Home Latest News ZIARA YA JPM MORO IMEFUFUA MATUMAINI

ZIARA YA JPM MORO IMEFUFUA MATUMAINI

5952
0
SHARE
Na Victor Makinda    |

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jonh Pombe Magufuli, ameutembelea mkoa wa Morogoro. Katika ziara yake ya siku nne aliyoimaliza tarehe 7 Mei, Rais Magufuli ameacha, vicheko, furaha na matumaini mapya kwa wakazi wa mkoa huu hususani katika wilaya tatu alizotembelea. Wilaya alizotembelea Rais Magufuli ni wilaya ya Kilosa, Kilombero na Morogoro mjini (Manispaa).

Kama ilivyo ada, wapo hususani viongozi waliobaki matumbo joto, kiti moto wakiwa wakiwa wametawaliwa na wasiwasi wa ama kutumbuliwa au kupata adhabu kali juu ya matendo yao ya kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Ukweli Ulivyo Rais Magufuli kwa sasa ameiacha au kuipumzisha ile staili yake maarufu ya kutumbua papo hapo na sasa anaondoka na kero za wananchi kwa viongozi na kuahidi kuwa anakwenda kuzushughulikia na majibu kupatikana haraka. Staili hii huacha wasiwasi kwa watendaji wazembe, wala rushwa na mafisadi kwani baada ya Rais kuondoka hubaki wakiwa hawajui kesho yao itakuwaje kwa kuwa wameumbuliwa mbele ya Rais ambaye kimsingi huichukia rushwa, huchukia uzembe unyonyaji, kutotimiza wajibu na uzembe.

Watendaji hao walionaswa na watakaonaswa katika mtego huo usingizi wao kwa sasa ni wa taabu kwani wanaiwaza hatima yao ya kesho. Nasema hivi, Rais Magufuli usiwaonee huruma wzembe hao, tumbua tu kwa kuwa wananchi wa Morogoro wanataka maendeleo. Wanakuamini kuwa wewe ni mkombozi wao. Wanaamini kuwa utawavusha. Njia nzuri na rais ya kuwavusha ni kuwazamisha majini viboko na mamba wote ambao wanaweza kuzizuri mbio zetu za kupiga mbizi kuvuka ng’ambo. Tumbua tu viongozi wote wanafiki wanaojikomba na kujifanya wanajali pindi ukiwepo halafu ukiondoka wanaendelea na mtindo waliouzoea ambao ni kikwazo kwa maendeleo ya masikini

Mkala yaUkweli Ulivyo siku ya leo itaanza ikiwa ni sehemu ya kwanza kuangazia masuala anuai yaliyojitokeza katika ziara ya Rais Magufuli mkoani hapa lakini kubwa zaidi mfululizo wa makala haya yenye sehemu ya kwanza leo na sehemu ya pili Alhamisi ijayo nitaanika kinaga ubaga udhaifu uliojitokeza katika ziara ya Rais Magufuli kwa upande wa viongozi wa serikali mkoani hapa hususani wale walio wazembe ambao wameshindwa kutatua hata kero hata ndogo ndogo mpaka kumsubiri rais. Kwa kuanzia tuangazie wilaya alizotembelea Rais na alizokutana nazo.

Wilayani Kilosa

Akiwa wilayani Kilosa,katika Kijiji cha Tundu, kata na tarafa ya Kidodi, rais Magufuli alisimamishwa na wananchi wakiwa na kero kubwa ya upatikana wa maji.

Fedha nyingi zimetolewa lakini maji hayatoki. Mkandarasi ametafuna pesa na mradi umesimama hauna mwendelezo. Hatua hiyo inamlazimu Rais Magufuli kumpigia simu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo na kumtaka kufika kijijini hapo ili kuangalia nini tatizo na utatuzi wake ni upi. Profesa Kitila aliahidi kufika kijijini hapo na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Hapa kuna jambo kubwa la kujifunza. Mkurugenzi wa Wilaya yupo, mkuu wa wilaya yupo, hali kadharika uongozi wa mko upo, lakini mradi wa maji unakwama mpaka rais anasimishwa na wananchi ili awatatulie kero hiyo. Hapa panahitaji mjadala mpana.

Wilaya ya Kilosa kama zilivyo wilaya nyingine inakabiliwana tatizo la maji safi ya kunywa.Pamoja na kwamba katika wilaya hii maeneo mengi yana mito na vyanzo vya maji lakini upatikanaji wa maji ni mgumu mno hususani jimbo la Mikumi, linaloongozwa na mbunge Joseph Haule au maarufu kama Profesa J. Katika kata ya Vidunda yenye vijiji vya Chonwe, Itembe, Khudung’u,na Vidunda, wilayani humo hakuna hata bomba moja la maji safi na salama tangu ulimwengu umweumbwa.

Mji mdogo wa Mikumi ulio katika jimbo la Mikumi una matatizo makubwa ya maji. Wananchi wa mji huo wanahangaika sana kupata huduma hiyo muhimu. Lakini kwa bahati mbaya sana Mbunge wa jimbo hilo, pamoja na viongozi wengine wa serikali wamelala usingizi wa pono huku wakiwaacha wananchi wakiwa katika mahangaiko makubwa ya kutafuta maji.

Rais Magufuli ameagiza viongozi wa mkoa na Wizara husika kuhakikisha maji yanapatikana haraka katika maeneo hayo. Pia amewataka wakandarasi wote ambao wametelekeza miradi mkoani Morogoro kuikamilisha, vinginevyo watashitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Ukweli ulivyo. ikiwa wakandarasi watashitakiwa hawata simama peke yao mahakamani. Hapa kuna baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanaweza kuwa wanashirikiana na wakandarasi kuhujumu kwa ama kuwapa kandarasi makampuni yasiyo na uwezo au kushirikiana na wakandarasi hao kutafuna fedha za serikali. Serikali ya wamu ya tano iwe macho sana juu ya hili. Na kwa picha ya jumla inaonekana rais wetu hana mzaha kabisa kwa masuala ambayo yanakwamisha maendeleo ya wananchi masikini. Kwa muktadha huu hapa furaha inabaki kwa wananchi na wasiwasi na woga unabaki kwa wakandaraji wezi na viongozi walioshirikiana na wakandara wezi. Siku zenu zinahesabika.

  WILAYANI KILOMBERO

Katika wilaya ya Kilombero Rais Magufuli amefanya kazi kubwa. Ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barbara ya Kidatu Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9, amezindua daraja la Kilombero lililopewa jina la Daraja la Magufuli na ameongea na wananchi sambamba na kuwatatulia kero zao. Niseme tu kama kuna wananchi walio furahishwa na kufarijika mno kwa na ziara ya Rais Magufuli mkoani Morogoro ni wananchi wa wilaya ya Kilombero kwa kuwa miradi iliyozinduliwa ina tija mno kwa maendeleo ya wananchi wa Kilombero.

Tukianzia na barabara ya Kidatu Ifakara, Ukweli Ulivyo barabara ya Kidatu Ifakara imekuwa ni kikwazo mno cha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa wilaya ya Kilombero, Ulanga na sasa Malinyi. Barabara hii ni kiungo kikubwa cha uchumi uliochangamka. Kwa miaka mingi tangu ukoloni maendeleo ya wilaya ya Ulanga na Kilombero yalidumazwa na kukosekana kwa barabara inayopitika kwa uhakika katika misimu yote ya mwaka. Licha ya wilaya hizo kuzalisha kwa wingi mazao ya mpunga, miwa, ndizi, mahindi na mengineyo, lakini mazao hayo yalikuwa yakiuzwa bei ya chini mno kwa kuwa miundombinu ya barabara pamoja na daraja kiungo la mto Kilombero kuwa ni mibovu mno.

Ujenzi wa daraja la mto Kilombero maarufu kama daraja la Magufuli, unao shamirishwa sasa na ujenzi wa barabara ya kutoka Kidatu mpaka Ifakara umewaacha na tababasamu na bashasha kubwa wakaazi wa wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi kwa kuwa sasa wanauona mwanga wa maendeleo kwani kikwazo chao cha maendeleo kinaondoshwa.

Wengi wanalia machozi ya furaha huku wakikumbuka vifo vya watu 30 wakati kivuko cha Kilombero kilipozama, wapo waliopoteza ndugu zao wakifia barabarani na kivukoni kwa kushindwa kuwafikisha ndugu hao hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis ya Ifakara kwa sababu tu ama kivuko kibovu, au Barabara haipitiki hususani nyakati za masika.

Wana Kilombero, Ulanga na Malinyi wamefarijika sana kwa ujio wa Rais Magufuli kwani licha ya kufanya uzinduzi wa Daraja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara pia amezungumza nao na kuwaondolea ama kuwapa ahadi ya kutatua kero zao sugu.

Mfano, Rais Magufuli aliposimama na kuzungumza na wananchi wa Mang’ula, aliwaahidi wananchi hao kuwa kiwanda cha Mang’ula Machine and Mechanical Tools(MMMT), kipo katika mchakato wa kurejeshwa serikalini na kupatiwa mwekezaji mwingini huku akiahidi kutuma timu yake kufanikisha suala hilo.

Hapa shangwe na matumaini ya wakazi wa Mang’ula, haina mfanowe. Wananchi hawa wamefurahishwa mno kusikia hivyo.

Ukweli Ulivyo huwezi kuuzungumzia mji wa Mang’ula katika muktadha wa ama kuendelea au kutoendelea bila kukitaja kiwanda cha MMMT. Maendeleo na ukuaji wa mji wa Mang’ula kwa kiasi kikubwa yametokana na kiwanda hili.

Kufa kwa kiwanda hiki kumezorotesha sana maendeleo ya Mang’ula na Kilombero kwa ujumla. Kiwanda hiki baada ya kufa amepewa mwekezaji, Mama Getrude Rwakatare ambaye ki ukweli kimemshinda kwanihakuna kinachoendelea pale zaidi ya mapori yanayofuga wezi na vibaka.

Ahadi ya Rais ya kurejesha kufanya mchakato wa kurejesha kiwanda hiki imetoa faraja kubwa mno kwa wananchi wa Mang’ula. Ombi kwa rais ni kwamba, kiwanda hiki ikiwa kitarejeshwa na kupewa mwekezaji mwingine basi sharti kiwe kinazalisha zana za kilimo au kiwe kiwanda cha kuchakata mazao ya kilimo. Hii itakuwa na tija mno katika ukuaji wa viwanda hasa ikizingatiwa kuwa serikali hii ya awamu ya tano ni ya viwanda vya ukuazji wa thamani ya mazao ya kilimo ni moja ya vipaumbele vyake.

Lakini ni vema pia tukagusia suala la kero za wananchi hao hususani wa Mang’ula na Kiberege katika tarafa hiyo hiyo ya Mangu’ula.

Pamoja na kero nyingine, moja ya kero kubwa ilikuwa ni huduma za mahakama. Mahakama ya Mang’ula inahudumia tarafa nzima ya Mang’ula. Ilikuwepo mahakama nyingine ya Kiberege ambayo kimsingi ilisaidia mno kuwaondolea kero wananchi wa kijiji cha Signal, Mkasu, Kadenge. Lihegama na Mpanga kwa kuwa walipata huduma karibu katika mahakama ya Mwanzo Kiberege.

Mahakama hiyo iliezuliwa paa lake na mvua miaka miwili ilyopita. Tangu kipindi hicho paa hilo halikuezekwa mpaka juzi Rais anapita na wananchi kumlalamikia kuwa wanapata tabu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama. Tatizo ni bati 40 tu, Mbunge yupo, fedha za mfuko wa jimbo zipo, mkuu wa wilaya yupo, madiwani wapo, lakini waliacha wananchi wapte kero mpaka kumweleza rais. Hapa kuna tatizo.

Tatizo kubwa, baadhi ya viongozi wetu wa chama na serikali kwa kweli naweza sema baadhi yao wamelala usingizi wa pono. Hivi kweli, suala la kuezeka paa la mahakama lilioezuliwa, suala la kuchimba matundu ya vyoo katika shule ya sekondari Mang’ula, linashindikana mpaka kumsubiri rais aje aelezwe? Hapa kuna tatizo kubwa la kimuundo, kimfumo na uwajibikaji.

ITAENDELEA WIKI IJAYO…