Home Makala ZIMBABWE KULIPA MADENI KWA KUSAFIRISHA TEMBO HAI

ZIMBABWE KULIPA MADENI KWA KUSAFIRISHA TEMBO HAI

945
0
SHARE

Habari za kushangaza kutoka nchini Zimbabwe ni kwamba mke wa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe, Grace Mugabe ambaye ananguvu kubwa ya kisiasa amekuja na mpango wa kulipa madeni ya nchi hiyo yanayodaiwa na nchi ya China.

Mpango huo wa kulipa deni ni kusafirisha wanyama hai wakiwemo watoto wa tembo 35, simba 8, fisi 12 na twiga mmoja.

Deni hilo ni la mwaka 1998 wakati Zimbabwe ilipoagiza silaha kutoka China wakati ilipotuma majeshi nchini DRC kumsaidia aliyekuwa rais wa nchi hiyo Laurent Kabila alipokuwa akipigana na waasi waliokuwa wanasaidiwa na Uganda na Rwanda.

Kwa Zimbabwe kutumia wanyama hai kulipa madeni yake ya nje si kitu kipya, na si nchi pekee kufanya hivyo. Limekuwa suala la kawaida katika nchi kadha kusini mwa Bara la Afrika kuuza wanyama zinaowafikiria kuwa wa ziada nchini mwao na kuwasafirisha kwenye hifadhi za wanyama hai (zoos) mbuga nyingine za wanyama (safari parks) nje ya Bara la Afrika.

Mwezi January 2016, Idara ya samaki na Wanyamapori nchini Marekani (US Fish and Wildlife Service) ilitoa ruhusa kwa nchi ya Swaziland kusafirisha tembo 18 kwenda hifadhi za wanyama za Marekani. Na kati ya 2010 na 2014 takriban faru 500 weupe na tembo 20 walisafirishwa kwenda nje kutoka nchi mbalimbali zenye maliasili hiyo.

Hata hivyo wanyama hai pia husafirishwa kwenda nje ili kusaidia uzalishaji wa wanyama katika hifadhi nyingine Barani Afrika.

Kwa mfano, hifadhi ya Bonde la Bubye nchini Zimbabwe (Bubye Valley Conservancy) ina mpango wa kusafirisha simba kati ya 8 na 10 kwenda Malawi, Rwanda na Zambia. Lengo la usafirishaji huu ni kuzisaidia nchi hizo kuongeza idadi ya wanyama wanaopungua katika hifadhi zao.

Uuzaji huu wa wanyama hai una utata mkubwa, lakini si haramu iwapo tu kanuni zilizowekwa na Shirika la Kimataifa la Kushughulika Wanyama na Mimea Iliyo katika Hatari ya Kutoweka (CITES) zinafuatwa.

Kanuni hizi zinatamka kwamba usafirishaji wa wanyama hai ufanyike baina ya mataifa ambayo ni wanachama wa CITES tu, na kwamba kuna vibali halali vya kusafirisha kutoka mamlaka ya uhifadhi wa wanyama pori wan chi hizo ambavyo vitakuwa vimeidhinishwa pia na CITES.

Mamlaka hizo zinatakiwa zijiridhishe kwamba usafirishaji huo hautaleta athari wa kuendelea kuwapo kwa wanyama wa aina hiyo katika nchi inayosafirisha, na kwamba wanyama hao wanapelekwa nchi zenye uwezo na mazingira chanya ya kuwahifadhi.

Lakini hatua ya Zimbabwe ya kuwaondoa watoto wa tembo kutoka makundi ambayo wamo inadaiwa kuwa itaharibu maisha ya wanyama wenyewe na makundi yake kwa ujumla. Wanaharakati wa hifadhi za wanyama hai wanasema hicho ni kitendo cha ukatili mkubwa kwa wanyama hao.

Ubalozi wa Zimbabwe nchini China imekanusha habari hizo za ulipaji deni kwa njia hiyo lakini Wizara ya Mazingira ya Zimbabwe haijatoa neno lolote kuhusu suala hilo.

Wachunguzi wa mambo wanasema habari hii itaiumbua serikali ya China wakati ambapo nchi hiyo inasifiwa katika hatua yake ya hivi karibuni ya kutangaza marufuku ya biashara ya meno ya tembo.

Ikumbukwwe pia kwamba katika mkutano wa CITES mjini Johannesburg mwaka jana, kundi la nchi wanachama 29 za Bara la Afrika (African Elephant Coalition) zinazopinga biashara ya meno ya tembo au tembo hai ziliomba CITES ibadilishe kanuni ili iweke marufuku ya kusafirisha tembo hai nje ya Bara la Afrika.

Ombi hili lilipingwa na nchi za kusini mwa Afrika na China na hivyo halikuwa na kura za kutosha kupitisha.

Hofu kubwa kwa wanaopinga usafirishaji wa tembo hai kwenda China ni kwamba hapo baadaye wakisha kua pembe zao zinaweza kuvunwa na kuuzwa kwa bei kubwa, hivyo kuathiri marufuku ya biashara ya meno ya tembo.