Home Afrika Mashariki Usafiri ajenda muhimu EALA

Usafiri ajenda muhimu EALA

5276
0
SHARE


MWANDISHI WETU

BUNGE la Afrika Mashariki (EALA) limeanza jijini Arusha, nchini Tanzania, huku suala la usafiri na usafirihaji likitazamwa kwa umakini zaidi.

Tayari kwenye ratiba ya shughuli za mkutano wa tano wa Bunge ulioanza mapema wiki hii, suala la wabunge wa Bunge hilo kukutana na baadhi ya wadau wa Mpango wa Usafiri na Usafirishaji (TTTFP), limepewa kipaumbele.

Dhamira kuu ya EALA ni kuhakikisha kunakuwa na uimarishwaji wa sekta ya miundombinu hasa barabara kwa ajili ya usafiri na usafirishaji.

Mpango huo kwa pamoja unaunganisha nchi zote wanachama wa Jumuiya za Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

Mbali na Bunge hili kulipa kipaumbele suala la MUSWAD Ana usafirishaji, pia limedhamiria kuupitia muswadawa Baraza la Vijana la Afrika Mashariki wa mwaka 2017 pamoja na Ripoti za Kamati za Utalii, Kilimo na Maliasili.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bunge la EALA kwa vyombo vya habari jijini Arusha, Bunge hilo litaendelea kwa wiki tatu hadi Mei 18, 2019 litapomalizika.

Mambo mengine yanayotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa wakati wa vikao vya bunge hilo ni Ripoti za Kamati za Bunge kwa ajili ya Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2017.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa lengo la muswada huo wa vijana wa mwaka 2017 ni kutoa mwongozo wa kisheria ili kuweka sawa sheria na sera, zinazowahusu vijana katika jamii ya nchi husika.

Muswada huu wa sheria upo katika kipengele cha 120 katika Sheria za Mkataba wa Uundwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao una dhima ya kusimamia utekelezwaji wa Sera ya Vijana wa Afrika Mashariki, 2014. Mwezi uliopita Bunge la Afrika Mashariki, liliendesha majadiliano ya umma katika nchi wanachama ili kupata mawazo ya vijana kama wadau mojawapo katika muswada huo.

Pia kutakuwa na vikao vya Kamati zote za Bunge, ambapo katika wiki ya kwanza kutakuwa na majadiliano ya mambo mbalimbali katika vikao vya kamati. Bunge la Afrika Mashariki lina Kamati sita za Bunge, ambazo ni Kamati ya Hesabu, Kamati ya Kilimo, Utalii na Maliasili, Kamati ya Mambo ya Jumla, Kamati ya Mambo ya Kikanda, Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji, Kamati ya Mambo ya Kisheria na Kamati ya Usuluhishi wa Migogoro.