Home Habari Zitto aungwe mkono kuhusu kuiheshimu sayansi

Zitto aungwe mkono kuhusu kuiheshimu sayansi

474
0
SHARE

NA JAVIUS KAIJAGE

WAKATI taifa na dunia nzima kwa ujumla ikiendelea kukumbwa na janga la virusi vya corona, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemwandikia barua Rais Dk. John Magufuli, akimshauri namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Taarifa ya kumwandikia barua Rais Magufuli, aliitoa mwenyewe Zitto wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 28 mwaka huu.

Zitto alisema kuwa yeye na chama chake waliamua kumwandikia barua Rais Magufuli kwa kuwa janga hilo ni kubwa, hivyo kuna haja ya kushirikiana kwa pamoja na Serikali.

Katika barua hiyo, Zitto alimpongeza Rais Magufuli na Serikali yake kwa hatua zilizochukuliwa katika kupunguza kasi ya virusi hivi zikiwemo wananchi kujizuia na mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni pamoja na kuundwa kwa kamati tatu za baraza la mawaziri ili kuratibu mpango mzima. 

Licha ya Zitto kutoa pongezi hizo lakini  aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika barua hiyo aliyomwandikia mkuu huyo wa nchi ni suala la kuhusu umoja kwa Watanzania wote bila kujali itikadi ya vyama, dini wala makabila huku akimwomba Rais Magufuli kuanzisha kampeni ya kupima virusi vya corona nchi nzima.
“Kama kuna jambo ninalolisisitiza kwa ukubwa wake basi ni kupima kupima kupima, lakini jambo lingine ni kuwepo kwa uwazi wa maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. 

“Nimemsihi Mheshimiwa Rais kwamba tusiongope kuwa wawazi kuhusu jambo hili kwa sababu uwazi una faida kubwa kuliko kuficha”, alisema Zitto katika barua hiyo.


Zaidi ya hapo Zitto alienda mbali kwa kutoa angalizo kwa viongozi na wananchi wote kwa ujumla akisema: licha ya imani zetu za dini tulizo nazo, licha ya nadharia zetu tulizo nazo lakini kamwe tusidharau sayansi.

Kauli ya Zitto ya kuwataka viongozi na wananchi kwa ujumla wake kutoidharau sayansi, huenda ni matokeo ya hali ilivyo hapa nchini na katika mataifa mengine  kwani inavyoonekana kuna hali fulani ya kutofautiana kimtazamo katika kuikabili corona.

Ni dhahiri licha ya mataifa makubwa yaliyoendelea kuchukua hatua madhubuti kwa maelekezo ya wanasayansi hususan wa masuala ya afya bado kwa upande wa mataifa yanayoendelea hususan bara la Afrika na Tanzania ikiwemo, wameendelea kulichukulia suala hili la virusi vya corona kama la kawaida.

Wapo watu wanaoendelea kutumia nadharia kuwa virusi hivi vinawasumbua wenzetu wenye ngozi nyeupe na kwa upande wetu sisi wenye ngozi nyeusi havifui dafu.

Wengine wanasema kwa kumwamini Mungu virusi hivi vitapita tu na wala  hapatatokea majanga katika mataifa yetu.

Ajabu zaidi ni huko nchini Uganda ambako baadhi ya viongozi wa dini, wamekwenda mbali kwa kuwaaminisha waumini wao kuwa Afrika hakuna kabisa virusi vya corona.

Ni kweli kabisa nguvu ya Mwenyezi Mungu hakuna mtu wa kuipinga wala kuifananisha nayo lakini pia ikumbukwe kuwa hata wanasayansi wamewekwa na Mungu kwani huwa wanatumia maarifa ya kisomi na wala siyo ramli.

Kwenye vitabu vikuu vya dini kwa maana ya Biblia takatifu na Quran tukufu vyote vinatambua nguvu ya elimu na maarifa katika kutatua changamoto ambazo huwa zinaikabili dunia.

Katika Biblia takatifu kitabu cha Mithali 4:13, Biblia inasema: mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.

Ni dhahiri kitabu hiki cha Biblia kinasisitiza kumkamata kwanza elimu, pili kutomuacha, kumshika na hatimaye kinafafanua kuwa elimu hiyo ni uzima wetu.

Jambo la kujiuliza ni kwa namna gani elimu inaweza kuwa uzima wetu sisi wanadamu ambao kimsingi tumeumbwa na Mungu kwa mikono yake mwenyewe?

Jibu ni rahisi sana kwamba kupitia elimu ndipo hupatikana maarifa ya kutatua matatizo ya Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii.

Kwa sasa tunakabiliwa na tatizo la virusi vya corona ambavyo si tu vimeendelea kutuathiri kiuchumi kutokana na kutumia rasilimali watu na fedha nyingi ili kukabiliana navyo, lakini pia vimeendelea kutuathiri kisaikolojia kwani tunaenedelea kuishi kwa hofu tunapopata taarifa za vifo vya wanadamu wenzetu.

Hata hivyo pamoja na changamoto zilizopo kutokana na virusi hivi bado wataalamu wa afya na wanasayansi duniani kote wameendelea kutumia maarifa yao ili kuhakikisha virusi hivi vinadhibitiwa na hatimaye dunia na watu wake vinabaki salama.

Tafiti za mara kwa mara zinazoendelea kufanyika ili kubaini kinga, tiba na namna bora zaidi ya kuendelea kujikinga katika njia zitakazosaidia kuepusha maambikizi mapya ya corona, bila kusahau tiba zinazofanyika kwa waathirika, ni matokeo ya matunda ya elimu iliyozaa maarifa kwa wataalamu wa afya na wanasayansi kwa ujumla wao.

Leo hii tunaposikia habari njema kuwa huko China ambako kimsingi virusi hivi vilianzia kwamba maambukizi yamepungua kwa kiasi kikubwa, ni dhahiri mafanikio hayo  hayatokani na miujiza wala matumizi ya nguvu za giza bali ni katika ushauri wa wataalamu wa afya na wanasayansi kwa ujumla.

Si tu biblia inazungumzia kumshika sana elimu bali pia inaendelea kusisitiza umuhimu wa  binadamu kuwa na maarifa ili kuepukana na majanga kwa mfano katika kitabu cha Hosea 4:6 Biblia inasema: watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.

Ni ukweli usiopingika baadhi ya vifo hapa duniani vimekuwa vikitokea si kwa sababu ni mapenzi ya Mungu bali ni wanadamu kukosoa maarifa katika kukabiliana na matukio fulani.

Ukitumia imani ya dini katika kuukabili ugonjwa bila kuchukua hatua za kupata tiba kutoka kwa wataalamu wa masuala ya afya huko nako ni kukosa maarifa ya Kimungu kwani Mungu hayuko hivyo.

Matabibu na wanasayansi kwa ujumla wao,  hawakuwekwa na shetani na bali wamewekwa na Mungu ili kutatua magonjwa, ajali na vitisho vingine ambavyo huwakabili wanadamu katika maisha.

Ni kukosa maarifa endapo kiongozi wa dini atasimama na kuwahamasisha waumini wake kumwamini Mungu katika kutibu magonjwa na katika kutatua changamoto nyingine huku wakipuuzia ushauri na majukumu ya wataalamu wa afya na nyanja nyingine za kisayansi.

Mtume Luka miongoni mwa waandishi wa vitabu vya Biblia, kitaaluma alikuwa ni tabibu wa kutibu watu walioumbwa na Mungu (rejea kitabu cha Wakolosai 4:14)

Si mtume Luka pekee ndiye alikuwa tabibu bali hata Mtume Paul naye alikuwa na maarifa ya kitabibu ndani mwake na ndiyo maana alimwelekeza mfuasi wake aitwaye Timotheo, badala ya kutumia maji kutibu   tumbo lake lililokuwa likimsumbua mara kwa mara, basi atumie mvinyo kidogo (rejea  kitabu cha 1Timotheo 5:23)

Si Biblia takatifu pekee ndiyo hutambua umuhimu wa elimu/maarifa peke yake bali pia hata Quran tukufu inatambua umuhimu huo. Inasemekana katika miongoni mwa hadhi za Mtume Muhammad, aliwahi kuwaambia wafuasi wake kuitafuta elimu hata kutoka katika mataifa ya mbali mfano China.

Mtume Muhamad aliwaagiza wafuasi wake kuisaka elimu huko China ambako tumeshuhudia virusi vya corona vikianzia lakini kutokana na watu wake kuheshimu ushauri wa wataalamu wa afya/wanasayansi wamefanikiwa kupunguza maambukizi.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la tatu la mwaka 2003 inafafanua kuwa dini ni: imani inayohusiana na mambo ya kiroho kwamba kuna ambaye aliumba ulimwengu huu na kwamba ndiye mtawala wa kila kilichomo. Tafsiri ya pili dini ni mfumo fulani wa imani hii na njia ya kuabudu, kusali na kuheshimu/kutii huyo muumba kama vile Ukristi, Uislamu, Uyahudi, Uhindu au Ubuda.

Kwa upande wa sayansi kamusi hiyo inafafanua kuwa sayansi ni: elimu inayotokana na uchunguzi, majaribio, vipimo na kuthibitishwa kwa muda uliopo.

Yote kwa yote ushauri wa Zitto kuhusu   kuheshimu sayansi licha ya uwepo wa imani na nadharia  zetu, hauna budi kuungwa mkono kwani ili tuweze kuiteketeza corona, watu na dini zao hawana budi kushirikiana na Wanasayansi.

Email:  HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com” javiusikaijage@yahoo.com, Simu: 0756521119