Home Habari ZITTO, ACT NJIA PANDA

ZITTO, ACT NJIA PANDA

1491
0
SHARE

*Mbowe atajwa


NA GABRIEL MUSHI

NI dhahiri uteuzi wa Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro unakiweka njia panda chama hicho pamoja na Kiongozi wake Mkuu, Zirro Kabwe. RAI linachambua.

Uteuzi wa mwanasiasa huyo ambaye alipeperusha bendera ya chama hicho kwenye mbio za urais mwaka 2015 mbali ya kumweka Zitto njia panda, lakini pia unatajwa kukitikisa  chama cha hicho kwa kiasi kikubwa na huenda kikaingia kwenye  mgogoro wa kiuongozi, unaoweza kukisambaratisha.

Imani ya Kiongozi wake Mkuu kuwa njia panda pamoja na uwezakano wa chama hicho kuingia kwenye kapu la mgogoro wa kiuongozi kama ilivyo kwa chama cha Wananchi-CUF, unaonekana wazi baada ya  Mghwira kuuridhia uteuzi huo wa Rais Dk. John Magufuli, huku akisisitiza kuendelea kusalia kwenye nafasi yake ya Uenyekiti.

Pamoja na kuteuliwa huko, Mghwira ambaye tayari ameshaapishwa na kukabidhiwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameshaweka wazi kuwa kamwe hatong’oka kwenye kiti chake ndani ya ACT-Wazalendo kwa madai kuwa haoni tabu yoyote katika kutumikia nafasi hizo mbili hali inayoonekana kukiweka chama kwenye wakati mgumu kimaamuzi.

Uamuzi wa Mghwira unaonekana kutofautiana sana na ule wa aliyekuwa Mshauri Mkuu wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliji aliamua kujivua wadhifa wake ndani ya chama.

Kwa upande wake Mghwira amesema wanaosema aachie nafasi yake ya uenyekiti wanabeba hoja dhaifu kwa sababu, haoni mahali popote patakapomsababishia kutotekeleza majukumu yake ndani ya mkoa wa Kilimanjaro na ndani ya chama chake.

Kuhusu kukabidhiwa Ilani ya CCM, alisema haoni ajabu kwani hata wao walimkabidhi Rais Dk. John Magufuli ilani ya chama chao alipoingia madarakani.

“Sina mpango wa kuachia nafasi ya Uenyekiti, hoja za kutaka niachie ngazi ni dhaifu, nasema ni dhaifu kwa sababu mbona hawahoji nyadhifa anazozishikilia Mbowe (Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe) “ Mbowe ni Mwenyekiti wa chama, mbunge lakini pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

“Kwanini ajabu iwe kwangu! Nitajipanga vizuri kutumikia nafasi zangu zote mbili, lakini pia ikumbukwe kazi ya Mkuu wa Mkoa ni kutumikia wananchi na suala la chama ni suala la nafasi tu.

 

“Wapo wanaozungumzia juu ya kukabidhiwa Ilani ya CCM, wanasahau hata mimi nilimkabidhi Rais Magufuli Ilani ya ACT-Wazalendo mara baada ya kuchaguliwa.

“Lakini tusisahau kuwa kila mmoja wetu anatekeleza ilani ya CCM iwe mpinzani au chama tawala, chama hiki ndicho kinaongoza nchi, sasa ajabu iko wapi kwenye kutekeleza ilani yake?”alihoji.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hata wabunge wa upinzani ndani na hata nje ya Bunge nao wanatekeleza ilani ya CCM.

Hatua hiyo ya Mghwira inafungua milango ya kumkaribisha bundi wa mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho kwa sababu tayari baadhi ya makada na viongozi ndani ya chama chake, wameshamkalia kooni wakimtaka aidha ajiuzulu au akaimishe wadhifa wake huo kwa Makamo Mwenyekiti bara Shabani Mambo hadi pale uchaguzi wa Kitaifa wa chama hicho utakapofanyika mwezi Machi, mwakani.

Uamuzi wa kuchagua kujiuzulu au kukaimisha nafasi yake unaelezwa kutolewa kwake mara baada ya Mkuu wa Mkoa huyo wa Kilimanjaro kutua nchini mwanzoni mwa wiki hii.

Mghwira ambaye uteuzi wake ulifanyika akiwa nje ya nchi kabla ya kuapishwa na Rais Magufuli alikutana na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya ACT- Wazalendo, ambao pamoja na mambo mengine walitaka kujua msimamo wake ni upi.

“Alipotua tu nchini tulikutana nae na tuliongea nae kwa muda mrefu tukitaka kuujua msimamo wake, alituambia ameridhia uteuzi wa Rais, lakini hataiachia nafasi yake ya Uenyekiti.

“Hatua hiyo ilitushangaza sana, tulimtaka aachie nafasi hiyo ili kumpa nafasi zaidi ya kutumikia ukuu wa mkoa, hata hivyo aligoma, baada ya hatua hiyo tumemtaka akaimishe nafasi yake kwa Makamu Mwenyekiti wa chama upande wa Bara, lakini pia chama kitakaa kikao ili kuangalia namna ya kufanya,”alisema mtoa taarifa wetu.

Zitto ambaye anadaiwa kutimkia nje ya nchi kwa kile kilichoitwa kuwa ni ziara ya siku 10 ya  kichama itakayojumuisha nchi za Uingereza, Ujerumani, Sweeden na Denmark, anatajwa kuwa kwenye wakati mgumu kuzungumzia suala hili na hata alipotafutwa haikuwa rahisi kumpata, hata hivyo katika baadhi ya makundi ya WhatsApp ambayo mwanasiasa huyo anashiriki, amekuwa akisisitiza subira kwa hoja kuwa suala hilo linashughulikiwa.

Aidha, hatua ya Zitto kwenda nje ya nchi na nafasi yake kukaimiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho, Samson Mwigamba inatajwa kuwa hatua nyingine ya kuruhusu kufanyika kwa maamuzi magumu dhidi ya Mghwira.

Tayari zipo taarifa kuwa kama Mkuu wa mkoa huyo ataendelea kung’ang’ania wadhifa wake huo upo uwezekano wa kumvua uanachama.

Wachambuzi wa mambo wanasema uteuzi wa Mghwira umeonekana dhahiri kumvuruga Zitto, ambaye alikuwa mwepesi kumpongeza Profesa Kitila mara baada ya uteuzi wake.

“Uteuzi huu umemvuruga Zitto, haijawahi kutokea akakaa kimya kwenye masuala kama haya, alipoteuliwa Kitila, haraka alimpongeza, lakini angalia kwenye uteuzi wa huyu mama, hajampongeza wala kusema lolote.”alisema mmoja wa watu wa karibu na Zitto.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa uteuzi wa Mghwira hauwezi kukiacha salama chama hicho na kwamba hatua ya sasa ndio njia pekee itakayoweza kuonesha uimara wa chama hicho katika kufanya maamuzi yake ya ndani na kama kitashindwa kusimama imara ni wazi kitaungana na CUF kwenye migogoro ya uongozi.

Kwa muda mrefu sasa CUF inapita kwenye mgogoro mzito wa kugombea madaraka huku vinara wakuu wa mgogoro huo wakiwa ni Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharif Hamad.

Inaelezwa kuwa hatua inayopitia sasa ACT-Wazalendo ni mwendelezo wa safari ya kufifisha upinzani nchini na kwamba chama hicho kama ilivyo kwa CUF kinapitishwa kwenye njia tofauti kidogo.

Wafuatiliaji wa siasa za upinzani nchini wamekwenda mbali zaidi kwa kuweka wazi kuwa hata Chadema imekuwa ikipitishwa kwenye njia za kutaka kukidhoofisha, lakini chenyewe kinabaki kuwa imara kwa sababu ya kujumuisha baadhi ya manguli wa siasa za chama kimoja na zile za vyama vingi.

Hofu ya uteuzi wa Mghwira kukiingaza chama chake kwenye mgogoro inabebwa na hoja moja tu ya wakuu wa mikoa wengi nchini wamekuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa wa Chama Cha Mapinduzi.

Hata hivyo ibara ya 91.(1) (c ) ya CCM inaweka wazi kuwa Mkuu wa Mkoa mwenye nafasi ya kuingia kwenye Mkutano huo ni yule ambaye ni mwanachama wa chama hicho.

Pamoja na katiba hiyo ya CCM kuondoa uwezekano wa Mghwira kushiriki vikao vya CCM, lakini inaelezwa kuwa mwanasiasa huyo bado atalazimika kusimamia kikamilifu Ilani ya chama hicho kwa manufaa ya wananchi wote.

Hatua hiyo inatajwa kuibua ukakasi kwa Mwanamama huyo kuwa na uwezo wa kuvihudumia vyama viwili vya siasa kwa ngazi ya Uenyekiti Ndani ya ACT-Wazalendo na ile ya kusimamia ilani ya CCM mkoani Kilimanjaro.