Home Makala ZIJUE DAWA ZA KULEVYA AINA NA ATHARI ZAKE

ZIJUE DAWA ZA KULEVYA AINA NA ATHARI ZAKE

1810
0
SHARE

NA PAUL ENOS


TATIZO la dawa za kulevya limetokea kuwa janga kubwa duniani kote, watu wengi wameathirika na janga hili. Jinsia zote wanaume, wanawake na vilevile rika zote vijana na wazee pia.

Hapa tutaongelea aina mbili za madawa ya kulevya; yaani Cocaine na Heroin. Cocaine hutokana na majani ya mmea ambao kitaalamu unaitwa ‘Erythroxylum coca bush.

Aina hii ya dawa ya kulevya hutolewa kwa mifumo ifuatayo; unga ambapo mitaani hujulikana kama ‘coke’ na hutumika kwa kuvutwa puani kama unga au kuyeyushwa na maji na kuchomwa kwenye mshipa wa damu.

Crack ambapo mitaani hujulikana kwa jina hilohilo crack au rock na hutengenezwa kwa kuchanganywa na kemikali. Na hutumika kwa kuvutwa kama sigara.

Cocaine pindi inapoingia kwenye damu huenda kwenye ubongo na kuzuia ufyonzwaji wa vihisishi vifuatavyo; dopamine, norepinephrine na serotonin kutoka kwenye ubongo.

Hivyo hubakia kwenye ubongo. Na vihisishi hivi husababisha ile hali ya furaha, uchangamfu na kujisikia mwenye nguvu kitaalamu ikijulikana kama euphoria.

Na huweza kuwa kwenye hali hii kwa nusu saa tu. Mara tu baada kutumia dawa hii, dalili zifuatazo hutokea: Mishipa ya damu husinyaa (constricted blood vessels), joto la mwili na mapigo ya moyo huongezeka. Pia shinikizo la damu ‘Dilated pupils’.

Nini madhara ya matumizi ya muda mrefu ya cocaine ?

Matumizi ya muda mrefu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara yafuatayo: Pamoja na kwenda kwenye ubongo husambaa sehemu nyingine za mwili na mzunguko wa damu moyo, kwenye moyo huweza kuleta shambulizi la moyo (heart attack) na vilevile mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio (Arrhythmia), hivyo unaweza kufa ghafla tu.

Ubongo; mishipa ya damu kwenye ubongo inaweza kusinyaa na kupelekea kupata kiharusi, hata kwa kijana. Vilevile unaweza kupata ugonjwa wa akili (substance abuse pyschosis).

Mapafu na mfumo wa hewa, uvutaji kupitia pua huweza kupelekea tatizo sugu la kutokwa damu puani kila wakati na mafua yasiyopona, kupoteza mfumo wa harufu na ikivutwa kama sigara kuharibu mapafu moja kwa moja.

Katika mfumo wa chakula, cocaine husababisha kusinyaa kwa mishipa ya damu kwenye tumbo na utumbo, hivyo kusababisha vidonda na kuweza kuharibu kabisa mfumo huu kwa utumbo kuoza.

Figo; kutokana na shinikizo la damu, figo zinaweza kushindwa kufanya kazi vizuri, vilevile cocaine inaweza kuleta madhara moja kwa moja kwenye figo kitaalamu yanajulikana kama Rhabdomyolysis.

Ngono; ingawa cocaine huweza kutumika kama njia ya kuongeza hamu ya ngono, husababisha kushindwa kumaliza kile ulichokianza. Matumizi sugu ya dawa hii ya kulevya huleta madhara kwa jinsia zote; kwa wanaume na wanawake. Na vile vile huweza kukufanya kuwa tegemezi wa dawa hii.

Kwa wanaotumia sindano kwa pamoja, wanaweza kupata maambukizi ya virusi ya hepatitis na vya ukimwi. Nini hutokea baada ya matumizi ya muda mrefu ya cocaine?

Baada ya kutumia cocaine kwa muda mrefu, punde unapoacha tu kutumia dalili zifuatazo hutokea: Unyong’ovu, uchovu, kushindwa kuzingatia na kutokuwa makini, kukosa uwezo wa kuwa na furaha au kusikia raha, kuongezeka kwa tamaa zaidi ya kutumia cocaine, kujisikia kuumwa, maumivu, baridi na kutetemeka.

Ikitokea mtu akitumia zaidi ya kiwango kinachotakiwa kwa muda mfupi yaani ‘overdose’, kifo cha ghafla huweza kutokea kutokana na madhara yafuatayo; Moyo kushindwa kufanya kazi, kiharusi, degedege mara kwa mara, mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi.

Heroin hujulikana kama diamorphine, hutokana na mmea uitwao kitaalamu ‘opium poppy’. Heroin kwa mfumo wa Morphine hutumiwa hospitalini kama dawa ya maumivu makali ya ghafla (acute pain) kwenye maumivu makali ya kifua wakati wa shambulizi la moyo na kwa maumivu ya mtu aliyepata ajali, vilevile baada ya upasuaji na maumivu sugu kwenye kansa. Hivyo hutolewa kwa kuangalifu mkubwa.

Aina hii ya dawa ya kulevya huweza kutumika kwa kuvuta kwa pua, kuvuta kama sigara na kwa kuchoma kwenye mshipa. Siku hizi watu hutumia njia ya haja kubwa na kwenye uke, ambapo kuta hufyonza heroin na kuanza kufanya kazi ndani ya sekunde arobaini.

Heroin mara tu baada ya kuingia kwenye damu kuenda kwenye mfumo wa neva na kukandamiza ufanyaji kazi wake, ndio huweza kutumika kupunguza maumivu. Dalili za mtu aliyetumia heroin; Kujisikia mwenye furaha, kupishana, kusikia hali ya usingizi na tahadhari, midomo kuwa mikavu, misuli kuishiwa nguvu, kuhema polepole, mikono na miguu kuwa mizito, kope za macho kulegea.

Nini madhara ya matumizi ya muda mrefu ya heroin?

Madhara ya matumizi ya muda mrefu wa dawa hii ya kulevya hutokana zaidi na matumizi ya sindano na vifaa vingine visivyo salama. Pia maambukizi kwenye kuta na milango ya moyo, maambukizi ya ini na virusi (kama hepatitis C na HIV), maambukizi ya figo, maambukizi ya mfumo wa hewa, maambukizi ya ngozi na majipu. Dalili ambazo hutokea mara tu unapoacha kutumia heroin; Kutotulia, maumivu ya misuli na mifupa, kutapika. Dalili hizi hufikia kilele ndani ya masaa 48 hadi 72 na hufika kikomo baada ya wiki.

Makala haya ni kwa hisani ya blog ya EPAMA 2255.