Home Makala PAMOJA NA AMANI NA UTULIVU ULIOPO: MAENDELEO YA DEMOKRASIA BADO KIZUNGUMKUTI

PAMOJA NA AMANI NA UTULIVU ULIOPO: MAENDELEO YA DEMOKRASIA BADO KIZUNGUMKUTI

1966
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Historia ya nchi hii inaonyesha kwamba mara mbili na katika vipindi na awamu mbili tofauti, utawala wa CCM uliandaa mazoezi ya kutafuta maoni ya wananchi kuhusu mustakabali wao wa kisiasa.

Na mara zote mbili utawala ulikataa (au tuseme ulipindua) kile wananchi walichoamua na utawala kulazimisha kuweka ilichotaka. Kwanza mwanzoni kabisa miaka ya 90 lilikuwapo zoezi la kutafuta maoni iwapo wananchi wanataka kuwepo na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi lililoendeshwa na Tume ya marehemu Jaji Francis Nyalali.

Matokeo yalikuwa kwamba takriban asilimia 80 ya wananchi walikataa mfumo wa vyama vingi na kupendekeza mfumo wa chama kimoja uliokuwapo kwa takriban miaka 25 iliyopita uendelee. Hata hivyo utawala uliamua kuiingiza nchi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Zoezi jingine la kutafuta maoni ni lile la kuhusu Katiba mpya miaka minne iliyopita chini ya Jaji Joseph Warioba, zoezi ambalo lilijikita zaidi katika mfumo wa Muungano; iwapo kuwepo Muungano wa Serikali tatu au uendelee huu huu uliopo wa Serikali mbili.

Matokeo yake ni kwamba wananchi wengi walitaka muundo wa muungano wa Serikali tatu, pandekezo ambalo watawala walilipindua kwa kulazimisha muundo huu uliopo wa Serikali mbili uendelee. Sote tunafahamu kilichotokea ambapo mchakato mzima uliogharimu mabilioni ya pesa umetiririka kwenye mtaro wa maji. Hili nitalirejea hapo mbele kwanza turudi miaka 25 ilyopita.

Wengi waliona kwamba uamuzi wa kuingiza nchi katika mfumo wa vyama vingi ulikuwa ni uamuzi mgumu kwani ulikuwa kitanzi kwa utawala wa CCM, kulikuwa hakuna kitu cha kuuzuia utawala huo kwenda na maji. Suala la vyama vingi lilitokana na mabadiliko ya upepo wa kisiasa uliovuma duniani mwishoni mwa miaka ya 80 na ulioanzia katika nchi za Kikomunisti za mashariki ya Ulaya, ikiwemo ile ya Urusi ya Kisovieti (Soviet Union – au USSR).

Hiyo ilitokana na kushindikana kwa itikadi ya Kikomunisti baada ya wananchi wa hizo nchi kudai uhuru zaidi wa kiuchumi, wa kisiasa na wa kujieleza. Baadhi ya nchi hizo mageuzi ya mfumo yalikuja kwa amani na utulivu kama vile Czechoslovakia, Bulgaria, Hungary, Urusi yenyewe na kadhalika, lakini nchi kama Romania na Yugoslavia mageuzi yaliambatana na vurugu kubwa za umwagaji damu.

Ni vyema kutaja hapa kwamba baadhi ya nchi hizo, kama vile Urusi na Romania zilikuwa maswahiba wakubwa wa Tanzania kutokana na itikadi ya ujamaa, hivyo kulikuwapo hofu ya kiasi fulani miongoni mwa watawala wetu kwamba tusiporekebisha kwa amani mfumo wa demokrasia yetu, basi huenda tutalazimika kurekebisha kwa njia ngumu.

Kwa ujumla watawala waliogopa ile dhana ya matokeo ya dadu ‘domimo effect’ yaani vipande vya dhumn vilivyopangwa kwa kusimamishwa mezani kimoja kikianguka basi hulalia cha pili yake, nacho hicho hulalia cha tatu yake, vivyo hivyo hadi vyote huanguka kwa kulaliana.

Hata hivyo, watawala waliona kwamba iwapo mageuzi watayafanya chini ya uratibu na uangalizi wa Serikali yao, basi watahakikisha upinzani haupati mwanya. Na tukiongelea upinzani, hadi mchakato wa kutafuta maoni chini ya jaji Nyalali unaanza, kulikuwa hakuna upinzani kwa maana ya ule uliohamasika (organized) na wenye uongozi uliokuwa ukijulikana, ingawa kwa hakika ulikuwapo ule upinzani uliokuwa hauonekani.

Lakini angalia jinsi upinzani ulivyokuja kwa nguvu baada ya Katiba kurekebishwa na vyama kuruhusiwa kiasi kwamba hadi uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi (1995), upinzani ulikuwa tishio kubwa kwa CCM.

Lakini tishio zaidi lilikuwa ni visiwani kwani matokeo (yasiyo rasmi) ya uchaguzi huo yalionyesha CCM imeshindwa kiasi kwamba hadi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, aliandika barua ndefu kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), akilalamika kwamba chama chake hakiko tayari kukubali matokeo yanayotarajiwa kutangazwa.

Yaliyofuata ni historia na suala zima la uchaguzi limekuwa likiitesa sehemu hiyo ya Muungano katika chaguzi zote nne zilizopita.

Kwa upande wa bara yaliyotokea katika nchi jirani ya Zambia (pia swahiba mkubwa wa Tanzania) katika uchaguzi wao wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1991, yaliufanya utawala wa CCM kuingiwa na wasiwasi. Swahiba wake mkubwa tangu enzi za kupigania uhuru Kusini mwa bara la Afrika, Rais Kenneth Kaunda aliangushwa katika uchaguzi na Frederick Chiluba wa Chama cha Upinzani cha MMD (Movement for Multiparty Democrasy).

Lakini wengi waliona kwamba kushindwa kwa Kaunda zaidi kulitokana na hulka yake binafsi ya kukubali mara moja kushindwa kuliko kutafuta njia za kiujanja ujanja au za kibabe za kutaka kuendelea kukaa madarakani, kitu ambacho viongozi wengi barani Afrika wamekuwa nacho ili kuendelea kutawala nchi zao.

Wengi waliona alichokifanya Kaunda kingeweza kuwa mfano mzuri kwa viongozi wa bara hili, lakini haikuwa hivyo. Sasa hivi suala la kukubali kushindwa kwa viongozi walio madarakani (incumbents) limeanza kujitokeza tena hasa kwa nchi za Afrika Magharibi ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, viongozi wa nchi tatu; Nigeria, Ghana na Gambia walikubali kushindwa na kuwapongeza wapinzani wao walioshinda. Hata hivyo, huyu wa Gambia alibadili msimamo wiki moja baadaye, lakini aliondolewa kwa nguvu ya nchi za jirani.

Hapa kwetu chama tawala (CCM) kimekuwa kikishinda kila chaguzi ingawa asilimia ya ushindi wake hasa katika kura za urais zimekuwa zikiporomoka na zile za upinzani kupanda, hasa katika chaguzi mbili zilizopita.

Pamoja na hayo, CCM imebakia kuwa ni chama pekee cha upinzani ambacho bado kipo madarakani na kikongwe zaidi katika ukanda huu wa Bara la Afrika, kikifuatiwa na Frelimo (Msumbiji) na MPLA (Angola) ingawa hivi viwili awali vilikuwa vyama vilivyopigana vita vya msituni vya ukombozi wa nchi zao.

Lakini wachunguzi wengi wanaona kwamba siri kubwa kwa CCM kuendelea kukaa madarakani haiko hasa katika kukubalika kwa umma, bali ni kutokana na Katiba pendelevu iliyopo ambayo ndiyo hiyo hiyo ilikuwa inatumika katika mfumo wa chama kimoja, baada ya kutiliwa viraka hapa na pale kuruhusu uwepo wa vyama vingine.

Kwa mfano Tume ya Uchaguzi (NEC) ambayo ndiyo inasimamia chaguzi za Urais, Ubunge na Udiwani haiko huru pamoja na madai ya siku zote ya wakuu mbalimbali wa taasisi hiyo kwamba iko huru.

Watu muhimu wa Tume wakati wa uchaguzi; wakurugenzi wa halmashauri (za miji na wilaya) na ambao ndio kwa sheria (zilizopo) wanakuwa ‘wasimamizi wa uchaguzi’ na wanaotangaza matokeo huteuliwa na rais wa nchi katika nyadhifa zao hizo za ukurugenzi. Na si mara moja au mbili, tumeona wakurugenzi wakihamishwa kutoka vituo vyao vya kazi wakati uchaguzi unakaribia pamoja na zile chaguzi ndogo.

Hilo pia hutajwa kwa mwenyekiti mwenyewe wa NEC na makamishna wake (na watendaji wengine wakuu), wote ni wateule wa rais wa nchi ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala na ambaye ndiye hugombea nafasi ya urais katika chaguzi.

Kwa ujumla ili kuimarisha demokrasia ya vyama vingi na kuwa na upinzani halisi katika uwanja ulio sawa, Katiba mpya inatakiwa. Lakini fursa ya kuipata Katiba hiyo iliyokuwepo katika Awamu ya Pili ya utawala wa Jakaya Kikwete imepotea na kuondoka kwake. Lakini kuna kitu kimoja kilicho dhahiri hapa.

Kama nilivyosema Katiba mpya inaweza kuuathiri uhai wa CCM kuwapo madarakani hasa pale mapungufu ya Katiba na sheria zinazokipendelea chama hicho yatarekebishwa. Kikwete alianzisha mchakato wa kutafuta Katiba mpya katika kipindi chake cha pili na si kile cha kwanza kwa sababu hakutaka Katiba mpya itumike wakati wa utawala wake. Alikuwa anafikiria Katiba mpya ianze na rais anayemfuatia.

Inatarajiwa hata Rais John Magufuli hawezi au kuufufua ule mchakato wa Katiba wa Kikwete ama hata kuanzia wa kwake mwenyewe katika kipindi chake. Iwapo atafanya hivyo, basi itakuwa katika kipindi chake cha pili ili katiba mpya ianze na rais atakayefuatia.

Wachunguzi wengi wa mambo wanaona mchakato wa kupata Katiba mpya aliouanzisha Kikwete haukuwa wa dhati kwani alishindwa kuusimamia vyema, hasa pale alipoonekana kupinga mapendekezo ya wananchi ya mfumo wa muungano wa Serikali tatu.

Vilevile wanasema Tanzania ilipoteza fursa kubwa ya kubadili Katiba katika hali ya utulivu iliyopo nchini na kwamba tulishindwa kujifunza kwa yaliyotokea Kenya baada ya uchaguzi wao wa 2007.

Vurugu kubwa zilizofuatia ushindi wa utata mkubwa wa Mwai Kibaki zilipelekea juhudi za usuluhishi kufanyika zilizosaidiwa na nchi za jirani na Umoja wa Afrika (AU) na kukawekwa Serikali ya mpito chini ya Kibaki.

Katiba mpya ikaandaliwa ambayo ilikuwa na marekebisho makubwa hasa katika namna ya kuteua tume ya uchaguzi na kuendesha uchaguzi.