Home Habari Ziara ya Prof. Kabudi China yaleta neema

Ziara ya Prof. Kabudi China yaleta neema

1109
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

ZIARA ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi nchini China, imezidi kufungua milango ya neema nchini.

Profesa Kabudi alikuwa nchini China kuhudhuria mkutano wa waratibu wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Pia alihudhuria  mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 53 za Afrika na taasisi za fedha za China ambazo ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo kati ya China na Afrika (CAD FUND).

Akiwa nchini humo, alisaini  mkataba wa kupatiwa fedha za msaada wa Sh bilioni 60 za Tanzania kutoka Serikali ya Watu wa China bila ya masharti yeyote ambapo Serikali itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkataba huo umesainiwa na Profesa Kabudi ambaye ameiwakilisha Serikali ya Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China, Zhou Liujun kwa upande wa Serikali ya China.

Mkataba ulisainiwa baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Profesa Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Mjumbe wa Baraza la Taifa, Wang Yi.

Mazungumzo ya mawaziri hao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya China na Tanzania sambamba na  kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya China na Tanzania.

Maeneo hayo ni pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwa  taasisi mahiri ya tiba ya moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawati 358) na Rumakali (megawati 222) mkoani yaliyoko mkoani Iringa na Njombe ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580.

Pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway) sambamba na ukarabati wa reli ya Tazara.

Aidha, katika mazungumzo yao, Serikali ya China imeahidi pia kuunga mkono ujenzi wa miundombinu muhimu katika mji mpya wa Serikali makao makuu Dodoma.

Waziri Yi alisifu uhusiano mwema na wa kirafiki baina ya Tanzania na China na kuongeza kuwa nchi hizo zimekuwa rafiki wa kweli kwa wakati wote.

Kwa upande wake, Profesa Kabudi, aliishukuru Serikali ya China sambamba na kueleza kuwa kipaumbele cha Tanzania ni kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisaiasa na kiuchumi yaliyopo baina ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote mbili.

Pia Profesa Kabudi aliipongeza Serikali ya China na nchi za Afrika kwa kuandaa mpango kazi wa kimkakati ambao umeainisha maeneo kumi ya kipaumbele yakiwemo uendelezaji wa sekta ya viwanda na miundombinu ambayo kwa nchi za Afrika hususan Tanzania ndio kipaumbele cha kwanza.

Maeneo mengine ya kipaumbele ni pamoja na uendelezaji wa biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika pamoja na ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama kwa kutaja machache.

Akihutubia mkutano wa FOCAS, Profesa Kabudi alisema kuwa endapo China itazisaidia nchi za Afrika kwa ufadhili ama kwa mikopo nafuu kuwekeza katika miradi hasa ya miundombinu itakayoziunganisha nchi  hizo kwa kiasi kikubwa, itazisaidia kufanya biashara zenyewe sambamba na kupiga hatua ya maendeleo na kiuchumi kwa kuzifanya ziweze kujitegemea.

Alisema mkutano huo umekuwa ni wa manufaa kwa kuwa nchi zenyewe za kiafrika zimepata fursa ya kutaja baadhi ya miradi ya kipaumbele kutokana na uhitaji wa nchi husika.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji kwa kuwa nchi nyingi za Afrika bado zina vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kuzalisha umeme ambao utakuwa ni wa bei nafuu na kusaidia katika ujenzi wa viwanda.

Katika mkutano huo wa siku mbili nchi za Afrika zimeitaka China kuhakikisha inasaidia ama kufadhili katika kuinua uwezo wa kitaaluma utakaowawezesha vijana kujiajiri na kupata wataalamu wabobezi katika masuala mbalimbali kutokana na uwekezaji hasa wa viwanda na miundombinu utakaofanywa kwa pamoja na China na nchi za Afrika.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba ya  Rais wa China, Xi Jimping, Waziri Yi, alisema kuwa China haitatoa misaada yenye masharti magumu kwa nchi za Afrika, badala yake itaendeleza ushirikiano wake katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Hata hivyo aliahidi kuongeza umoja na ushirikiano kati yake na Afrika katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na usalama  ili kuleta maendeleo endelevu kwa watu na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.