Home Habari ZITTO KUONGEZA NGUVU UKAWA

ZITTO KUONGEZA NGUVU UKAWA

1611
0
SHARE

Na Mwandishi Wetu


MWENENDO wa kisiasa nchini unaonekana kumsukuma Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, , kuongeza nguvu za kimapambano ndani ya kundi la vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), RAI linachambua.

Ukweli wa hili unathibitishwa na kauli ya Zitto ya hivi karibuni, kuwa ni lazima kuangalia picha kubwa, kwani leo upinzani wote unashughulikiwa, hivyo ni chaguo lao kufa mmoja mmoja au kufa kwa pamoja.

“Lazima kuangalia picha kubwa. Leo upinzani wote unashughulikiwa. Ni chaguo letu, kufa mmoja mmoja au kufa kwa pamoja,” alisema Zitto.

Mbali na kauli hiyo, lakini pia katika siku za karibuni Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, ameonekana kushirikiana na baadhi ya viongozi wa juu wa Ukawa kwa maneno na matendo, jambo ambalo halikuwapo kabla.

Awali Zitto, ambaye alijiunga na ACT-Wazalendo  mwaka 2015 akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikuwa akitajwa na baadhi ya wapinzani wenzake kama msaliti na kwamba hata chama alichojiunga nacho kilikuwa na nia ya kuua upinzani na kusaidia CCM kwa hoja ile ile ya usaliti.

Hali iliendelea kuwa hivyo hata wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Bunge la 11, lililofunguliwa na Rais Dk. John Magufuli,  wabunge wote wa upinzani walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kwa hoja kuwa hawamtambui Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ni Zitto pekee ndiye mbunge wa upinzani alisalia bungeni, kitendo kilichokoleza hoja ya usaliti.

Hata hivyo, katika hali inayoashiria kumaliza tofauti za kisiasa,  Zitto, ambaye anabeba taswira ya ACT-Wazalendo, ameanza kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Ukawa.

Uamuzi huu wa Zitto unaonekana ni mwanzo wa kutekeleza kauli ya mshauri wa chama chake, Prof. Kitila Mkumbo, wa kutaka muungano imara wa vyama vya siasa vyenye nguvu.

Kitila alipata kutoa ushauri huu wakati wa mchakato wa kuelekea kwenye chaguzi ndogo za madiwani zilizofanyika mwezi uliopita.

Katika kufanikisha hilo, Zitto tayari ameanza kushiriki kwenye baadhi ya matukio binafsi yanayowahusu  baadhi ya viongozi na wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa.

Miongoni mwa matukio hayo ni hatua yake ya kusafiri hadi gereza la Kisongo, jijini Arusha, kwa nia ya kumjulia hali Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliyekamatwa mjini Dodoma Novemba 2, mwaka jana.

Zitto, ambaye ni mbunge pekee ndani ya Bunge asiyefungamana na Ukawa, pia kwa sasa amekuwa akishirikiana na wabunge wa umoja huo katika hoja mbalimbali.

Ushirika huo ulikolea zaidi pale Zitto alipoomba mwongozo kwa Spika, akipinga njia zilizotumika kumkamata Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, aliyekuwa akihudhuria mkutano wa Bunge na kumsafirisha hadi Dar es Salaam bila  taarifa kufikishwa kwa Spika wa Bunge.

Katika maelezo yake, alisema Bunge linapaswa kuilinda hadhi yake kwa mujibu wa kanuni ya 51, kanuni ndogo ya 51(1) hadi 51(4), jambo linalohusu mamlaka ya Jeshi la Polisi kukamata waheshimiwa wabunge wakati mikutano ya Bunge ikiendelea.

Alisema: “Tunafahamu kwamba, kwa mujibu wa sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, sheria hiyo imezuia mbunge yeyote kukamatwa ndani ya viunga vya bunge, isipokuwa tu kwa ruhusu ambayo imetolewa na mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

Aidha, Zitto pia alijitwisha hoja ya kupinga kukamatwa kwa Lema, ambaye hadi sasa bado yuko mahabusu pamoja na hukumu ya miezi sita jela aliyokumbana nayo Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali.

Anasema wote hao walikamatwa huku Spika akiwa hana taarifa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha taratibu na desturi za mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo ilipaswa hakimu atoe taarifa rasmi kwa Spika wa Bunge.

Katika kuhakikisha Ukawa unaimarika na kuwa na nguvu ya pamoja, Zitto aliketi meza moja na Mbowe, katika mkutano uliofanyika mjini Dodoma, uliolenga kujibu tuhuma za kuhusishwa na biashara za dawa za kulevya.

Katika mkutano ule, Zitto alipewa nafasi ya kuzungumza na alitumia muda wake kumtetea Mbowe, huku akihusisha tuhuma hizo na chuki za kisiasa.

Bila kumung’unya maneno, Zitto alisema, dhamira yake ya kwenda kwenye mkutano huo ni kuunganisha nguvu na wapinzani wenzake kwa sababu vita ile ina lengo la kushambulia demokrasia nchini.

Uamuzi wake huo ulishangaza wengi, hali iliyoibua mjadala kwenye maeneo mbalimbali, huku baadhi ya vijana wa chama chake wakimlaumu kwa hatua yake hiyo.

Hata hivyo, Zitto katika maandiko yake alijibu mashambulizi hayo kwa kuwaeleza vijana hao kuwa makini kwa sababu anajua anachokifanya.

Katika andiko lake anawaambia: “Mnasema nimekosea na wengine mnakwenda kunipinga mitandaoni ili Makonda awaone. Vijana muwe makini sana. Hii ni siasa, mimi najua nafanya nini.

“Siwezi kuhatarisha ‘image’ yangu ama ya chama. Ninajua kuna mchezo wa siasa na bila kuungana na wengine tutapigwa wote. Mimi nina taarifa nyingi kuliko ninyi nyote”.

Pamoja na mambo mengine, kwa sasa Zitto amekuwa akifanya mambo kwa kushirikiana na wabunge wengine wa upinzani, tofauti na awali, ambapo kwenye mkutano wa sita uliomalizika hivi karibuni aliridhia kumwachia dakika kadhaa Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea.

Pia Februari 15, mwaka huu, alikwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfariji Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya uchochezi.

Kama hiyo haitoshi, Zitto pia alimtembelea nyumbani kwake Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, ambaye kwa sasa ni mgonjwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya uongozi wa Chama cha Wananchi -CUF, Julius Mtatiro, Januari 23, mwaka huu, alipata kuandika kuwa ACT –Wazalendo kinahitajika Ukawa.

Kwa maneno yake, Mtatiro anasema kwamba sababu ya chama hicho kutakiwa katika Ukawa ni mafanikio iliyopata katika uchaguzi mdogo uliofanyika Januari 22, mwaka huu.

Mtatiro aliandika: “Uchaguzi huo ACT ndicho chama kilichofanikiwa kuliko vyama vyote, ikiwamo CCM, pamoja na uchanga wake, kimevishinda baadhi ya vyama vikongwe kwenye kata chache kwa idadi ya kura na si ushindi wa jumla.

“Ushindi huo ni ‘alert call’ kwamba ACT inahitajika katika kapu la Ukawa na kwa hiyo ianze kujiona kama ‘true party’, wakati Ukawa pia ikikiandalia mazingira kisaikolojia”.

Kwa upande wake, amesema kwa mujibu wa katiba ya chama chao, linapotokea jambo linalohusu chama waamuzi huwa na vikao vya chama.

Kwa sasa Ukawa unaundwa na chama cha NLD, ambacho ni kama hakipo.  NCCR-Mageuzi, tayari kimeshaingia kwenye mgogoro wa ndani, CUF ambacho kimepasuka na Chadema ambacho ndicho pekee kilicho imara kwenye umoja huo.