwa nafasi ya kuvifunga nikisaidiana na mtaalamu wa masuala ya sauti,” anasema.

Zaiid anasema, katika muda ambao walikuwa wakiutumia kufunga vifaa hivyo, aliutumia kurudia (kuchana) baadhi ya mistari aliyoiandika na ndipo mjomba wake alipogundua kuwa yupo vizuri kwenye michano ya Hip hop.

AANZA MUZIKI RASMI

Zaiid, alipata umaarufu na mashabiki wengi baada ya kutoa  wimbo ya Who Dat, uliokuwa unapatikana katika kanda zake mseto (Mix tapes) za Kanda Mbovu, Kwanini na Mistari Yako.

Asilimia kubwa ya nyimbo zilizokuwamo katika kanda hizo mseto zilikuwa zinatumia midundo ya nyimbo za Hip hop za wasanii wa Marekani.

Licha ya ‘Mix tapes’ hizo kufanya vizuri, hakuweza kueleweka haraka katika jamii kutokana na nyimbo nyingi zilikuwa za kuelimisha kutokana na elimu aliyoipata kutoka kwa mjomba wake.

“Niliamua kuacha muziki wa kuelimisha na kuhamia katika ngoma za kuburudisha na kutoa ile traki yangu ya Kimbaumbau, kisha nikaachia wimbo wa Wowowo ambao ulinipatia umaarufu zaidi,” anasema Zaiid.

Baada ya kutoa Wowowo, iliyompa mafanikio ya kupiga shoo karibia nchi nzima, alimua kurudi darasani ili kumalizia masomo yake ya chuo ambako sasa amebakiza muda mchache ili ahitimu ngazi ya Astashahada katika Chuo Huria cha Dar es Salaam.

Zaiid, ambaye ni Mndengereko, alizaliwa hospitali ya Misheni Kigamboni na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Lugalo na sekondari shule ya  Ardhi, Dar es Salaam.

Anasema muziki umempatia faida ya fedha za kujikimu katika mambo mbalimbali ukizingatia kwa sasa ajira yake kubwa ni muziki.

Mbali na muziki anafanya biashara ndogo ndogo akiwa bado hajapata biashara kubwa ambayo anaweza kuiweka hadharani watu wakaifahamu.

Zaiid ni baba wa mtoto mmoja ila hadi sasa hajafanikiwa kuoa na bado hajawa na matarajio hayo hadi mipango yake itakapokamilika.

Anasema hivi karibuni ameachia ngoma mpya aliyoipa jina la ‘Tuserebuke’ ambao ameshirikiana na Papii Kocha, huku lengo lake likiwa ni kuendelea kuachia nyimbo mfululizo ili kukata kiu ya mashabiki.