Home Habari kuu ZIARA YA JPM CHUNGU KWA MAWAZIRI

ZIARA YA JPM CHUNGU KWA MAWAZIRI

1338
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA


Ziara ya kikazi ya Rais Dk. John Magufuli katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa, inatajwa kuwa chungu kwa baadhi ya viongozi wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, madiwani, wabunge na hata wafanyabiashara. RAI linachambua.

Ziara ya Rais Magufuli iliyoanza Septemba 3, mwaka huu na kukamilika mapema wiki hii, ilihusisha mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.

Rais alifanya ziara hiyo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, pamoja na kuzungumza na wananchi, lakini pia aliweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali pamoja na kufungua miradi kadhaa ya maendeleo.

Katika ziara hiyo wapo baadhi ya mawaziri walikutana na uamuzi mgumu wa Rais kwa baadhi yao kukataliwa maombi yao na wengine taarifa zao kupingwa waziwazi.

Miongoni mwa mawaziri waliokutana na uchungu wa ziara ya Rais Kanda ya Ziwa, ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye pia ni mbunge wa Kisesa.

Akiwa mkoani Simiyu, kwenye jimbo la Kisesa, Rais Magufuli aliombwa na waziri wake huyo aridhie jimbo hilo liwe Halmashauri kwa madai kuwa ni kubwa na lina idadi kubwa ya watu.

Rais alilikataa ombi hilo hadharani na kuweka wazi kuwa kutekeleza ombi la waziri huyo ni kuiongezea Serikali mzigo.

Alisema hata Chato yenye watu wengi zaidi ya Kisesa, lakini haijatenga maeneo ya utawala.

“Sababu ya Mpina kwamba kuna  watu wengi ni jambo jingine, hata Chato ina watu wengi zaidi, lakini hatujawapa Halmashauri.”

Mbali na Mpina, waziri mwingine aliyekutana na uchungu kwenye ziara hiyo ya Rais ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.

Katika ziara hiyo ya Rais, Mhandisi, Kamwelwe, alionekana kumpamba mkandarasi wa daraja la mto Sibiti kwa kudai kuwa pamoja na kuchelewa kwa kazi, lakini anafanya kazi nzuri.

Akiweka jiwe na msingi la ujenzi wa daraja la Mto Sibiti na barabara inayounganisha Simiyu na Singida, Rais alilazimika kuwa mkali baada ya kupokea maelezo hayo ya waziri wake.

Katika kumpamba mkandarasi huyo, Kamwelwe alisema kuwa uchelewaji wa daraja hilo umekuwa ukisababishwa na mvua za mara kwa mara.

Akimshushia rungu waziri wake, Rais alisema yeye amekwenda hapo kuhakikisha daraja linajengwa na linamalizika kwa wakati na si kusikiliza visingizio.

“Kwani mkandarasi aliyepewa kazi hii, hakujua kuwa kipande hiki kinaharibika wakati wa mvua, nataka ikifika Machi mwaka kesho kazi hii iwe imekwisha, wananchi wanataka kazi imalizike ili wafanye shughuli za maendeleo.

“Nawaeleza wote nyie wa wizarani na mkandarasi, nitakuja kuwafukuza wote kwa sababu fedha zinazotolewa na Serikali ninayoiongoza ni kodi za wananchi, tena wa chini, kama mkandarasi hana vifaa vya kutosha akakodi, malori yapo mengi, nataka daraja limalizike.”

Katika kudhihirisha uchungu wa ziara hiyo kwa waziri huyo, Rais aliitaka wizara hiyo kujipanga na wakifanya mchezo atawafukuza kwa sababu ya daraja hilo.

Rais alimshangaa Mhandisi Kamwelwe kusimama na kumsifia mkandarasi wakati alipaswa kumfokea ili ahakikishe kazi inafanyika kwa haraka.

Katika kudhihirisha kuwa machungu hayo hayaishii kwa waziri pekee, Rais alimtaka pia Mhandisi wa Mkoa wa Singida, Katibu Mkuu wa Wizara na Mtendaji Mkuu wa TANROADS kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa daraja hilo ili likamilike kwa sababu waliweza kufanya hivyo kwenye madaraja mengi na makubwa.

Maagizo na makatazo hayakuishia kwa mawaziri hao tu, bali pia yalielekezwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , William Lukuvi.

Akiwa wilayani Bunda katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Mara Rais Dk. Magufuli, alimwagiza Waziri Lukuvu kumsimamisha kazi  Kamshina wa Ardhi Kanda ya Mara, kwa kushindwa kutekeleza agizo alilowahi kumpa la kutatua  mgogoro wa ardhi kati ya mfanyabiashara na bibi kizee aitwaye Nyasasi Masike.

Ilielezwa kuwa bibi huyu mwenye zaidi wa miaka 80 alinyang’anywa kiwanja chake na mfanyabiashara  huyo hatua iliyomshangaza Rais ambaye kwa huruma yake alitoa kiasi cha Sh. milioni moja kwa wazee hao.

Aidha, Rais alishangazwa zaidi na hatua ya kutoshughulikiwa kwa jambo hilo, ambalo linafahamika na viongozi mbalimbali wa mkoa, wilaya akiwamo Mkuu wa wilaya,  Lydia Bipilipili pamoja na waziri husika.

Akiwa mkoani Mara, Rais aliwataka wakuu wa wilaya za mkoa wa Mara wahakikishe wanamaliza migogoro ya ardhi inayotokea katika maeneo yao.

Alitoa agizo hilo wakati akizindua barabara ya makutano ya Natta hadi Mugumu yenye urefu wa kilometa 135 katika Uwanja wa Mwenge wilayani Butiama.

Rais Magufuli alisema endapo watashindwa kufanya hivyo hawatakuwa na sababu ya kutawala wakati watu wa nchi moja wanagombea mipaka ndani ya nchi yao.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama mjini Musoma kufuatilia vitendo vya ufisadi vilivyofanywa na mmiliki wa hoteli ya Musoma ,  ambayo alidai kuwa tangu ilipobinafsishwa zaidi ya miaka 10 iliyopita haijaweza kuleta tija jambo linalosababisha serikali kukosa mapato stahiki.

Akiwahutubia wananchi Mjini Musoma Rais Magufuli alieleza kuwa anazo taarifa za mfanyabiashara huyo kuiweka mfukoni idara ya usalama wilayani Musoma hali inayosababisha kufanya atakavyo ikiwamo kuwazuia wananchi kwenda kuogelea kwenye fukwe za Ziwa Victoria.

Mbali na agizo hilo, lakini pia Rais alimkosoa waziwazi mbunge wa Serengeti, Marwa Ryoba kwa kutoa madai ya wizi dhidi ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Juma Hamsini.

Ryoba pamoja na kutoa tuhuma hizo, lakini pia alipendekeza Mkurugenzi huyo atumbuliwe kwa kile alichodai kuwa ni mwizi na mbadhirifu wa fedha za wananchi.

Hata hivyo, Dk. Magufuli alikataa shinikizo la kumtumbua Hamsini ambaye alilazimika kumwaga chozi hadharani kutokana na kutwishwa madai hayo, ambayo Rais alisema kuwa ni ya uongo na uzushi yaliyotawaliwa na siasa.

Akizungumzia suala hilo Dk. Magufuli alisema hawezi kumfukuza mtu kwa kumwonea na kusema kuwa ikiwa viongozi wataingiza siasa katika kazi hawatafanya kazi vizuri.

Pamoja na baadhi ya viongozi kukutana na machungu kwenye ziara hiyo, lakini pia wapo waliopata faraja, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, ambaye alipongezwa kwa utendaji wake mzuri licha ya uteuzi wake kuzongwa na taarifa zilizodai kuwa hafai hata kuwa mkuu wa wilaya.

Alitoa pongezi hizo alipokuwa wilayani Bariadi mkoani humo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 49.7 kutoka Bariadi hadi Maswa.

Katika ziara yake hiyo Rais Magufuli, alipata nafasi ya kuzunguka kwa nyakati tofauti na  mawaziri wake kadhaa kwa lengo la kueleza kile walichokifanya katika kuwatumikia wananchi.

Mwanzoni mwa wiki hii akiwa mkoani Singida, mawaziri sita na manaibu watatu kila mmoja katika jukwaa moja kila mmoja alipata nafasi ya kueleza wananchi namna serikali inavyoweza kutekeleza ilani ya Chama Cha mapinduzi kisekta kwenye maeneo mbalimbali ukiwamo mkoa huo.

Mawaziri hao ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri Kamwele, Waziri Mpina, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye nae pia  katika ziara ya Rais alipokea maagizo kadhaa ya kushughulika nayo.

Waziri mwingine ni Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo na manaibu waziri wa Madini, Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo na Naibu waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Sima.