Home Latest News ZIARA YA DONALD TRUMP ASIA: MIAKA 46 TANGU SAFARI YA SIRI...

ZIARA YA DONALD TRUMP ASIA: MIAKA 46 TANGU SAFARI YA SIRI YA HENRY KISSINGER CHINA MWAKA 1971

1297
0
SHARE

NA ABBAS ABDUL MWALIMU

Ni miaka 46 sasa imepita tangu aliyewahi kuwa Msaidizi wa Rais wa 37 wa Marekani, Rais Richard Nixon na Mshauri wake wa Masuala ya Usalama kuanzia mwaka 1969 mpaka 1975 Bwana Henry Kissinger alipofanya safari ya siri nchini China mwaka 1971.

Henry Kissinger pia alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuanzia mwaka 1973 mpaka 1977.

Henry Kissinger ni Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa wa ngazi ya juu alifanya uchunguzi wa kitaalamu ambao ulimpa taswira ya China ya miaka 50 baadaye. Miaka hiyo ndiyo hii tuliyo nayo sasa.

Katika uchunguzi wake Henry Kissinger aliitazama China kwa Ukubwa wake (Size of Territory), idadi ya watu (Population), Uwepo wa Bahari inayoizunguka China, Mapinduzi ya kiuchumi yaliyokuwa yakifanyika wakati ule, falsafa ya viongozi wa kizazi kile sambamba na utamaduni wa kichina.

Mipaka (Territory) kwa mujibu wa maelezo ya Bwana Henry Kissinger katika kitabu chake cha “On China” cha mwaka 2011 sambamba na kile cha “White House Years” alieleza kuwa nchi kama China ambazo zina eneo kubwa la mipaka (territory) zinaweza kuja kuibuka kuwa nchi tajiri zenye nguvu ya kiuchumi, kijeshi na ushawishi katika siasa za kimataifa. Alizigusia pia nchi za Brazili, Urusi, India na Afrika ya Kusini (BRICS).

Idadi ya watu (Population), kwa mujibu wa Kissinger nchi zenye idadi kubwa ya watu kama ilivyo China na India zina nafasi ya kunyanyuka na kuwa mihimili ya kiuchumi na kiusalama duniani.

Uwepo wa bandari, mapinduzi ya kiuchumi yaliyofaywa na Mao na Deng Xiaoping sambamba na falsafa zao kama vile mawazo ya Mwenyekiti Mao na dhana ya kiuchumi ya Deng Xiaoping “Deng Xiaoping Economic Theory”  vilitoa mwelekeo wa China ya miaka 50 baadae ambayo ndiyo hii China ya sasa.

Utamaduni ni nyenzo nzuri sana ya kuhakikisha nchi inafikia azma ya kiuchumi na kama itatumiwa vizuri.

China imekuwa ikitumia utamaduni wake vizuri kiasi cha kuweza kuinufaisha kiuchumi kwa kuwa ushirikiano wa kiutamduni huimarisha uhusiano wa nchi na nchi na kutoa mwanya kwa ushirikiano wa kiuchumi kufanyika.

Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alifanya ziara ya siku 13 barani Asia akizuru nchi za Japan, Korea Kusini, China, Vietnam ambapo alihudhuria mkutano wa Muungano wa Kiuchumi wa nchi za Asia Pasifiki-APEC yaani Asia Pacific Economic Cooperation sambamba na Ufilipino.

Ziara hii ni ziara ndefu ya kwanza kwa miaka ya karibuni tangu ile iliyofaywa na Rais George H.W Bush mwaka 1992.

Ziara hii ilikuwa na malengo makuu mawili:

(1) Kuunganisha nguvu ya pamoja ili kukabiliana na vitisho vya Korea Kaskazini juu ya mpango wake wa Silaha za Nyuklia na za Masafa Mafupi na Marefu.

(2) Mahusiano ya Kibiashara baina ya Marekani na nchi za Asia hasa China.

Rais Donald Trump alianza ziara yake kwa kuitembelea nchi ya Japan ambapo alikutana na Waziri Mkuu wa Japan Bwana Shinzo Abe na kujadiliana kuhusu suala la kitisho cha Korea Kaskazini.

Waziri Mkuu Shinzo Abe alirejea adhma yake ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na serikali ya Pyongyang. Abe alidai kuwa ni zaidi ya miaka ishirini sasa imepita bila ya nchi hizo kukaa pamoja kwenye meza ya majadiliano na kujaribu kutatua changamoto zao kwa njia ya amani hivyo ni wakati muafaka wa kufanya jambo hilo kwa sasa.

Licha ya Rais Trump kujielekeza zaidi katika masuala ya kijeshi akiwa Japan lakini kwa upande wa biashara Marekani bado inaonekana kutonufaika na mahusiano yake na Japan.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Hazina ya Marekani kwa mwaka 2016 Japan ilikuwa na faida ya kibiashara (trade surplus) ya Dola za Marekani Bilioni 69 dhidi yake na Marekani.

Rais Donald Trump aliaendelea na ziara yake kwa kuitembelea nchi ya Korea Kusini  ambapo aliahidi kuongeza wanajeshi  waliopo katika eneo la kiulinzi la Marekani ndani ya nchi hiyo ili kukabiliana vilivyo na Korea Kaskazini. Sambamba na hilo pia Rais Donald Trump aliahidi nchi yake kuendelea kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi (Joint military drills) ili kujiweka katika hali ya utayari kwa lolote linaloweza kujitokeza.

Licha ya uswahiba mkubwa na Korea Kusini lakini lilipokuja suala la kujadili mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo Rais Trump alishutumu mpango wa biashara baina ya nchi hizo (KORUS) kwa kusema kuwa umekuwa hauna manufaa kwa Marekani na kutishia kuufuta endapo vipengele vinavyoonekana kuiweka Marekani kwenye upande wa kupoteza (Losing side) havitaondewa ama kurekebishwa.

Ingawa Rais Trump alitembelea nchi za Japan, Korea Kusini, Vietnam na Ufilipino lakini mkazo wa ziara yake ulionekana alipozuru China ambapo aliweza kukaa kwa siku tatu.

Rais Donald Trump aliwasili nchi ya China mnamo tarehe 8 Novemba akiwa ameambatana na mkewe Melanie Trump na kulakiwa na mwenyeji wao Rais Xi Jinping. Trump na mkewe walitembelea eneo la kihistoria la makazi ya wafalme wa zamani na familia zao ambao waliotawala China zaidi ya miaka 500 iliyopita linalojulikana kama “The Forbidden City.”

Trump na mwenza wake waliweza kupata chakula cha jioni ndani ya jengo hilo. Trump anakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kupata chakula maalum cha jioni ndani ya jumba hilo tokea kuzaliwa kwa nchi ya China mwaka 1949.

Siku ya tarehe 9 Novemba, Rais Trump alipata nafasi ya kuhutubia viongozi wa China katika ukumbi wa “Great Hall of the people” na kueleza kile kilichoonesha lengo halisi la ziara yake katika nchi za Asia.

“Tunataka biashara baina yetu na China iongezeke”, alisema Rais Donald Trump.

Aliendelea kusisitiza kuwa Marekani inahitaji usawa katika biashara: ” Pia tunataka biashara yenye usawa na yenye kuleta mrejesho (reciprocity) kwa pande zote mbili”.

Rais Trump aliendelea kusema kuwa hailaumu China kwa kutumia nafasi (advantage) iliyojitokeza kimkataba bali alielekeza lawama zake kwa tawala zilizopita kwa kushindwa kuliona hilo.

Trump aliendelea kukazania azma yake ya kuitaka China kupunguza uwiano mbovu wa kimasharti ya kibiashara ambao unapelekea Marekani kutonufaika na mahusiano ya kibiashara yaliyopo baina ya nchi hizo mbili.

Mbali na biashara, nchi hizo pia zimeahidi kushirikiana katika kukabiliana na kitisho cha Korea Kaskazini. Rais Donald Trump alisema, “Dunia nzima iliyostaarabika haina budi iungane kukabiliana na ‘ukichaa’ wa Korea Kaskazini.”

Mnamo tarehe 10 Novemba, 2017 Rais Donald Trump alizuru nchi ya Vietnam na kuhudhuria mkutano wa viongozi (summit) wa nchi za ukanda wa Pasifiki (Pacific Rim) katika mji wa Da Nang.

Rais Donald Trump na Rais wa China walitifautiana mitazamo juu ya biashara ya sasa na kwa miaka ya baadae duniani.

Katika hotuba yake kwa mkutano huo, Rais Trump alikosoa muundo wa biashara ambao kwa maelezo yake “umedhuru wafanyakazi waamerika.”

Rais Trump aliendelea kusema, “Hatutaifanya Marekani ichukuliwe kama srhemu ya kunufaika tena.”

Rais Trump alisisitiza, “Siku zote nitakuwa naweka maslahi ya Marekani kwanza kama ambavyo nategemea ninyi ndani ya chumba hiki kuweka mbele maslahi ya mataifa yenu kwanza.”

Rais Trump aliendelea kusema kuwa hataendelea tena kuhanikiza ushirikiano wa kibiashara kimataifa (multinational trade agreements) badala yake atajikita zaidi katika ushirikiano wa nchi mbili mbili (bilateral trade agreements).

Rais Trump aliendelea kusisitiza kuwa hatavumilia tena mchezo mchafu uliokithiri kwenye biashara.

Katika mkutano huo wa APEC Rais Trump pia aliikosoa taasisi ya biashara ya kimataifa WTO (World Trade Organization) ambayo ndiyo huandaa sheria zinazoongoza biashara duniani kwa kusena, ‘Ni taasisi ambayo haiwezi kufanya kazi sawasawa kama nchi wanachama hazitaheshimu sheria zilizopo’.

Rais Trump aliendelea kulaumu kuwa wakati Marekani ikipunguza vikwazo vya kimasoko na kumaliza vikwazo vya kiforodha nchi nyingine zimekuwa hazifanyi hivyo jambo ambalo limeidhuru Marekani.

Rais Trump aliongeza kusema kuwa biashara huru (free trade) imegharimu mamilioni ya kazi za wamarekani.

Tofauti na hotuba ya Rais Trump, hotuba ya Rais wa China Xi Jinping ilionesha taswira tofauti kiasi cha kuonekana kuwa ndiyo kiranja mpya katika soko la dunia (world trade).

Xi alisema, “Utandawazi ni muendelezo usiorejesheka nyuma (Globalization is irreversible trendy) lakini kuna falsafa zinazoongoza soko huria zinapaswa kutazamwa upya ili kufanya biashara kuwa ‘wazi zaidi’ yenye mizania sawa  na haki kwa nchi zote sambamba na kuwa na manufaa kwa nchi zote.”

Rais Xi alisisitiza kuwa mpango wa biashara wa pamoja (multilateral trade deals) unazisadia nchi masikini kuweza kunufaika.

Rais Xi alisema, “Ni lazima tusaidie mfumo wa biashara wa pamoja (multilateral trade regime) na kufanya muundo huru wa kikanda (open regionalism) ili kufanya nchi wanachama zinazokuwa kiuchumi zinufaike kutokana na biashara ya kimataifa na uwekezaji (international trade and investment).”

KWA NINI ZIARA YA TRUMP CHINA ILIWEKEWA MKAZO?

China ni mnufaikaji mkubwa wa mahusiano ya kibiashara (Bilateral Trade Agreements) baina yake na Marekani. Marekani ina pengo la kibiashara (Trade deficit) la zaidi ya Dola za Marekani Billioni 310 dhidi ya China.

Mbali na hilo la kukosekana uwiano wa kibiashara baina ya nchi hizo, China imeendelea kuwa nchi mdai inayoshikilia hazina kubwa ya deni la Marekani kuliko nchi yoyote ile duniani.

Kwa mujibu wa Hazina ya Marekani, mpaka kufikia mwezi Juni, 2017 deni inalodaiwa Marekani na China liliongozeka kwa bilioni za Marekani 44 na kufikia jumla ya Trilioni 1.15 za Marekani. Imeelezwa kuwa kufikia mwezi August mwaka huu wa 2017 deni limefikia dola Trilioni 1.2 za Marekani.

Mahusiano ya jumla ya kibiashara baina ya China na Marekani kwa mwaka uliopita wa 2016 yalikuwa Dola za Marekani Bilioni 648 lakini mahusiano haya yameonekana kuinufaisha zaidi China kitu ambacho Rais Donald Trump kinamkera.

Katika kile kinachoonekana ni ‘kumridhisha’ Rais Donald Trump, Wizara ya mambo ya nje ya China mara tu baada ya mkutano wa Rais Xi na Trump ilieleza kuwa serikali ya China itaondoa vikwazo kwenye masuala ya kibenki, bima, fedha sambamba na kupunguza ushuru wa forodha kwa kwenye magari.

Ni wazi kuwa Rais Trump na wamarekani wanaumizwa na hali, hali iliyopelekea Rais Trump kusema kuwa vigezo na masharti ya mkataba wa Marekani na China vinaizuru Marekani na watu wake na kuinufaisha zaidi China kwa kufanya biashara kuegemea zaidi China.

Ingawa katika mkutano wake na Rais wa China nchi hizo mbili zilisaini mikataba yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 250 lakini haikuthibitika kama imejumuisha makubaliano ya awali ama matarajio ya mikataba ya baadae.

TRUMP NA MPANGO MPYA WA INDO-PACIFIC

Katika hotuba yake aliyotoa kwa viongozi wa APEC, Rais Trump alisikika mara kwa mara akitamka akizungumzia mahusiano ya mahusiano ya Marekani na nchi za Asia-Pasifiki kwa jina jipya la ‘Indo-Pacific.’

Mfano katika maelezo yake Rais Trump alisikika akisema, “Tutafanya ushirikiano na nchi yoyote ya Indo-Pacific ambayo itataka kuwa mshirika wetu na ambayo itakubaliana na kanuni za usawa na mrejesho katika biashara ambao zinakuwa zenye kuheshimiana na manufaa kwa pande zote (principles of fair and reciprocal trade, mutual respect and benefits)

Indo-Pacific ni dhana iliyoibuliwa hivi karibuni na nchi ya Japan ambayo inazungumzia eneo jipya la ushirikiano wa kikanda la nchi za Asia ukijumuisha nchi ya India ambayo inakuja juu kiuchumi kama iliyotabiriwa na Henry Kissinger ( a new geopolitical view of Asia).

Dhana hii inahanikizwa sana na nchi ya Marekani ikionekana kama mpango mpya wa kukabiliana na utawala wa China kibiashara katika eneo lote la Asia. Rais Trump ameiita dhana hii kama ” Huru na wazi” kwa kingereza “Free and open Indo-Pacific Region.”

Tukumbuke kuwa mara tu baada ya kuingia Marekani Rais Trump alitumia uwezo wake wa kikatiba ulioelezwa kwenye Ibara ya Pili (Article II)  ya Katiba ya Marekani (Law of the Land) kuvunja mkatana wa Trans Pacific Trade (TTP/TPP).

Trans Pacific Trade ni ushikiano wa kibiashara ambao sasa una nchi 11 ambazo kwa ujumla wake zinatoa asilimia 40 ya pato la dunia (GDP) na asilimia 26 ya biashara biashara duniani.

Mpango huu ulikuwa unasimama kwenye maeneo yote muhimu kuanzia biashara hadi kilimo, Rais Trump aliitoa Marekani kwa kueleza kuwa vigezo na masharti vilivyokuwemo kwenye mkataba ule (TTP) umekuwa ukiidhuru Marekani na wafanya biashara wake.

Tukumbuke pia kuwa katika mkataba huu, nchi ya Canada ni sehemu ya wanachama na ndiyo nchi inayoonekana kunufaika zaidi. Marekani ina pengo la kibiashara (trade deficit) dhidi ya nchi ya Canada.

Muungano wa Asia-Pasifiki una jumla ya nchi 21 ambazo kwa ujumla wake zinatoa pato (GDP) la dunia kwa asilimia 60. Kwa msingi huo ni muungano ambao una manufaa makubwa kwa Marekani. Lakini wataalamu wengi wa masuala ya kiuchumi wanadhani sababu alizotoa Rais Trump za kujitoa kwa Marekani Trans Pacific hazikuwa na mashiko, wengi wanaamini kuwa lengo la kujitoa lilikuwa kuelekeza nguvu nchi za Asia ambako kwa hakika Trump ana kazi ya ziada ya kufanya.

Nchi za Trans Pacific zilisema Alhamisi iliyopita kuwa zitaendelea na ushirikiano pasina uwepo wa Marekani. Ikumbukwe kuwa Marekani lilikuwa mshirika mkubwa wa Singapore na Malaysia hivyo kujitoa kwake katika TTP kunaweza kupelekea nchi hizi kutathmini upya mahusiano yao na Marekani.

Rais Donald Trump amekosolewa na wataalamu wengi wa uchumi kuwa Sera yake ya “America First” inaipeleka Marekani mahali pabaya, wakidai kuwa itaifanya Marekani kutengwa katika biashara za kimataifa. Huenda hali hii pia ndiyo iliyopelekea Rais Donald Trump kuilekeza Marekani kwenye ushirikiano wa nchi mbili (Bilateral Trade Agreements) na kuua biashara ya pamoja (multilateral/multinational trade agreements) ingawa Marekani yenyewe ndiyo ilikuwa na mchango mkubwa katika kuasisiwa na kuendelezwa kwa WTO ambayo leo hii Rais Trump anaona haifai.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Iseas Yusof Ishak ya nchini Singapore kwa kuwahoji viongozi wa serikali, wawakilishi wa biashara, wanataaluma na waandishi wa habari Kusini Mashariki mwa Bara la Asia ulionesha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya waliohojiwa walionesha kuwa China ndiyo nchi yenye ushawishi mkubwa kwa sasa katika ulingo wa kimataifa na hali hii itakuwa hivyo kwa miaka kumi ijayo.

Wakati huo huo asilimia mbili ya tatu ya waliohojiwa walisema kuwa ushawishi wa Marekani umepungua ukilinganisha na miezi minne iliyopita. Hii ni kwa mujibu wa utafiti huo wa taasisi ya Iseas Yusof Ishak.

China imeendelea kupanua wigo wake wa kiuchumi kati yake na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia kwa kuziba pengo ambalo limeonekana kuachwa na utawala wa Marekani.

Watafiti wengi wameeleza kuwa licha ya ziara yake barani Asia bado Rais Donald Trump na utawala wake watakuwa wameongeza pengo la biashara baina yake na China badala ya kupunguza.

Maelezo ya Henry Kissinger kuhusu safari yake siri nchi China, kupandishwa hadhi kwa Rais Xi Jinping na mawazo yake kuingizwa katika katika ya Communist Party of China (CPC) kama ambavyo mawazo na falsafa za Mao zilivyoingizwa huenda vimeishtua Marekani na kuona utabiri wa Kissinger unaweza kutumia hivyo kutafuta namna za kuzima utabiri huu kabla haujawa kweli.

  • Abbas Abdul Mwalimu ni mchambuzi wa siasa za kimataifa na diplomasia na ni mwandishi wa makala fupi katika ukurasa wa Facebook Uwanja wa Diplomasia

Simu 0719258484