Home Makala Kimataifa
2753
0
SHARE
Sehemu ya bandari ya Beirut ulipotokea mlipuko

MWANDISHI WETU NA MASHIRIKA YA HABARI


WIKI hii inashuhudia hatua ambazo hazitarajiwi na wengi katika serikali nyingi duniani, ni suala la kujiuzulu kwa mawaziri kadhaa na kisha Waziri Mkuu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali kutangaza kujiuzulu na Serikali nzima aliyokuwa akiiongoza.

Mtiririko wa matukio tangu kulipotokea mlipuko wa moto ulioharibu Bandari ya Beirut nchini Lebanon, Jumanne Agosti 4 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 220 na kuwajeruhi wengine 6,000 huku wengi wakiwa hawajapatikana uanaibua maswali mengi.

Mlipuko huo unahusishwa na tani 2,750 za kemikali ya ammonium nitrate kwenye ghala moja katika bandari hiyo, unaleta fursa ya kuingia na kuangalia mpya mfumo na utawala wa Lebanon kwa sasa.

Ni kutokana na mlipuko huo, ulifuatiwa na msururu wa matukio ya kuilaumu Serikali na shinikizo la uwajibikaji, lililoanza kuwasukuma mawaziri kujiuzulu nyadhifa zao serikalini, akiwemo Waziri wa Sheria na Waziri wa Fedha, ambao wanakuwa mawaziri wa mwanzo kujiuzulu tangu ulipotokea mlipuko mkubwa mjini Beirut wiki iliyopita.

Waziri wa Sheria, Marie-Claude Najm, alieleza katika barua yake ya kujiuzulu kwamba uamuzi wake umetokana na mlipuko wa Beirut na maandamano.

Siku chache baadaye, Jumatatu Agosti 10 mwaka huu Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab anatangaza kujiuzulu kwa serikali yake, akisema mlipuko huo ulioutikisa mji wa Beirut hivi karibuni na kusababisha hasira ya umma ulitokana na ufisadi mkubwa.

“Leo tunafuata matakwa ya watu wa Lebanon ya kuwawajibisha wale waliohusika na maafa haya,” anasema waziri mkuu Diab katika hotuba yake wakati akitangaza kujiuzulu kwa serikali yake.

Anaongeza kuwa maafa hayo yametokana na mfumo wa ufisadi, huku akisema kuwa wale waliohusika wanapaswa kuona aibu kwa sababu, matendo yao yamesababisha janga kubwa lisiloweza kuelezeka.

Japokuwa Rais Michel Aoun anaikubali barua ya kujiuzulu ya Serikali ya Waziri Mkuu Diab iliyoundwa mwezi Januari na kuungwa mkono na kundi kubwa lililo na nguvu nchini humo linaloungwa mkono na Iran la Hizbolla na washirika wake, lakini ameiomba ibakie kuwa serikali ya muda au ya mpito hadi pale baraza jipya la mawaziri litakapoteuliwa.

Kulingana na mfumo wa serikali, Rais Aoun anatarajiwa kuwasiliana na wabunge kujua ni nani atakayekuwa waziri mkuu mpya na kisha kumpa nafasi hiyo mgombea atakayekuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wabunge.

Mgogoro wa kisiasa na kiuchumi huenda ukaufanya mchakato wa kumtafuta Waziri Mkuu kuwa mgumu zaidi.

Hii inatokana na ukweli kwamba hatua ya kujiuzulu kwa Diab ambaye aliteuliwa mwanzoni mwa mwaka huu baada ya mvutano wa muda mrefu na Serikali yake kunamuacha Rais Aoun katika umbwe la kiutawala.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab

Hatua ya Diab kujiuzulu inatafsiriwa kuwa ni ya masilahi zaidi ya kisiasa kwake na yenye nia ya kujisafisha dhidi ya ufisadi na rushwa, ambavyo amekuwa akidai wakati wote kuwa juhudi zake za kupambana na mambo hayo zimekuwa zikipata upinzani mkubwa, huenda kutoka kwa rais wa nchi hiyo.

Kuunda serikali wakati kukiwa na mivutano na migawanyiko imekuwa changamoto kubwa hapo awali, lakini kwa sasa kutokana na kuongezeka kwa mashaka na kutouamini utawala uliopo hasa kutokana na mlipuko wa hivi karibuni na kukua kwa mgogoro wa kisiasa huenda ikawa vigumu kumpata mgombea atakayetaka kuwa waziri mkuu.

Wakati hatua ya Diab ikinuiwa kujibu hasira za watu kuhusu mlipuko wa Beirut inaonekana pia kuitumbukiza zaidi Lebanon katika mgogoro wa kisiasa na inaweza kuathiri zaidi mazungumzo yaliyosimama kati ya taifa hilo na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusiana na mipango ya kuuokoa uchumi wa taifa hilo.

Mazungumzo hayo yalioanza Mei yalisitishwa kutokana na serikali kushindwa kutekeleza mabadiliko yaliyohitajika na mvutano uliokuwepo kati ya serikali hiyo na mabenki na wanasiasa juu ya kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo.

ADUI WA LEBANON NI SERIKALI

Tayari mlipuko huo wa Lebanon uliosukuma kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Diab na baraza lake la mawaziri umeibua maoni mbalimbali kuhusu uimara wa Serikali iliyokuwepo na namna ambavyo imekuwa ikibeba mambo ya nchi hiyo.

Wachambuzi wa siasa za Lebanon wamekuwa wakiangazia maeneo tofauti kuhusu utendaji wa Serikali, lakini sasa wanachukulia sababu za janga la hivi karibuni la mlipuko katika bandari ya mjini Beirut wakieleza kuwa zinahitaji kuchunguzwa, lakini sio na serikali hiyo bali taasisi za nje.

Kwa maoni yake, mwandishi wa DW Diana Hodali anaeleza kuwa Lebanon imepitia mengi, ikiwemo vita, mizozo na majanga, lakini kile kilichotokea hivi karibuni katika bandari ya Beirut kilishinda chochote kile ambacho raia wa nchi hiyo wangefikiria.

Anasema mlipuko huo uliharibu sehemu kubwa ya mji huo mkuu kusalia kuwa vifusi, kuwafanya watu zaidi ya 300,000 kupoteza makazi na kuondoa matumaini ya maisha bora ambayo yalifurahiwa hasa na vijana wadogo nchini humo.

Mkazi wa Beirut, Lebanon akiangalia mabaki ya makazi yake

Hodali anasema licha ya kila kitu ambacho kimetokea nchini humo hadi kufikia sasa, kushindwa kwa kiasi kikubwa kwa serikali ya nchi hiyo kutimiza majukumu yake kumezidisha hofu ya raia wa nchi hiyo.

Anasema kwa siku kadhaa sasa, shughuli ya kutafuta waliopotea katika mkasa huo imekuwa ikiendelea katika mji huo bila ya msaada wa serikali na hakuna hata msamaha uliotolewa na kundi la wanasiasa mashuhuri na pia hakuna aliyejiuzulu. Badala yake, serikali imekuwa ikipongeza ujasiri wa raia wa nchi hiyo.

“Ni wazi kwamba hakuna aliye madarakani anayejihisi kuhusika na ukweli kwamba kemikali ya Ammonia Naitreti yenye uwezo mkubwa wa kuripuka ilihifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita karibu na maeneo ambayo watu wanafanya kazi na kuishi katikati mwa mji huo. Badala yake wamewakamata baadhi ya maofisa wakuu wa bandari. Kama hali inavyokuwa kila kunapokuwa na matatizo nchini Lebanon, hakuna aliye madarakani anayelaumiwa.

“Lakini licha ya mitazamo mbali mbali ya watu, mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari hiyo ya Beirut ulitokana na ufisadi mkubwa katika serikali ya nchi hiyo. Kwa miaka kadhaa sasa, wanasiasa kutoka vyama vyote vya kisiasa wamekuwa wakipora nchi hiyo na kuisukuma katika matatizo. Hata wanasiasa wa upinzani, walishirikiana katika mfumo huo fisadi kujinufaisha. Inapofikia suala la maslahi, walikubaliana,” anasema.

MASAIBU

Hodali anasema janga hilo ni la hivi karibuni ni mfano unaotisha wa jinsi serikali moja hadi nyingine ya Lebanon zimeshindwa kutimiza majukumu yao ya kimsingi ambayo ni kuangalia maslahi ya wananchi.

Anasema kwa miaka kadhaa sasa, umeme umekuwa ukipotea kwa saa kadhaa kwa siku. Unaweza kujiuliza kwanini, na jibu ni kuwa wafanyabiashara matajiri ambao aidha wanatokea katika siasa ama kushirikiana kwa karibu nazo, hupata faida kila wakati watu wanapolipia umeme wa ziada.

Anasema mbali na hayo kuna mirundiko ya taka, wa miaka kadhaa, mirundiko mikubwa ya taka imekuwa ikiongezeka karibu na uwanja wa ndege, ambapo kumekuwa na bidhaa za plastiki zilizotapakaa karibu kila mahali katika fuo za bahari na uchafu wa kemikali haujakuwa ukitupwa kwa njia bora na kuhatarisha maisha ya watu.

Hodali ambaye amekuwa mfuatiliaji wa karibu wa siasa na maisha ya watu wa Lebanon anasema wakati mioto mibaya zaidi ya misitu ilipotokea mnamo Oktoba mwaka 2019, serikali haikuwa na ndege yoyote ya kukabiliana na moto kwa kuwa kuna mtu aliyesahau kuzishughulikia na kuzijaza mafuta lakini haijulikani alwiajibishwa vipi?

Anasmea mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe, raia wengi wa Lebanon wameshuhudia vita mara mbili na Israeli, mizozo kadhaa ya kiuchumi, viwango vikubwa vya ukosefu wa ajira na mauaji ya kisiasa.

Tangu Oktoba mwaka jana, waandamanaji wamekuwa wakitoa wito kwa wanasiasa mafisadi kujiuzulu. Hii  ni kwa sababu wale wanaoshikilia uongozi ni wababe wa kivita waliopigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kutafuta amani na kuendelea kujinufaisha na kuchochea ghasia katika misingi ya madhehebu.

Hodali anasema hadi pale mizizi ya matatizo nchini humo itakaposhughulikiwa na iwapo wababe hao wa kivita wataendelea kubaki madarakani, kuna tishio kwamba kwa mara nyingine, Lebanon itatumbukia katika mzozo.

KAULI YA MACRON

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ni miongoni mwa watu waliojitokeza baada ya kukutana na mwenzake wa Lebanon, Aoun pamoja na waziri mkuu aambaye kwa sasa amejiuzulu na Serikali yake, Diab katika makazi ya rais wa Lebanon na kutaka mageuzi ya haraka nchini humo.

Sasa taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na mzozo mbaya wa kiuchumi, linakabiliwa na changamoto ya kuujenga upya mji huo mkuu. Hata hivyo bado haiko wazi ni kiasi gani cha msaada utakaotolewa na jamii za kimataifa nchini humo.

Macron anazungumza na viongozi waandamizi wa Lebanon, ikiwa ni pamoja na rais Aoun kuhusu mustakabali wa taifa hilo akisema ziara hiyo ilikuwa ni fursa ya kuwa na majadiliano ya uwazi lakini magumu na viongozi wa kisiasa na wa kitaasisi wa Lebanon, baada ya kutembelea bandari iliyoharibiwa na mlipuko huo na kukutana na maofisa wa ngazi za juu.

Mandamano ya watu wa mji wa Beirut yaliyoshinikiza serikali kujiuzulu

Anasema, Ufaransa itashughulika na kuratibu misaada, lakini akionya kwamba iwapo hakutafanyika mageuzi, Lebanon itaendelea kuzama.

“Tutaleta chakula na vifaa ili kuyajenga upya makazi, lakini pia kinachotakiwa hapa ni mabadiliko makubwa ya kisiasa. Mlipuko huu unapaswa kuwa mwanzo wa enzi mpya. Hiki ndio kitu cha pekee kinachoweza kuleta mwanzo wa enzi mpya,” anasema Rais Macron.

Hata hivyo Macron anasema hakwenda pale kwa lengo la kuirekebisha serikali, na kuapa kwamba msaada ya Ufaransa hautaangukia mikononi mwa wala rushwa.

Mbali na Ufaransa, Lebanon imekataa msaada kutoka Israel, kutokana na kutokuwepo kwa mahusiano ya kidiplomasia baina ya mataifa hayo ambayo yako katika hali ya kivita, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi kati ya Israel na vuguvugu la Hezbollah la Kishia linaloungwa mkono na Iran katika eneo la mpakani.

UFADHILI

Rais wa Ufaransa, Macron pia anajivuika jukumu jingine la kusimamia ufadhili kwa kuwa mwenyeji wa mkutano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) na atashiriki Rais Donald Trump pamoja na wawakilishi wengine kutafuta msaada kwa Lebanon.

Macron anatarajia  kwamba ahadi zitakazotolewa  katika  mkutano huo  kwa  njia  ya  vidio, utakuwa mchango thabiti na  fedha  hizo  zitatumika kwa  uwazi  na  kwa  lengo lililokusudiwa.

“Pia  tutaweka uongozi wa wazi na sahihi  ili misaada  hii  yote , iwapo inatoka  Ufaransa ama  ya kimataifa, iweze kwenda  moja  kwa moja  kwa  watu, katika  asasi  za  kijamii na  timu katika  maeneo ambayo  yana  uhitaji, bila ya  uwezekano wa  kuhodhi  ama kupelekwa  mahali  ambako hakustahili,” anasema.

Anasema haja ya mageuzi  makubwa  yana maana na kwamba muda umewadia sasa wa uwajibikaji kwa Lebanon ya leo  na  viongozi wake, ambao wanahitaji makubaliano  mapya  na  watu  wa Lebanon katika  wiki zijazo.

Trump  akithibitisha  kushiriki kwake katika  mkutano  huo, aliandika katika  ukurasa wa Twitter kuwa “kila mmoja  anataka kusaidia!”

Chanzo  katika  ofisi  ya  rais  ya  Ufaransa ambacho  hakikutaka kutajwa  jina , kimesema  kuwa  Umoja  wa  Ulaya, Uingereza, China, Urusi, Jordan na  Misri zitawakilishwa, licha  ya  kuwa haikufahamika  mara  moja katika  ngazi gani. Israel, ambayo Lebanon  haina uhusiano  wa kidiplomasia nayo, haitarajiwi kushiriki.

Mataifa  muhimu  ya  Kirabu katika  eneo  la  ghuba, ikiwa  ni  pamoja na  saudi Arabia, Qatar na  Umoja  wa  falme  za  Kiarabu yanatarajiwa  kushiriki  lakini  Iran, ambayo  ina  ushawishi  mkubwa katika  Lebanon  kupitia kundi la  Kishia  la  Hezbollah, haijaonesha nia  ya kushiriki, ofisa  huyo  anasema.