Home Latest News ZAMBIA: MAJAJI WA KENYA WAMTIKISA RAIS LUNGU

ZAMBIA: MAJAJI WA KENYA WAMTIKISA RAIS LUNGU

858
0
SHARE

LUSAKA, ZAMBIA

Uamuzi wa Septemba 1 wa Majaji wa Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya Kenya kubatilisha matokeo ya nuchaguzi wa nchi hiyo yaiyompa ushindi Uhuru Kenyatta dhidi ya mgombea wa Upinzani Raila Odinga umepeleka mtikiso nchini Zambia.

Rais wa nchi hiyo Edgar Lungu amewatahadharisha majaji nchini humo kwamba kunaweza kuibuka ghasia kubwa nchini humo iwapo nao watathubutu kumzuia kuwania katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2021.

Rais Lungu aliingia madarakani baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Michael Sata aliyefariki Oktoba 28 2014. Sata, aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza 2011, ilikuwa amalize kipindi chake cha kwanza cha urais mwaka jana 2016.

Katiba ya nchi hiyo inahitaji uchaguzi mdogo wa urais ufanyike kumpata rais wa kumalizia kipindi cha Sata. Uchaguzi huo ulifanyika Januari 20 2015 na Lungu alimshinda mpinzani wake Hakainde Hichilema kwa tofauti ya kura 27,757 tu (asilimia 1.66).

Kwa mara ya pili Lungu alimshinda Hichilema katika uchaguzi wa urais wa mwaka jana 2016 na tayari kumeibuka mjadala kuhusu iwapo Lungu ana haki kuwania au la kugombea uchaguzi ujao wa 2021 huku wakosoaji wake wanasema kwamba sasa hivi anahudumu muhula wa pili na hivyo hawezi kuwania tena.

Wanasema kipindi ambacho alihudumu baada ya kifo cha Rais Michael Sata mwaka 2014 kinatakiwa kuhesabiwa kama muhula wa kwanza.

Wafuasi wa Lungu wanasisitiza kwamba alikuwa anamalizia tu muhula wa mtangulizi wake na kwamba muhula wake wa kwanza ulianza aliposhinda uchaguzi wa mwaka jana 2016, ambao nao ulikumbwa na utata.

Mgogoro huu wa kikatiba iwapo Lungu ana haki au la ya kugombea urais kipindi kingine katika uchaguzi ujao wa 2021, unatakiwa kuamuliwa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.

Bila shaka kwa hofu ya kutoa hukumu hasi kwake Lungu alisema Majaji wa Mahakama ya nchi yake hawafai kuwaiga wale wa Kenya ambao alidai waliitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 ambapo Rais Kenyatta alikuwa ametangazwa kuwa mshindi.

Wiki iliyopita Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Alhamisi wiki iliyopita baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kususia.

Akiwahutubia wafuasi wake kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Bw Lungu lisema wenzake katika idara ya mahakama, ujumbe wangu wake ni kwamba wafanye kazi yao, wafasiri sheria bila woga au kupendelea upande wowote kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Aliongeza; “Msiwe watu wa kuiga na mfikirie kwamba mtakuwa mashujaa iwapo mtatumbukiza nchi hii kwenye vurugu,” na kwamba wale watu ambao hawapendi amani na uhuru watasema kwamba Rais Lungu anatoa vitisho kwa mahakama za kisheria.

Alidai kwamba yeye hatoi vitisho kwa mahakama ila  alikuwa anawatahadharisha tu kwa sababu “kuna habari kwamba baadhi yenu huenda mkapenda kujaribu mambo. Majaribio hayo yenu yasituingize kwenye fujo, tafadhali.”

Baadhi ya wananchi wa Zambia wamekuwa wakisema kwamba mahakama za nchi hiyo zinafaa kufuata mfano wa mahakama za Kenya, kwamba zinapaswa kuwa na ujasiri na kufanya maamuzi ambayo yanazingatia maslahi ya raia.

Alizionya mahakama za Zambia kutochukua hatua “kana kwamba majaji hao si sehemu ya bara letu la Afrika.”

Aidha alisema jambo muhimu ni kwamba mwaka 2021, atakuwapo na atawania kugombea urais iwapo chama changu kitanichagua.”

Mahakama ya Juu nchini Kenya ilisifiwa sana kwa kufanya uamuzi wa ‘kijasiri’ kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Majaji wanne wa mahakama hiyo waliunga mkono uamuzi huo ingawa wawili waliupinga.

Siku moja kabla ya uchaguzi wa marudio hata hivyo, mahakama hiyo ya juu ilishindwa kusikiliza kesi ambayo ilihusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya kukosekana kwa majaji wa kutosha mahakamani.

Ni Jaji Mkuu David Maraga na Jaji Isaac Lenaola pekee waliofika kortini.

Kikao cha mahakama hiyo huhitajika kuwa na angalau majaji watano kwa mujibu wa Katiba.