Home Tukumbushane AU inapingana na misingi yake!

AU inapingana na misingi yake!

2407
0
SHARE

Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi (kulia) akikabidhiwa uenyekiti wa AU kutoka kwa Rais Paul Kagama wa Rwanda mjini Addis Ababa mapema wiki hii.

HILAL K SUED

Wiki iliyopita Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao akirithi nafasi hiyo kutoka kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Kuchaguliwa kwa rais huyu ni kielelezo kimoja cha changamoto za Bara hili kuhusu uduni wa maendeleo yake, ukosefu wa demokrasia ya kweli, ukosefu ambao umesababisha kutoweka kwa utawala bora na hivyo kushamiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi yake. Kwa ujumla AU inapingana na misingi na malengo yake yenyewe kama ilivyoasisiwa.

Tayari wadadisi wa masuala ya siasa barani wanasema kwamba Sisi hakupaswa kuongoza Umoja huo kwa sababu kuingia kwake madarakani nchini mwake hakukuwa kwa kidemokrasia – ni kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa rais aliyechaguliwa kihalali kwa kura – Mohamed Morsi mwaka 2013.

Ikumbukwe Misri, tangu mapinduzi yaliyouondoa ufalme mwaka 1952 imekuwa ikitawaliwa na wanajeshi na demokrasia ilianza kurejea baada ya kuanguka kwa Hosni Mubarak mwaka 2011 na uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia ulifanyika Juni 2012 na kumuingiza Morsi madarakani.

Na kutokana na kwamba AU ilipitisha azimio la kutozitambua tawala zilizoingia madarakani kimabavu – yaani kijeshi, AU ilisimamisha Misri, chini ya Sisi, kama mwanachama kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.

Sasa pamoja na kufanya uchaguzi mapema mwaka jana (2018) uchaguzi uliotuhumiwa kutokuwa huru na wa haki (wagombea mashuhuri wa upinzani waliuzuliwa kugombea na wengine kutupwa gerezani) Sisi pia anatuhumiwa kuendesha utawala unaokiuka misingi ya haki – watetezi na wanaharakati wengi wa haki za binadamu wakiwemo waandishi wa habari wametupwa jela kupitia michakato ya mahakama isiyofuata misingi ya haki.

Wiki iliyopita Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alitembelea Misri na kumtaka Sisi airekebishe hali hiyo inaloiletea nchi sifa mbaya mbele ya uso wa dunia.

Sasa kuna hoja kwamba iwapo nchini mwake (Misri) anaendesha utawala wa kibabe usiofuata misingi ya kidemokrasia na haki je anaweza kusisitiza hivyo katika nchi za ndani ya Umoja, ambako nyingi zinaendeshwa kwa namna kama yake?

Kwa mfano, sasa hivi ana mpango wa kurekebisha katiba ya nchi yake ili kujiongezea muda wa ukomo – suala ambalo limekuwa sugu barani Afrika na kusababisha kuwepo kwa chaguzi za kiini macho na hivyo kuibuka kwa farakano nyingi na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe na maendeleo duni. Je, anaweza kukemea tabia hiyo iwapo yeye mwenyewe tayari ameanza kuiiga nchini mwake?  

Na ukitaka uthibitisho wa nchi nyingi katika Bara hili la Afrika kuwa na maendeleo duni zaidi ya miaka 50 baada ya uhuru, angalia jinsi uhamiaji haramu unavyozidi kushamiri miongoni mwa nchi mbali mbali. Lakini awali naomba nieleweke – ninaposema ‘maendeleo’ namaananisha maendeleo ya watu, na siyo vitu.

Watu wengi bado hali zao ni duni Barani humu. Na uduni huo unatokana na usimamizi mbovu wa rasilimali za nchi ambazo hunufaisha wachache tu na wawekezaji wageni. Hivyo watu wako tayari kuzihama nchi zao kwenda kutafuta nafuu ya kuishi katika nchi nyingine ambako hufikiri uwezekano wa kupata neema. Huwa hawafikiri kwamba nako huko kuna matatizo kama hayo wanayoyakimbia.

Miaka michache iliyopita kulizuka ghasia kubwa Afrika ya Kusini baina ya wazalendo wa huko – pale walipoanza kuwashambulia wageni kutoka nchi nyingine, hususan nchi zile za za jirani waliokwenda huko kutafuta kazi. Wazalendo walijikuta wanagombania ajira na wageni, kwani wao wenyewe ajira zilizopo hazitoshi.

Aidha humu Tanzania tumeshuhudia katika miaka ya karibuni wimbi la wahamiaji haramu wanaopita kwenda kusini mwa Afrika kutafuta neema ya maisha. Hawa wamekuwa wakikamatwa na mamlaka za uhamiaji na kufunguliwa mashitaka na hata kufungwa gerezani. Safari zao huwa za hatari sana kwani wengine hufa njiani katika makontena kwa kukosa hewa. Pamoja na hatari zote hizi, uhamiaji haramu wa namna hii haujakoma.

Kuna wengine wanakimbilia Bara la Ulaya – kwenda nchi ambazo zilikuwa zinawatawala, na kusahau kwamba huko nyuma mababa na mama zao waliwaona wakoloni hao ni wakandamizaji, waporaji wa ardhi na rasilimali zao na kila kitu kibaya walichokuwa wakifanyiwa n.k. sababu kubwa ya haya ni kwamba viongozi wa Afrika wamawaangusha pakubwa sana watu wao.

Siku hizi ‘demokrasia’ barani humu limekuwa ni neno lisilokuwa na maana yoyote, kwani kila mtu, watu, au vikundi vya watu hutoa tafsiri inayolenga kulinda masilahi yao, na si masilahi ya waliyo wengi. Hawa hutulizwa kwa viambatanisho vyake – yaani propaganda zinazoenezwa kwa uwezo wao wa kifedha.

Na ndiyo sababu wananchi walio wengi hujikuta katika njia panda, bila msaada wowote, na katika jitihada za kujikwamua, huamua kuchukua njia ya kuwakwepa wawakilishi waliochaguliwa ambao huwaona si chochote bali ni watu wa kati wanaowakilisha masilahi ya nguvu hizo za makampuni.

Takriban miaka 20 iliyopita ilipoanzishwa AU kama chombo mbadala cha iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kilibuniwa ndani yake chombo kingine kilicholenga kudhibiti hali hii – yaani kusisitiza utawala bora katika nchi za Kiafrika.

Jukumu kubwa la chombo hicho – African Peer Review Mechanism (APRM) lilikuwa ni kusisitiza nchi zijiratibu (self-monitoring) zenyewwe katika kuzishawishi kuwepo na usawa na maadili yanayopaswa katika masuala ya uchumi na ya siasa katika lengo zima la kuleta maendeleo ya uchumi na ya kijamii katika nchi za Afrika.

Sasa hivi ni vigumu kusema kuna mafanikio yoyote katika lengo hilo. Tuchukulie siasa, kitu ambacho kama kinaendeshwa vyema kwa misingi inayokubalika ya kuwapa wananchi sauti ya kujiamulia mambo yao, ambacho ndicho kingewakwamua kutoka katika maendeleo yao duni.

Iwapo AU yenyewe, ambayo kwa kiasi fulani inao uwezo wa kuingilia masuala ya migogoro ya siasa ya nchi wananchama wake imeshindwa kumaliza migogoro katika nchi kadha, sembuse hili suala za kuzitaka nchi ziwe zinajiratibu zenyewe katika masuala ya utawala bora? 

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kumekuwapo mapinduzi ya kijeshi nchini Mauritania, Guinea, Ivory Coast, Madagascar, na Mali, Burkina Faso, Misri na Zimbabwe. Pia kumekuwepo mapinduzi yaliyochochewa na umma katika nchi za Tunisia, Misri na Libya na machafuko ya kisiasa nchini Kenya, Zimbabwe, Ethiopia, Congo (DRC) na Malawi.

Mengi ya matukio haya yalitokana na uendeshaji mbovu wa chaguzi ambazo kwa kuwa husimamiwa na wateule wa viongozi walio madarakani, basi ni vigumu matokeo yake kuwa vingine zaidi ya kuwarudisha madarakani wale wale.

Au chukulia nchi ya Guinea, mojawapo ya nchi za kwanza kwanza kabisa katika Bara hili kujipatia uhuru. Kwa muda wa miaka 50 iliyofuatia, nchi hiyo ilitawaliwa na madikteta wawili – Ahmed Sekeu Toure na Lassana Conte, kila mmoja miaka 25, na wote wawili hao vifo ndiyo viliwaondoa madarakani. Wananchi wa Guinea, pamoja na utajiri wa madini, bado ni masikini sana.

Hali kama hiyo pia inapatikana katika nchi nyingine kama vile Congo (DRC) ambayo utajiri wa madini yake haujawanifaisha wananchi humo katika zaidi ya miaka 50 ya uhuru wake. Hata kama ilishindikana kuwaendeleza wananchi, basi hata kuendeleza miundombinu?