Home Makala ZAO LA KOROSHO PASUA KICHWA?

ZAO LA KOROSHO PASUA KICHWA?

4675
0
SHARE

NA MUDHIHIR MUDHIHIR


KATIKA mkutano wa Bunge la Bajeti uliyomalizika hivi karibuni tulishuhudia mjadala mzito kuhusu fedha za ushuru wa korosho ghafi zinazosafirishwa nje ya nchi. Sikusudii hapa kuwatambua waheshimiwa wabunge waliyokuwa wanazungumza kwa sababu ya kushughulika moyoni au kwa sababu ya mshawasha wa maslahi ya kisiasa.

Kwa ujumla makala hii haina chembe ya mwelekeo wa kuyarejea yaliyojitokeza bungeni chambilecho Waswahili, ya nini kuyadhukuru na yakishapita huwa hayadhuru? Wala makala hii hailengi katika kutaka kujua fedha hizi za ushuru wa korosho ni mali ya nani na zimilikiwe na nani. Unajua  jambo  jema likishughulikiwa kwa namna isiyofaa huleta madhara! Tusigombee fito na hali nyumba tuijengayo ni moja.

Ikiwa tunatamani kuamini kuwa zao la korosho ni pasua kichwa basi ni vyema serikali na wadau wa korosho tukalitazama tatizo la msingi linaloleta taharuki ndani ya tasnia ya korosho, badala ya kuhangaika na fedha za ushuru. Tukumbuke kwamba kulitambua tatizo kunahitaji umakinifu (critical thinking) na kulitatua tatizo kunahitaji ubunifu (creative thinking). Umakinifu na ubunifu hulet uyakinifu.

Matatizo yanayoatili au kuhafifisha ustawi wa tasnia ya korosho hapa Tanzania yanaogelea ndani ya kasoro za uendeshaji wa tasnia yenyewe ya korosho, uendelezaji wa zao hili na soko lake. Mambo haya matatu ndiyo harabu yanayoharibu ustawi wa tasnia ya korosho nchini mwetu. Matatizo haya yanatatulika kwani kila kufuli na ufunguo wake. Vishindo vya kisiasa na ukali wa kiutawala vinahitaji umakinifu na ubunifu.

Kimsingi tasnia ya korosho hapa Tanzania huendeshwa na utatu wa serikali, wakulima wa korosho na wabanguaji. Serikali katika utatu huu inawakilishwa na Bodi ya Korosho ambayo ipo kisheria katika kuundwa kwake na katika majukumu yake ndani ya tasnia. Wizara ya Kilimo na Ushirika huwakilishwa katika Bodi ya Wakurugenzi na Afisa wake wa ngazi za juu.

Kundi la pili katika uendeshaji wa tasnia ni wakulima wa korosho kupitia vyama vya ushirika (AMCOS) na vyama vikuu vya shirika ambavyo ni Mwambao na Runali (Lindi), TANECU na MAMCU (Mtwara), TAMCU (Tunduru) na CORECU (Pwani). Ushirika una wajibu mkubwa wa kuwaunganisha wakulima na kuhakikisha kuwa wanakuwa na sauti moja na uamuzi wenye tija kwao.

Kundi la tatu katika kuiendesha tasnia ya korosho ni umoja wa wabanguaji. Matarajio ya serikali kutoka katika kundi hili ni kuhafifisha mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi na kuongeza kasi ya ubanguaji hapa nchini. Hatua hii ililenga kuongeza thamani ya korosho sokoni, kutengeneza ajira nchini, na kunufaika na mabaki yanayotokana na uchakataji kama vile kemikali za korosho na kadhalika.

Kasoro ya pili inayohitaji kufanyiwa kazi imo ndani ya mbinu na mikakati ya kuliendeleza zao la korosho. Maeneo yanayohitaji kupewa uzito ni utafiti ili kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya korosho, kutumika kwa matunda yake kibiashara kama vile vinywaji na siagi, na udhibiti wa magonjwa ya mikorosho. Eneo jingine ni elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kukiendesha kilimo cha korosho.

Kasoro ya tatu kubwa na yenye kuleta taharuki ni soko la korosho. Maeneo yanayohitaji kutazamwa na kupatiwa suluhu ni kuyumba kwa bei ndani na nje ya nchi, elimu na ufahamu miongoni mwa watendaji na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu (Unions). Wakulima nao wanahitaji maarifa ya namna ya kupata korosho safi kabla ya kuzifikisha sokoni.

Matatizo makubwa ndani ya tasnia ya korosho hujitokeza wakati wa msimu, yaani soko. Katika kipindi hiki cha mauzo na ununuzi wa korosho, wanunuzi wa korosho hutembea na nyavu za jarife zinazowanasa samaki wakubwa, na nyavu za kokoro zinazowanasa samaki wadogo. Hiki ndicho kipindi zinaposikika ngurumo za wenye mamlaka na shinikizo za wanasiasa. Ni kipindi ambacho jasho la mkulima lenye chumvi hunywewa kama juisi yenye sukari.

Ili kuikabili vururu vururu ndani ya soko la korosho ghafi serikali ikatunga  sheria ya kutoza ushuru wa kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi. Matarajio yalikuwa kuhamasisha ubanguaji ndani ya nchi. Lakini wanunuzi wa korosho ghafi hawaumizwi na ushuru huu kwa kupata nafuu ya ruzuku huko wanakozipeleka. Huko hawako tayari kupoteza ajira ya watu wao na kodi kwa serikali.

Kumbe tufanyeje basi ili tujinasue na matatizo yaliyomo ndani ya tasnia ya korosho? Kwa upande wa uendeshaji serikali haina budi kuratibu  namna bora ya mahusiano na mwingiliano baina ya wadau mbalimbali wa korosho. Hatua za makusudi zichukuliwe ili kuleta ujuzi na maarifa miongoni mwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika. Na ziwepo programu za kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima namna bora ya kuendeleza zao la korosho.

Kasoro zilizomo katika uendelezaji wa zao la korosho zinaweza zikadhibitiwa kwa mosi, kuwa na programu nzuri na sahihi ya utafiti. Pili, kuwepo na mpango na utaratibu unaozingatia majira ya kupatikana na kusambaza viuatilifu vya kukinga na kutibu magonjwa ya mikorosho kwa gharama nafuu. Na tatu tuweke utaratibu wa kutoa elimu na usimamizi kwa wakulima juu ya namna na wakati wakutumia viuatilifu.

Na kasoro zilizopo katika soko la korosho zitaondoshwa kwa mafanikio makubwa iwapo serikali itaweka mkazo katika kuuza nje ya nchi korosho zilizobanguliwa badala ya ya kuuza korosho ghafi. Uamuzi huu utaanzisha vita vikali baina yetu na nchi inayonunua korosho zetu ghafi. Tutakuwa tumewasababishia ukosefu wa ajira nchini mwao na nakisi katika mauzo ndani ya masoko ya Ulaya. Lakini lisilobudi hutendwa.

Ubanguaji wa korosho unawezekana iwapo juhudi zitaelekezwa katika ubanguaji miongoni mwa wakulima wenyewe. Viwanda  viwili vikubwa vinatosha kwa kuanzia kumalizia hatua za vifungashio na nembo. Ndivyo inavyofanyika nchini India na Vietnam. Hatuhitaji fedha nyingi kuwawezesha wakulima kuanzisha viwanda vidogo vya kubangua korosho. SIDO wanaweza kutoa mchango mkubwa katika suala hili.

Badala ya kuvutana juu ya fedha za ushuru wa korosho zimilikiwe na nani, rai yangu ni kuwaomba wahusika ndani ya serikali kuweka utaratibu na namna ya fedha hizo zitakavyowezesha utafiti, ubanguaji mdogo miongoni mwa wakulima, na upatikanaji wa pembejeo. Ng’ombe anayelishwa vizuri hutoa maziwa mengi na bora.